
Watalaam wa Umoja wa Mataifa
Wataalam wa Umoja wa Mataifa wanaoshughulikia maswala ya silaha za maangamizi duniani OPCW wameanza kuharibu silaha za kemikali za Syria.Wiki iliyopita, wataalam hao waliwasili jijini Damascus kuanza zoezi hilo la kihistoria nchini humo baada ya makubaliano kati ya Marekani na Urusi kuhusu silaha hizo za kemikali ambazo serikali ya Damascus imeendelea kukashifiwa kutumia dhidi ya wapinzani.
Marekani inasema serikali ya rais wa Syria Bashar Al Assad inahitaji pongezi kwa kuanza kutekeleza azimio la kuharibu silaha zake za kemikali kama ilivyokubaliwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Serikali ya Syria imekuwa ikituhumiwa na serikali ya Marekani kutumia silaha za kemikali kuwashambulia wapinzani, madai ambayo serikali ya Damascus inakanusha.
Mwezi Agosti silaha za kemikali zilitumiwa katika ngome za wapinzani nje ya jiji la Damascus na kusababisha vifo ya maelfu ya raia wasiokuwa na hatia.
Marekani ilisitisha mpango wake wa kuishambulia Syria kijeshi mwezi uliopita baada ya kuafikiana na Urusi kuhusu mpango huu ambao ulikubaliwa na serikali ya rais Assad kusalimisha silaha zake za kemikali licha ya kuendelea kukanusha kuwa imekuwa ikitumia silaha hizo dhidi ya wapinzani.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya watu 100,000 wamepoteza maisha nchini Syria tangu kuanza kwa machafuko nchini humo miaka 2 iliyopita na pia kusababisha ya watu kukimbia makwao.
Wiki iliyopita Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio la kutaka serikali ya Syria kuruhusu msaada wa kibinadamu kuwafikia waathiriwa wa machafuko nchini humo.
No comments
Post a Comment