Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Thursday, September 19, 2013

Katiba mwafaka 2015 inawezekana, lakini..

Katika kile kinachoonekana bayana kama kumaliza uvumi uliozagaa nchini kwamba Serikali ya Awamu ya Nne inajiandaa kubaki madarakani baada ya muda wake kumalizika mwaka 2015, Waziri anayeshughulikia masuala ya Katiba na Sheria, Mathias Chikawe ameibuka na kusema Rais Jakaya Kikwete hana mpango kabisa wa kuongeza muda wa uongozi wake baada ya kipindi chake kumalizika.
Tunadhani tamko hilo ni muhimu mno, hasa tukizingatia mashaka na wasiwasi uliowakumba wananchi wengi baada ya Bunge kupitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika mazingira ya kutatanisha na ya kutia shaka. Muswada huo ulipitishwa na wabunge wa CCM kwa misingi ya kiitikadi baada ya wenzao wa vyama vya upinzani kususia mjadala wa muswada huo na kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge.
Kinyume na ilivyotarajiwa na wengi, wabunge wa CCM waliobaki bungeni hawakuujadili muswada huo, bali walitumia fursa hiyo adhimu kuporomosha matusi ya nguoni, kuwabeza, kuwakejeli na kuwapiga vijembe wabunge wa upinzani kabla ya kukurupuka na kupiga kura ya kuupitisha muswada huo katika mazingira hayo ya aibu. Hivyo, uvumi ulioenea kwamba Rais Kikwete atabaki madarakani baada ya kuisha muda wake wa uongozi ulitokana na hali hiyo, kwamba muda uliobaki kabla ya mwaka 2015 hautoshi kupatikana kwa Katiba Mpya kutokana na makundi mengi kupinga muswada huo uliopitishwa na Bunge katika mazingira hasi tuliyoyataja.
Maana yake ni kuwa, hata kama Rais Kikwete atakubali kuegemea upande mmoja wa CCM na kuusaini muswada huo na kuwa sheria na hatimaye Rasimu ya Katiba kupitishwa na wajumbe wengi wa chama hicho watakaounda Bunge Maalumu la Katiba, bado makundi yanayopinga mchakato huo yatakwenda kwa wananchi na kuwashawishi kuikataa katika Kura ya Maoni mwaka ujao.
Maeneo ya muswada huo yanayopingwa na makundi mbalimbali ni mengi. Lakini baadhi tu ya mambo yanayopingwa ni: Wananchi wa Zanzibar kutoshirikishwa kikamilifu katika kutoa maoni; Serikali kuonekana kuandaa mkakati wenye mwelekeo wa kukibeba chama tawala; Kumpa Rais nafasi kubwa katika uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka katika asasi za kiraia; na suala la asilimia 72 ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kubeba wanasiasa ambao wengi watatoka katika chama hicho.
Matokeo yake ni kuiingiza nchi yetu katika zahama na maangamizi kama ilivyotokea nchini Kenya baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007. Baada wa wananchi wa Kenya kuikataa Rasimu ya Katiba katika Kura ya Maoni, nchi hiyo ililazimika kuingia katika Uchaguzi Mkuu kwa kutumia Katiba ya zamani iliyokuwa na upungufu mkubwa kama ilivyo Katiba yetu ya sasa ambayo inalalamikiwa na umma wa Watanzania.
Hivyo, hofu kubwa hivi sasa ni kuwa, iwapo Rais Kikwete atatia pamba masikioni na kukataa kutafuta mwafaka wa kitaifa kwa kusikiliza hoja za makundi yote katika nchi yetu, kitakachotokea ni uwezekano wa kutokea machafuko kwa kuingia katika uchaguzi katika mazingira yasiyokubalika. Uvumi wa Rais Kikwete kubaki madarakani baada ya mwaka 2015 ulitokana na dhana kwamba atahitaji muda zaidi kutafuta mwafaka wa kitaifa kabla ya kupata Rasimu ya Katiba Mpya itakayopigiwa Kura ya Maoni. Njia pekee ya kutuepusha na zahama ni Rais Kikwete kutafuta mwafaka wa kitaifa.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment