Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Saturday, November 23, 2013

Ngugi awashambulia wasomi barani Afrika

Mwanafasihi wa lugha za Kiafrika na Mtunzi wa vitabu, Profesa Ngugi waThiong’o akitoa mhadhara  katika Chuo Kikuu cha Dar es Saalam jana kuhusu wasomi na viongozi wa Kiafrika kukosa uzalendo wa kuzitumia lugha zao.Picha na Fidelis Felix 
Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Dar es Salaam. Nguli wa Fasihi za lugha za Kiafrika na mtunzi wa vitabu maarufu, Profesa Ngugi wa Thiong’o amewashukia wasomi na viongozi wa Kiafrika kwa kukosa uzalendo wa kuzitumia lugha zao na badala yake, kuzitukuza za kigeni.
Akihutubia katika Chuo Kikuu cha Dar es Saalam jana, kuhusu lugha za Kiafrika na Ulaya, aliwataja wasomi na viongozi wa Serikali kuwa ni majemadari wa Afrika walioshikwa mateka na adui wanaowalazimisha kufanya kila kitu wanachowaamuru.
Ngugi anayetarajiwa kutunukiwa shahada ya heshima na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo, alisema wasomi wa wakati wa uhuru wanatofautiana sana na wa sasa.
Alisema wasomi wa sasa wameacha misingi ya utamaduni wa Mwafrika na badala yake, wanatukuza wazungu.
“Ninaposema majemadari simaanishi Serikali pekee yake, ninamaanisha pia tabaka la wasomi na hakuna hata mmoja ambaye anaweza kusema hakuathirika,” alisema.
“Sasa inakuwaje kama wewe ni jemadari unaongoza wengine lakini mwenyewe umetekwa, utawapeleka wapi,” alihoji.
Alisema wakati nchi za Afrika zinapata uhuru, wasomi walitumia ujuzi wao katika Kiingereza kuziongezea umaarufu lugha zao, lakini Waafrika wa tabaka la baada ya uhuru, ambao baadhi yao wako serikalini, wamekuwa mateka wa lugha za Ulaya huku wakijivunia kuwa na majina ya kizungu.
Ngugi alisema inashangaza kuona Afrika inaendelea kuteswa chini ya ukoloni wa lugha na nchi ndogo za Ulaya.
Alisema kimsingi uhuru uliopatikana ni wa kukomboa miili pekee yake na kuacha ubongo ukiwa na fikra za kizungu.
“Kwa upande wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alikifanya Kiswahili kuwa na kwao baada ya kuwa na tabia ya kupenda kutoa hotuba zake kwa lugha hiyo, na kwamba kitendo chake cha kutafsiri kitabu cha Shake Spear na Mabepari wa Venisi kiliongeza umaarufu wa lugha hiyo duniani,” alisema.
Akitoa mfano alisema miaka kadhaa iliyopita Bunge la Kenya lilipiga marufuku matumizi ya lugha za kikabila zisizungumzwe katika maeneo rasmi, lakini sheria hiyo haikupitishwa baada ya rais kukataa kuitia saini.
Msomi huyo alisema siku zote lugha imekuwa uwanja wa vita baina ya utumwa na harakati za kujikomboa na kujipa uwezo.Akichangia mada hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Hamudi Majamba, alihoji sababu za Ngugi kuhimiza Waafrika kutumia lugha za kiafrika wakati Rais wa Kwanza wa Kenya, Hayati Jomo Kenyatta, alikuwa akihutubia wananchi wake kwa kutumia Kijaluo.
Hata hivyo, Ngugi alikanusha taarifa hizo.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment