Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, February 18, 2014

Bunge la Katiba vipande vipande

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakijiandikisha bungeni mjini Dodoma, ikiwa ni maandalizi ya kuanza kwa vikao vya bunge hilo. Picha na Silvan Kiwale 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba, linaanza leo mjini hapa, huku kukiwa na mpasuko mkubwa miongoni mwa wajumbe, unaotokana na misimamo tofauti.
Kipengele kinachowagawa wajumbe hao ni Muundo wa Serikali uliopendekezwa katika Rasimu ya Katiba.
Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, iliyokutana kwa siku mbili Mjini Dodoma imeondoka na msimamo wa kutaka wajumbe wake wa bunge hilo kutetea hoja ya Serikali mbili huku Chadema na CUF vinataka Serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila hivi karibuni alikaririwa akitishia kwenda mahakamani kuzuia mchakato mzima wa Katiba hadi iundwe Serikali ya Tanganyika.
Msimamo wa CCM
Akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya CCM Mjini Dodoma jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema msimamo wa chama chake haujabadilika na kwamba wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki na mfumo wa Serikali mbili.
“Hatuwezi kukataa mawazo ya watu wengine, lakini kikubwa ambacho tunakisimamia ni kuhakikisha kuwa tunabaki na Serikali mbili na ndiyo maana tumezungumza na wajumbe wa NEC na leo (jana), tunakutana na wabunge wetu wa Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,” alisema Nape.
Kuhusu kero zinazolalamikiwa na pande zote, alisema CCM inafahamu kero nyingi na kwamba upande wa Bara kuna kero nane na Zanzibar idadi kama hiyo.
“CCM imetengeneza mfumo mzuri wa kuziondoa kero hizo ndani ya Serikali mbili siyo kama wenzetu ambao wamebuni Serikali tatu eti iwe dawa ya kumaliza kero hizo kitu ambacho hakiwezekani,” alisema huku akiwataka wajumbe na Watanzania kwa jumla, kulumbana kwa hoja badala ya kupiga kelele.
Malecela aipinga CCM
Hata hivyo, kada mkongwe aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, John Malecela alitofautiana na msimamo huo akisema si sahihi kwa viongozi kuwatungia wananchi Katiba kama inayoonekana kufanywa na baadhi yao.
Akizungumza kwa simu kutoka Nairobi, Kenya, Malecela alisema: “Kama tuliona inafaa kuwatungia wananchi Katiba, hakuna ulazima wa kuwataka maoni yao. Mimi ni kiongozi na Katiba hii ni ya wananchi, nisingependa kutoa maelekezo ya nini kifanyike, kama viongozi wengine wanavyofanya.
“Ushauri wangu ni kwamba viongozi tusiwawekee wananchi misimamo. Tuwaache wafanye uamuzi kwa kuwa katiba hiyo ni yao.”
Mnyika ataka mawazo ya umma
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema anakusudia kuwasilisha mapendekezo kwamba ratiba ya Bunge ifanyiwe mabadiliko ili kuwe na kikao cha kusikiliza mawazo ya umma.
Alisema kwa kusikiliza mawazo hayo juu ya kanuni hizo, kutawezesha maoni ya Watanzania wengi kusikilizwa wakati wa maandalizi ya kanuni kabla ya Bunge kupitisha azimio la kuridhia kanuni hizo.
Pia alisema atawasilisha hoja kwa Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi ambao ndiyo waitishaji wa mkutano huo ili kanuni hizo zisitolewe kwa wajumbe wa Bunge hilo tu, bali ziwekwe pia kwenye tovuti za Bunge, Baraza la Wawakilishi.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, (Udomasa), Paul Losulite alisema anaamini kuwa mwafaka utapatikana katika majadiliano ya bunge hilo. “Wajadiliane lakini ifike sehemu wafahamu kuwa maoni ya wananchi lazima yaheshimiwe,” alisema.
Aliwataka wajumbe kukubaliana katika mambo yanayohusu masilahi ya taifa akisema si dhambi kutofautiana lakini ni vizuri kufikia mwafaka.
Chanzo:www.mwananchi.co.tz
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment