Writen by
sadataley
9:05 AM
-
0
Comments
Phillip Mangula alipoteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), niliandika uchambuzi nikirejea miujiza katika Biblia nikistaajabu miujiza ya kurejeshwa ulingo wa siasa baada ya kupotea.
Katika kitabu chake, Nabii Ezekieli Sura ya 37 anaandika kuhusu miujiza ya mifupa mikavu iliyotapakaa kondeni kuungana, kupata mishipa, uhai, pumzi ya uzima na kugeuka jeshi kubwa la Israel.
Leo simzungumzii Mangula kama mfupa mkavu uliopata uhai, bali nataka kuhoji kama atautafuna mfupa uliomshinda mwaka 2005 – kudhibiti wanaokiuka maadili katika harakati za kuwania uteuzi nafasi ya urais.
Kwa wenye kumbukumbu wanajua mambo yaliyomkuta Mangula wakati huo akiwa na wadhifa wa katibu mkuu wa CCM, kabla na baada ya mchakato wa kumtafuta na mgombea urais kupitia chama hicho.
Mangula alitumia nguvu kubwa bila mafanikio kusimamia uadilifu, miongozo, kanuni na katiba ya CCM kusimamia zoezi la uteuzi wa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi wa 2005.
Juhudi za Mangula kupitia Kamati ya Maadili ya wakati huo chini ya Mzee Paul Sozigwa na mwenzake Kanali Mstaafu Abdi Mhando haikufua dafu mbele ya wana-mtandao uliomwingiza madarakani Rais Jakaya Kikwete.
Kamati ya Sozigwa na Mhando ilielezwa kuwa na tuhuma, ushahidi na vielelezo vikiwamo vya picha za video na sauti kuhusu vitendo vya ukiukaji wa maadili vilivyodaiwa kufanywa na wanamtandao.
Kama inavyodaiwa hivi sasa, wanamtandao walianza maandalizi mapema kuhakikisha mgombea wao anateuliwa kupeperusha bendera ya CCM, na walifanikiwa bila vikwazo vyovyote.
Siyo hilo tu, wanamtandao walifanikiwa kuzuia taarifa ya Kamati ya Maadili ya akina Sozigwa kutumika kwenye vikao vya uteuzi, pia hata kubadili utaratibu wa kura tatu ndani ya NEC ukawa kura moja. Ilidaiwa kuwa taarifa hiyo ilibatizwa ‘eti majungu’.
Mfumo wa kawaida ya kura tatu kwa kila mjumbe, ungemwengua mapema Kikwete kwenye kinyang’anyiro baada ya wagombea wenzake waliomwona kuwa tishio kubainika kufunga fungate la kubebana.
Mwenyekiti wa wakati huo, Benjamin Mkapa akatangaza utaratibu wa kura moja kwenye kikao cha NEC, tofauti na mazoea ya kura tatu.
Jina la mgombea wa wanamtandao likapenya miongoni mwa matatu yaliyopita kwenda kupigiwa kura na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, na Kikwete kuibuka kidedea dhidi ya Dk Salim Ahamed Salim na Profesa Mark Mwandosya.
Yaliyomkuta Mzee Mangula baada ya ushindi wa wanamtandao sote tunayajua, hadi alipokumbukwa majuzi tena kuwa makamu mwenyekiti.
Itoshe tu kusema nafasi yake alikabidhiwa Yusuf Makamba huku yeye akirejea maisha yake ya ‘ujamaa na kujitegemea’ kijijini kwake akijishughulisha na kilimo cha viazi ulaya. Sozigwa na Mhando nao wakatupiwa virago kwa kosa kama lile la Mangula – kujaribu kuzuia wanamtandao kuingia Ikulu!
Mara hii, tena Mangula kakabidhiwa jukumu linalofanana kwa sura, mienendo na vitendo na lile la 2005. Kamati ya Mangula imewahoji wanaotajwa kuanza mbio za kuwania uteuzi nafasi ya urais. Miongoni mwa waliohoji waliomshinda Mangula akiwa katibu mkuu ndio hao anaotakiwa kuwadhibiti sasa akiwa makamu mwenyekiti akiongoza Kamati ya Maadili, katibu wake akiwa, Abdulrahaman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM.
Chanzo: www. mwananchi.co.tz
No comments
Post a Comment