Writen by
sadataley
10:32 AM
-
0
Comments

Bagamoyo. Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa mara ya kwanza amezishukia hadharani Kamati zote za Kudumu za Bunge na kuzitaka kufanya kazi zake kwa uadilifu na kuacha kupokea bahasha ama rushwa.
Amesisitiza kwamba kama wabunge watashindwa kuwa waadilifu na wataendelea kupokea rushwa ‘bahasha’ wataiuza nchi.
“Naomba hizo bahasha zikome, kwa upande wetu kama zipo.”
Makinda aliyasema hayo jana mjini hapa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Bajeti yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Naamini mmenielewa na naomba tushirikiane katika hili, na kama ni ‘bahasha’ lazima ninyi ndio mtakuwa mnawashawishi wawape. Waheshimiwa nawaombeni sana, wabunge ndiyo watu pekee wanaoweza kujenga nchi hii na ndiyo tegemeo la wananchi.”
Kauli ya Spika Makinda inakuja ukiwa umepita takriban mwaka mmoja tangu Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, kueleza kuwa Kamati ya LAAC imekithiri kwa rushwa.
Baada ya Kafulila kutoa kauli hiyo, siku chache baadaye mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Badwel, alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kupokea rushwa ya Sh1 milioni.
Siku tano baada ya mbunge huyo kufikishwa mahakamni, wajumbe wa Kamati hiyo walianza kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
No comments
Post a Comment