Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Friday, July 26, 2013

Kikwete: Atakayethubutu kuigusa Tanzania atakiona

Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakifyatua risasi baridi hewani kuomboleza vifo vya askari 101 waliofariki katika Vita ya Ukombozi Msumbiji (1970-1978), wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yaliyofanyika Naliendele Mjini Mtwara jana .Picha na Abdallah Bakari 
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ametuma ujumbe kwa wale wanaoitishia Tanzania. Amewaambia wakithubutu watakiona cha mtemakuni kama ilivyokuwa kwa Idd Amin wa Uganda.
Alisema mamlaka za ulinzi na usalama zilimdhibiti Amin alipofanya uvamizi katika ardhi ya Tanzania mwaka 1978 na kwamba hazitashindwa kufanya hivyo kwa mtu mwingine yeyote atakayechezea usalama wa nchi.
Wakati Rais akisema hayo, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange amewahakikishia wananchi kuwa wakati wote jeshi liko imara na kuwataka wasiogope lolote.
Viongozi hao walisema hayo jana katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa iliyofanyika katika Kambi ya Jeshi ya Kaboya iliyopo Muleba, Kagera.
“Sihitaji kusema tena, mmeshamsikia Mkuu wa Majeshi, atakayejaribu atakiona cha mtemakuni, laleni usingizi na msiwe na wasiwasi, msisikilize maneno ya mitaani,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Wakati wowote, saa yoyote tuko tayari kulinda nchi yetu. Hatuko tayari kuona amani inaharibika nchini, hatuwezi kuruhusu mtu yeyote kuimega au kuichezea nchi yetu kama alivyofanya Idd Amin.”
Katika siku za karibuni kumekuwa na kauli kadhaa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa nchi jirani ambazo zinatafsiriwa na wananchi kwamba ni za kuitisha Tanzania.
Jenerali Mwamunyange alisema jeshi wakati wote liko imara kuwalinda wananchi na nchi kwa jumla hivyo wasiogope...“Endeleeni na shughuli zenu na msiogope mtu yeyote, fanyeni kazi zenu bila wasiwasi.”
Huku akishangiliwa na mamia ya watu waliohudhuria maadhimisho hayo, Jenerali Mwamnyanye alisema yeyote atakayethubutu kuchezea usalama wa nchi atakiona cha mtema kuni.
Akizungumzia Siku ya Mashujaa, Rais Kikwete alisema ni siku ya kuwakumbuka mashujaa waliojitolea maisha yao wakati wa Vita ya Kagera kuilinda nchi yao ili iwe salama na yenye amani.
“Kuhakikisha usalama wa nchi kuna gharama yake kwani kuna wengine walikufa na wengine wakabaki na vilema kwa ajili ya hilo. Wale ambao wamebaki na wana matatizo lazima tuwaangalie vizuri na vile ambavyo havijafanyika tutavishughulikia kwani kutetea taifa ni kazi ngumu.”
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo, Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk Mohammed Shein, Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu ambao wote walipewa nafasi ya kuwasalimia wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment