Writen by
sadataley
5:40 PM
-
0
Comments
Na Freddy Azzah na Fidelis Butahe, Mwananchi
Asema atakuwa wa mwisho kutoka kwa hiari yake, atoa majibu ya tuhuma sita
Dar es Salaam. Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe amesema kuwa hana mpango wa kujiondoa Chadema na kusisitiza kwamba atakuwa mtu wa mwisho kujitoa ndani ya chama hicho kwa hiari yake.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana katika mkutano aliouandaa kwa pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo, Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini alisema kwamba amekuwa mwanachama wa Chadema tangu akiwa na umri wa miaka 16 hivyo haiyumkiniki akikimbia chama hicho.
Zitto na Dk Kitila walivuliwa nyadhifa zao wiki iliyopita wakihutumiwa kukihujumu chama hicho.
“Kuna watu ambao walitegemea kuwa leo hii ningejibu mapigo, ‘ningezodoa,’ watu wengine kwa majina kama ilivyo kawaida kwa siasa za Tanzania. Natambua pia kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro kwa vyama hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza kinachoitwa ‘maamuzi magumu’,” alisema na kuongeza:
“Natambua kuwa wapo ambao wangependa kutumia nafasi zao kudhoofisha mapambano ya siasa za demokrasia nchini mwetu, napenda wanachama wa Chadema na wapenda demokrasia wote nchini watambue kuwa, mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa mwisho kutoka kwa hiari yangu.”
“Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka.”
Alisema kuwa atafuata taratibu zote za ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hilo.
“Mimi sitoki, wanaotaka nitoke, wanitoe wao,” alisema Zitto.
Zitto alisema Chadema ndicho chama kilichomlea na kumfikisha hapo alipo sasa, hivyo hata siku moja hatokuwa chanzo cha kuvunjika kwa chama hicho.
“Ningependa hata mtoto wangu akikua, awe pia mwanachama wa chama hiki, nimejiunga na chama hiki nikiwa na umri wa miaka 16 mpaka sasa nina miaka 37, nimetumia muda mrefu zaidi Chadema kuliko kipindi chote cha maisha yangu, Chadema ni kama maisha yangu, kukivunja chama hiki ni sawa na kujivunja mimi mwenyewe, kitu ambacho siwezi,” alisema Zitto.
Nyuma ya paziaZitto alisema sababu za kumvua uongozi zilizotolewa na chama ni waraka unaojulikana kama ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’.
“Waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama,” alisema na kuongeza:
“Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa.”
Tuhuma ya kwanza aliyoitaja Zitto ni ile ya kudaiwa kutokushiriki kumpigia kampeni mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Alisema tuhuma hiyo aliitolea ufafanuzi kuwa pamoja na kuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, alifanya kampeni kwenye majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwamo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa.
“Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais na kote nilipopita niliwapigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na urais,” alisema.
Tuhuma ya pili ni kwamba akiwa mkoani Kigoma alishindwa kuwapigia kampeni wagombea wengine wa Chadema na ndiyo maana ni yeye pekee aliyeshinda. Alisema siyo kweli, bali aliwapigia kampeni wagombea wote lakini kilichotokea ndiyo uliokuwa uamuzi wa wananchi wa Kigoma.
Zitto alisema tuhuma ya tatu iliyotolewa ni kushiriki kuwashawishi wagombea wa chama hicho katika baadhi ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa.
“Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho,” alisema.
Tuhuma nyingine ni kutokushiriki operesheni mbalimbali za chama. Alisema siyo kweli na ameshiriki karibu katika operesheni zote na hivi karibuni alikuwa kwenye operesheni za kujenga chama kwenye Mikoa ya Tabora na Katavi.
Tuhuma nyingine aliyosema ilichukua muda mrefu zaidi kujadiliwa na Kamati Kuu ni ile ya kutaka vyama vya siasa vikaguliwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Alisema baadhi ya wajumbe walitaka akitaarifu kwanza chama chake juu ya hatua hiyo kabla ya kuiweka hadharani.“Niliwaambia kuwa, utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC (Kamati ya Bunge Hesabu za Serikali) kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zilezile ambazo tunazipinga na tunapigania kuzibadilisha,” alisema.
Tuhuma ya mwisho ambayo aliitaja ni ile ya kukataa posho za vikao.
Alisema alikataa hizo posho tangu mwaka 2011 na ataendelea na msimamo huo kwani ni jambo ambalo lipo kwenye ilani ya chama hicho na kuwataka wabunge wengine wamuunge mkono.
Kuhusu waraka
Alisema licha ya kutokujua juu ya waraka huo, laiti kama angeufahamu kabla, angetekeleza mara moja yale yaliyo ndani ya waraka huo.
Alisema pia kuwa kwa sasa hajafanya uamuzi kama atagombea uenyekiti ndani ya chama hicho lakini wakati utakapofika na kama atashauriwa kufanya hivyo, atafuata taratibu za chama hicho.
No comments
Post a Comment