Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Thursday, July 18, 2013

Salim: Mandela ni nuru ya dunia


Na George Njogopa 
Dar es Salaam. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk Salim Ahmed Salim amesema katika kipindi cha miaka saba alichofanya kazi na Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aligundua kuwa ni mtu muungwana na mwenye hisia kubwa kuhusu ubinadamu.
Dk Salim alisema jana katika mahojiano maalumu kuwa katika siku za mwanzo hakujiamini kufanya kazi na kiongozi huyo ambaye anatambuliwa kama nuru ya dunia.
Alisema alikutana kwa mara ya kwanza na Mandela Mjini Addis Ababa, Ethiopia mwaka 1990 alipokuwa mtendaji mkuu wa OAU ambapo Mandela alikatiza ziara yake ya Tanzania Mei, 1990 na kwenda Ethiopia kwa siku moja na kurejea tena nchini kuendelea na ziara yake.
“Kwanza niseme kwamba pamoja na kuwa wakati ule wa ubaguzi wa rangi sisi sote tulikuwa tukishiriki kuupinga, lakini moyoni mwangu sikuamini kama Mandela atakuja kutoka na hatimaye kuiunganisha Afrika Kusini.
“Sasa alipoachiliwa tu, nakumbuka alikuja Addis Ababa na ndipo nilipoanza kufanya naye kazi,” alisema Dk Salim, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.
Dk Salim alisema wakati wote, Mandela alionyesha kuwa ni mtu mwenye kuzingatia misingi ya haki za binadamu na kutoa sura ya matumaini kwa wale waliozungumza naye. “Nimebahatika kufanya naye kazi kwa karibu sana… nakumbuka hata tulipokutana Tunisia kwa ajili ya mkutano wa Afrika, wakati wote Mandela alionyesha sura ya kujali utu na ubinadamu.
“Kusema kweli Mandela ni mtu wa aina yake… alipitia mazingira magumu yaliyoambatana na mateso makubwa, lakini pamoja na yote hayo, alisimama na kuhubiri umoja uliofanikisha kujenga taifa la Afrika Kusini hadi leo,” alisema.
Akizungumzia namna Afrika inavyomkumbuka kiongozi huyo wa Afrika Kusini, Dk Salim alisema pamoja na kwamba ni vigumu kumpata kiongozi kama Mandela, Afrika bado ina nafasi ya kuyaendeleza yale mema yaliyofanywa na kiongozi huyo kwa manufaa ya kizazi cha baadaye.
“Ninachoweza kusema ni kwamba, si jambo rahisi kumpata kiongozi kama Mandela, ila tutambue kwamba kila awamu ina mazingira yake, pengine vijana wa sasa wamepata motisha kutokana na uongozi wa Mandela na hivyo wanaweza kuyaendeleza mawazo yake kwa mustakabali wa kizazi cha baadaye.”
Alisema Mandela ni kiongozi wa aina yake ambaye alifanikiwa kutoa ujumbe wa matumaini jambo ambalo limemfanya awe kama nuru duniani kote.
Alisema kitendo cha Mandela kukaa madarakani kwa muhula mmoja na kisha kupisha uongozi kwa mwanasiasa mwingine, ni fundisho kwa wanasiasa wa Afrika wanaopenda kung’ang’ania madaraka.
“Hii peke yake inatosha kutoa fundisho kwa viongozi wa Afrika kwamba urais siyo wa milele, unaweza kufanya kazi katika muda wako na kisha kuwapisha wengine, hivyo ndivyo Mandela anavyotufundisha,” alisema.
Akizungumzia uhusiano baina ya Tanzania na Afrika Kusini, Dk Salim alisema msimamo ulioonyeshwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyepinga hadharani utawala wa ubaguzi wa rangi uliiponza Tanzania katika duru za kimataifa.
Alisema pamoja na kuwa uamuzi wa Tanzania ulikuwa wa busara, ulikumbana na wingu la upinzani kutoka kwa baadhi ya mataifa ambayo yalikuwa yakitetea siasa za ubaguzi wa rangi kwa masilahi binafsi.
“Tusisahau hata sisi Tanzania tulikumbana na misukosuko kutokana na msimamo wetu wa kupinga ubaguzi wa rangi… lakini jambo la kushukuru ni kwamba matunda ya msimamo wetu sasa yamejidhihirisha,” alisema Dk Salim.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment