Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Friday, February 28, 2014

Mwigulu amwaga ahadi kibao Kalenga

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kalenga kwa tiketi ya CCM, Godfrey Mgimwa (mwenye skafu shingoni) akisalimia wananchi baada ya kuwasili kwenye Kijiji cha Ifunda jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 
Na Hakimu Mwafongo na Zainabu Maeda, Mwananchi
Iringa. Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba jana alizindua kampeni za chama hicho katika Jimbo la Kalenga mkoani hapa kwa kumwaga ahadi za kuwapatia wananchi maji, umeme na mawasiliano ambayo ni changamoto katika jimbo hilo.
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, aliyasema hayo jana alipokuwa akihutubia uzinduzi huo uliofanyika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ifunda.
Aliwataka Wanakalenga kuacha kupotoshwa na maneno ya wagombea wengine kwa sababu hawana ridhaa, sifa ya kuwa viongozi wa jimbo hilo na wala hawana uwezo wa kuwaletea maendeleo.
Alisema endapo watamchagua mgombea wa CCM, Godfrey Mgimwa watashirikiana naye kupitia Ilani ya chama hicho kuhakikisha changamoto zote za jimbo hilo zinafanyiwa kazi na mengine mapya yanaongezeka kwa kipindi hiki cha miezi 22 iliyobaki hadi mwaka 2015.
“Nazungumza hili nikiwa kama Naibu Katibu Mkuu wa chama ila msisahau mimi pia ni Naibu Waziri wa Fedha. Nakuagiza Mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa andika matatizo yanayolikabili jimbo hili, chama kipeleke serikalini na wananchi watatuliwe kero zao,” alisema Mwigulu.
“Mpeni ridhaa mgombea wa CCM kwa kushirikiana na viongozi wa chama akiwamo Rais wetu ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, tutahakikisha tunayaendeleza mambo yaliyoachwa na marehemu mbunge wetu na kuyamaliza kabisa,” alisema na kuongeza:
“Wagombea wengine wanawadanganya, hawana nia nzuri na ninyi, msijaribu kuwapa upinzani kwani mtapata shida, mtumeni kijana Mgimwa awapelekee changamoto zenu zipatiwe ufumbuzi, mkichagua mgombea mwingine mnajichelewesha wenyewe.”
“Mchagueni mbunge atakayeenda bungeni kutetea bajeti. Wabunge walio wengi wakiwa bungeni kipindi cha kupitisha bajeti wanakataa kuunga mkono bajeti kwa sababu hawana mema na nyie, hawataki maendeleo ya wananchi ili waseme Serikali ya CCM haitekelezi.”
Alisema kati ya shughuli alizokuwa akizitekeleza aliyekuwa mbunge wa Kalenga, marehemu Dk William Mgimwa ni ujenzi wa barabara, hivyo kuwataka wananchi wamchague mgombea wa CCM ili waweze kushirikiana nao ili kuhakikisha kero inamalizika.
Mgimwa
Akizungumza katika mkutano huo, Mgimwa aliwaomba Wanakalenga kumchagua ili aweze kuungana na wabunge wengine kuwaletea maendeleo.
Alisema yupo tayari kuendeleza yote yaliyopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM na yaliyoachwa na baba yake, marehemu Dk Mgimwa, huku akiweka kipaumbele chake kuwa ni elimu hasa shule za msingi na sekondari, afya na ujenzi wa zahanati katika kila kijiji.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment