Writen by
sadataley
8:19 AM
-
0
Comments
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Dodoma. Kikao cha kwanza cha Bunge Maalumu la Katiba kinaanza leo mchana mjini hapa na kitaongozwa na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dk Thomas Kashililah na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad.
Kazi kubwa itakayofanywa leo ni wajumbe wa Bunge hilo kupewa miongozo.
Kikao hicho kitaanza kwa kumchagua mwenyekiti wa muda miongoni mwa wajumbe 629 wa Bunge hilo na kazi na yake kubwa itakuwa ni kuandaa kanuni ambazo zitatumika katika kumchagua mwenyekiti wa kudumu wa Bunge hilo na kuanzisha mchakato wa vikao vyake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk Kashililah alisema: “Mjumbe yeyote anayetaka kugombea uenyekiti wa muda nafasi ipo wazi. Anatakiwa kuchukua fomu kutoka kwa Katibu wa Bunge kuanzia leo (jana) saa sita mchana hadi kesho (leo) saa tano asubuhi. Mpaka kufika kesho (leo) saa nane mchana tutakuwa na majina yote,” alisema.
Alisema kila mgombea atatakiwa kuwa na wadhamini 10 kutoka miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo. Alisema kuanzia saa tatu asubuhi leo, wajumbe wa Bunge hilo wataelekezwa namna ya kuketi na kuutumia Ukumbi wa Bunge kabla ya kikao kitakachoanza saa 8:00 mchana.
“Uchaguzi wa mwenyekiti wa muda wa kikao unafanyika kwa sababu uchaguzi wa mwenyekiti wa kudumu na makamu wake hauwezi kufanyika bila kanuni zitakazoandaliwa na mwenyekiti wa muda,” alisema Kashililah na kuongeza: “Mimi na Khamis Hamad tutasimamia kazi ya uchaguzi wa mwenyekiti wa muda. Ila katika kikao cha kesho (leo) tutachagua mmoja kati ya wajumbe kwa ajili ya kukiongoza ili kumchagua huyo mwenyekiti wa muda. Sisi kikanuni hatuwezi kuongoza kikao,” alisema.
No comments
Post a Comment