Writen by
sadataley
3:32 PM
-
0
Comments

Askofu wa Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar/ Iringa. Askofu wa Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa amewataka wanasiasa nchini kuwaheshimu waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutokana na kazi kubwa waliyoifanya ya kuwasilisha maoni ya wananchi kwa uaminifu.
Akizungumza katika ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Albano Dar es Salaam, Askofu Mokiwa alisema baadhi ya watu wamekuwa wakilalamika kwamba waasisi wa Muungano wanakashifiwa, lakini haohao ndiyo wanaowatukana wajumbe wa Tume iliyokuwa inaongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Alisema Wajumbe wa Tume wanastahili shukurani kwa kazi waliyoifanya na kwamba wakitukanwa, hata wananchi waliotoa maoni pia wanakuwa wametukanwa.
Kuhusu kauli ya kwamba zikiundwa Serikali tatu jeshi litapindua nchi, alisema ni ya kichochezi na yenye lengo la kupandikiza chuki miongoni mwa wanajeshi wenye kuifahamu vizuri nchi yao.
Aliwataka wanajeshi kupuuzia kauli hiyo aliyosema haina busara kutoka kwa kiongozi wa Serikali mwenye ajenda yake binafsi.
Hivi karibuni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alikaririwa katika Kanisa la Methodist mjini Dodoma akisema Tanzania ikiwa na serikali tatu, jeshi litapindua nchi kwa sababu Serikali ya Muungano iliyopendekezwa haina vyanzo vya mapato kuwalipa mishahara yao.
Mahitaji ya wananchi
Katika hatua nyingine, maaskofu mbalimbali mkoani Iringa wamelitaka Bunge la Katiba kuzingatia mahitaji ya wananchi, ikiwa ni pamoja na kuwataka wajumbe wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurudi bungeni kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya.
Akitoa salamu za Sikukuu ya Pasaka kwenye Kanisa Kuu Iringa, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, Dk Owdenburg Mdegela aliwataka wajumbe wa Ukawa kurudi bungeni kuendelea na mjadala wa katiba na wasiende kwa wananchi kwa kuwa wameona kila kitu kinachoendelea bungeni.
“Ukawa warudi bungeni au wanyamaze kimya la sivyo tutaandamana nchi nzima tukipiga madebe na sufuria kuwapinga,” alisema.
Hata hivyo, alisema hana imani na Bunge la Katiba linaloendelea kwa kuwa linakwenda ovyoovyo na huenda likaleta katiba ya ovyoovyo.
Kwa upande wake, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki la Iringa alisema wajumbe wa Bunge la Katiba wanatakiwa kujadili masuala ya msingi kwa Watanzania ikiwamo umaskini, huduma za jamii na maendeleo.
“Hatujawatuma na kuwaagiza kwenda Dodoma kwa ajili ya kupata bahasha tu, bali mustakabali wa taifa na amani ya nchi bila kusahau maendeleo ya nchi,” alisema.
Askofu wa Makanisa ya Overcomes Iringa, Dk Boaz Sollo alimshauri Rais Jakaya Kikwete kuvunja Bunge la Katiba ili kulinda amani ya nchi.
Imeandikwa na Peter Elias (Dar), Geofrey Nyang’oro, Hakimu Mwafongo (Iringa).
No comments
Post a Comment