Writen by
sadataley
11:17 AM
-
0
Comments
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Viongozi wadai muswada huo unalenga kuviua badala ya kuviendeleza na kwamba, usubiri mabadiliko ya Katiba Mpya.
Dar es Salaam. Viongozi wa vyama vya siasa, wamepinga mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa yaliyowasilishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, wakidai yanalenga kuviua.
Pia, wamemtaka Jaji Mutungi kuachana na mapendekezo hayo kwa kile walichoita kuwa, huo ulikuwa mpango wa Msajili wa zamani, John Tendwa, ambaye hakutaka vyama hivyo vistawi.
Wakizungumza katika mkutano wao wa kwanza na Jaji Mtungi, viongozi hao wa vyama vya siasa, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Uenezi Chadema, John Mnyika, Mwenyekiti wa UPDP, Faham Dovutwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, walitaka muswada huo usijadiliwe hivi sasa na badala yake usubiri hadi itakapopatikana Katiba Mpya.
Mnyika alisema marekebisho hayo hayana tija wakati huu, ambao Watanzania wanasubiri Katiba Mpya.
“Katiba Mpya ndiyo sheria mama ambayo itaweka miongozo jinsi msajili wa vyama anatakiwa kupatikana na utaratibu wa kuendesha ofisi hiyo. Sasa kukimbilia kuleta mabadiliko ya sheria hiyo wakati huu haionekani kuleta maana yoyote,” alisema Mnyika.
Mtatiro alisema marekebisho hayo yamelenga kumpa nguvu msajili wa vyama vya siasa na kumfanya kuwa mwamuzi wa mwisho, badala ya kuwa mlezi wa vyama hivyo.
“Kwanza huwezi kuviwekea madaraja vyama maana havikai kileleni muda wote. Unakumbuka NCCR, CUF na TLP vilipata kuwa vyama vikubwa kabisa, sasa kila mtu anajua vilipo, lakini kuvipanga vyama katika madaraja ni kuvibagua,” alisema Dovutwa.
Naye Jaji Mutungi alisema dhana ya kufanya mkutano huo, ni kukusanya maoni yatakayosaidia kuleta mabadiliko makubwa kwenye ofisi yake. “Tusingekutana hapa hata haya maoni yenu nisingeyapata. lengo ni kuboresha na hii ni mara ya kwanza lakini tutaendelea kukutana,” alisema.
No comments
Post a Comment