Writen by
sadataley
8:18 AM
-
0
Comments
ASKOFU WA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA DAYOSISI YA IRINGA
DKT.O.M MDEGELLA
AZINDUZI WA USHARIKA WA NYAMHANGA
JIMBO LA KUSINI
MAGHARIBI(IHEMI)
1. HISTORIA YA USHARIKA
WA NYAMHANGA.
Bwana Yesu Asifiwe.
Tunawasalimu katika jina
la Mwokozi wetu Yesu Kristo.
Nyamhanga ilikuwa moja kati ya
Mitaa kumi na mbili (12) ya Usharika wa Ipogolo.
Msukumo wa kuanzishwa mtaa wa
Nyamhanga ulitokana na mara kwa mara Washarika kukosa huduma za kiroho hasa
nyakati za mvua nyingi ilikuwa vigumu
kwa wazee, wagonjwa na watoto kuvuka korongo lililopo kati ya Usharika wa
Ipogolo na eneo la Nyamhanga.
Mwanga ulianza kujitokeza pale mzee
wa kanisa Dauson Mbembe alipombatiza ubatizo wa dharura mgonjwa mahututi ndugu
Yohana Mnyihanga tarehe 12/10/1992.
Wakati huo Usharika ulikuwa
unaongozwa na Mwinjilisti Yona Kinganga (Kaimu Mchungaji) baada ya Mchg Sawike
kuhama.
Kutokana na tukio hilo kaimu
Mchungaji alimwomba aliyebatizwa (ndg. Yohana Myihana) nyumba yake itumike kwa
sala za asubuhi, alikubali na huduma hiyo ilikaanza tarehe 15/10/1992.
Huduma zingine ziliendelea kutolewa
Usharikani Ipogolo.
Kaimu Mchungaji alipoona maendeleo
ya sala za asubuhi zinaendelea vizuri,
aliwaruhusu Washarika waliokuwa wakiishi eneo la Nyamhanga kuanza maandalizi ya
kuanzisha mtaa ili huduma za kiroho ziweze kufanyika katika eneo hilo.
Mnamo mwaka 1993 sala za asubuhi zilihamia nyumbani kwa mzee
Mbwilo (Baba Tula ) kukiwa na washarika wanane (08) chini ya uongozi wa mzee wa
kanisa Ndugu Dauson Mbembe.
Uongozi wa maandalizi ya Mtaa huo
ulibuni mbinu mbalimbali za kuanzisha Mtaa ikiwa ni pamoja na:-
-
Kuanzishwa kwaya ya Upendo ambayo
inaendelea na uimbaji
hadi sasa.
-
Kuwa na minada
ya aina mbalimbali.
-
Kuanzisha
Uinjilisti wa nyumba kwa nyumba siku za
Jumanne na Mikesha ya mara kwa mara.
-
Kuundwa kwa kamati ya majengo.
Kwa kutumia mbinu tajwa hapo
juu tarehe 13/8/1993 tulifanikiwa
kununua kiwanja chenye ukubwa wa robo tatu eka (3/4) toka kwa mzee Pauli Kanuru
kwa Tsh elfu tatu (3,000).Hatua hii ya kupata
kiwanja iliwasukuma washarika kuanza kukusanya mawe kwa ajili ya ujenzi wa
kanisa.
Kiwanja hicho kipo mwambao wa
daraja la Cagrielo, hakijapimwa na
kinatumika kama shamba la
viongozi wa kanisa.
Mnamo mwaka 1994 chini ya Mwenyekiti wa majengo Ndugu Awarywa Nnko
tulipata kiwanja kilichopimwa.
Kutokana na kupatikana kwa kiwanja
hicho uongozi uliamua kanisa lijengwe
katika kiwanja hicho, ndipo washarika walipoanza shughuli za ufyatuaji wa
matofali. Tunamshukuru Mungu kwa
kuwatumia watumishi wake Ndugu Awarywa Nnko na Ndugu Chua kusimamia usombaji wa
kuni za kuchomea matofali kwa trekta lililotolewa na Shirika la kilimo (EEC).
Trekta hili lilitumiwa pia kipindi
hicho kusomba matofali ya awamu ya kwanza. Kazi ya ufyatuaji na uchomaji wa matofali
ya awamu ya pili zilifanyika mnamo mwaka 1995. Kutokana na mzee Mbwilo kuhamia
Makete sala za asubuhi zilihamishiwa nyumbani
kwa mzee Dauson
Mbembe kuanzia tarehe 14/7/1995.
Katika kipindi hiki Uongozi uliomba
huduma ya shule ya Jumapili (Sunday School)
ianze, uongozi wa Usharika ulikubali na watoto walianza ibada za Shule ya
Jumapili tarehe 19/10/1996.
Kazi ya ujenzi wa kanisa ilianza rasmi tarehe 26/9/1996.
Ili kufanikisha ujenzi wa kanisa zilibuniwa mbinu au njia mbalimbali
zikiwemo:-
-
Kuanzisha mgahawa.
-
Bahati na sibu
iliyotupatia Tsh laki mbili na elfu hamsini (250,000)
-
Wahisani R.C Ipogolo
walitupatia Tsh elfu ishirini (20,000).
-
Harambee
iliyoongozwa na Mchg Agness Kulanga ilitupatia Tsh laki moja elfu
thelathini (130,000).
-
Makanisa
rafiki wa Usharika wa Ipogolo toka Augustana Marekani walitupatia bati sitini (60)
gage 28.
Kutokana na Ndugu Awarywa Nnko kupata uhamisho wa kikazi mwaka 1997, Ndugu Mathew
Mlangi alichaguliwa kushika nafasi ya Mwenyekiti wa Majengo.
Ndugu Mathew Mlangi alisimamia
kamati hiyo ya Majengo, awamu ya pili ya usombaji wa tofali kwa ajili ya ujenzi
wa kanisa.
Ndugu Mathew Mlangi alienda masomoni nje ya nchi, na ndg Henry Mwaipopo
alichaguliwa kuchukua nafasi ya uwenyekiti wa majengo, Ili kuharakisha ujenzi
wa kanisa unaendelea bila kukwama.
Wakati ujenzi wa Kanisa unaendelea, Uongozi uliamua, ibada za shule ya Jumapili pamoja na
mazoezi ya uimbaji yafanyike kwenye jengo la kanisa lililokuwa linaendelea
kujengwa (pagale).
Uongozi wa Mtaa wakati huo ulipata changa moto nyingi kutoka kwa wamiliki
wa kiwanja cha kanisa. Kanisa lililazimika kulipa fidia ya Tsh elfu ishirini na
tano (25,000) kwa wamiliki wa eneo hilo kwa ajili ya vitindi na mlimao kama
ilivyoamuliwa na ofisi ya
Kata ya Kitwiru.
Tunamshukuru sana Mungu kupitia kwa msaidizi wa Askofu wakati huo Mchg Dr
Richard Lubava na aliyekuwa Mchg wa Usharika wa Ipogolo Mchg Lusungu Msigwa waliweza
kuishawishi ofisi ya bega kwa bega ambayo ilitupatia Tsh Milioni tatu laki nne
elfu kumi tatu na mia nne (3,413,400), saruji mifuko mia moja (100), mbao mia
moja (100), chokaa mifuko miwili (02) na waya za “Ringbeam”.
Mchango huu pamoja na michango ya washarika ilifanikisha kazi ya ujenzi wa kanisa
kukamilika kuta, kupaua na kuchonga milango.
Shughuli hizi zilifanyika chini ya usimamizi wa mwenyekiti wa majengo Ndugu
Henry Mwaipopo na mzee wa kanisa ndugu Dauson Mbembe.
Kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa
kanisa tarehe 11/8/2002 ibada zote zilianza kufanyika yamhanga na ukawa mtaa
unaojitegemea chini ya uongozi wa mzee wa kanisa Ndugu Dauson Mbembe, kukiwa na
waumini sabini na mbili (72).
Huduma ziliendelea chini ya mzee wa kanisa Ndugu Dauson Mbembe hadi tarehe 30/11/2002 Mtaa ulipopata
mwinjilisti, Regina Kibasa. Mtaa ulipopata mwinjilisti, washarika walipata
hamasa, na mikakati ya maandalizi ya kuchonga mabenchi, kutengeneza samani za
ofisi, kuingiza umeme na maji zilianza.
Michango
ya washarika wa Mtaa huu, pamoja na
minada ya ndani
kazi zote hizo zilikamilika.
Baada ya Mtaa kukamilisha kazi zilizotajwa hapo juu, lilijitokeza wazo la
kujenga nyumba ya mtumishi.
Washarika wa Mtaa huu, kwa michango yao na nguvu kazi wakishirikiana na
vijana ishirini na moja (21) toka Usharika wa
Augustana Marekani walifanikiwa
kukamilisha kazi ya kujenga Msingi wa nyumba ya mtumishi.
Mnamo
mwaka 2004, uongozi wa
Mtaa uliandaa harambee, na Baba Askofu DKT Owdenburg
Moses Mdegella ukiwa mgeni rasmi katika harambee hiyo kwa lengo la kuhamasisha.
Waalikwa wengine walikuwa, Kwaya kuu toka Usharika wa Kanisa Kuu, viongozi wa kanisa pamoja na viongozi wa Serikali, ndugu
na marafiki.
Harambee hii ilichangisha kiasi cha Tsh
laki nane themanini na mbili elfu na mia tatu (882,300/=). Kiasi
kilichopatikana katika harambee hiyo kiliwezesha
kukamilisha kazi ya ujenzi wa kuta, kupaua, Milango, kupiga plasta ndani.
Kazi hii ya ujenzi ilifanyika chini ya
uongozi wa Mwilisti wa mtaa Regina Kibasa, wachungaji wa Usharika wa Ipogolo, Mchg
Abass Tagamtwa na Mchg Nixon Mwitula.
Jengo la kanisa pamoja na nyumba ya mtumishi zilizinduliwa
rasmi na Baba Askofu DKT Owdenburg Moses Mdegella tarehe 21/06/2009.
Mtaa wa Nyamhanga hadi kupata hadhi ya kuwa Usharika umeongozwa na watumishi hawa
wafuatao:-
1. Mzee wa
kanisa Dauson Mbembe 11/08/2012
– 30/11/2011
2. Mwinjilisti
Regina Kibasa 30/12/2002 – 30/11/2009
3. Shemasi
Regina Kibasa 01/11/2009
– 14/12/2009
4. Shemasi
Gaitan Mkemwa 15/12/2009
– 20/09/2011
5. Mwinjilisti
Aneth Mkongwa 2009
– Hadi sasa ni Mwinjilisti wa
Mtaa
wa Stesheni
6. Mchg Nuru
Makweta -20/9/2011 hadi sasa ni Mchg
kiongozi wa Usharika huu mpya.
Makatibu waliotumika hadi kupata Usharika
ni hawa wafuatao:-
1. Vicky Motto
- 2002
2. Mathias .B. Masele – 2002
- 2006
3. Noel Chengula - 2006-Hadi sasa ni Katibu/Mtunza Hazina wa
Usharika.
Tunamshukuru Mungu kwa kufanikisha
upatikanaji wa viwanja vinavyoungana na
eneo la kanisa. Viwanja hivi
vilipatikana baada ya kanisa kulipa fidia ya Tsh Milioni saba laki moja na nne
elfu mia tisa hamsini (7,104,950/=) kwa
waliokuwa wamiliki wa viwanja hivyo tarehe 04/02/2012.
Tunawapongeza Wazee
wa kanisa, Kamati ya majengo,Kamati
ya ununuzi wa viwanja pamoja na wote
walioshiriki katika kufanikisha upatikanaji wa viwanja hivyo.
Imeandaliwa na: KAMATI
YA MAANDALIZI YA UFUNGUZI WA USHARIKA WA
NYAMHANGA:
Tarehe: 12/05/2013
2. RISALA
Baba Askofu wa Dayosisi ya Iringa. Msaidizi wa Askofu.
Katibu Mkuu, Wakuu wa Majimbo, Wachungaji Wote, Viongozi wa Serikari na Waumini
wote mliohudhuria katika ibada hii,
“ BWANA YESU
ASIFIWE”
Baba Askofu.
Kwa niaba ya Washarika wa Usharika Mpya wa Nyamhanga,
ambao baada ya muda mfupi ujao utaufungua, awali ya yote napenda kutoa
shukurani zangu za dhati, kwanza kwako wewe Baba Askofu, Msaidizi wa Askofu,
Katibu Mkuu, Wakuu wa majimbo, Viongozi wa Serikali na wote mliohudhuria katika
ibada hii, kwa kumshukuru Mungu kutufikisha
siku ya leo.
Pia napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa Washarika
wote wa Usharika wa Ipogolo na Wachungaji wote waliohudumu katika Usharika huo
kwa kuuongoza Mtaa wa Nyamhanga hadi kufikia kuwa Usharika, na leo Baba Askofu
utaufungua rasmi.
Ningependa Kuwataja
Wachungaji waliohudumu katika Usharika wa Ipogolo, Nyamhanga ukiwa moja
wa Mitaa ya Usharika huo. Wachungaji hao ni hawa wafuatao:-
(1)
Mchungaji Agness Kulanga na msaidizi wake Mchg. Aleki
Mhanga
(2)
Mchungaji Damian Ngandango
(3)
Mchungaji Lusungu Msigwa
(4)
Mchungaji Abbas Tagamtwa
(5)
Mchungaji Nixon Mwitula (Mchungaji Kiongozi wa Usharika
wa Ipogolo hadi sasa) na wasaidizi wake wafuatao;- Mchg. Lunyiliko Muhile,
Shemasi Gaitan Mkemwa, Mchg. Lucrecia Mbwilo, na Mchg. Nuru Makweta.
Wote hawa wamefanya kazi kubwa katika kuufikisha Mtaa wa
Nyamhanga kuwa Usharika.
Baba Askofu, Mtaa wa Nyamhanga ulianza tarehe 11/08/2002 kwa juhudi za Waumini wa
Mtaa huo kwa kushirikiana na Usharika wa Ipogolo.
Wakati Mtaa ulipoanza ulikuwa na Washarika 72, Washarika
wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku na kufikia Washarika 1,180 hadi Mtaa ulipofikia kupewa hadhi ya Usharika Mwezi
Januari, 2013.
Baba Askofu, kuanzishwa kwa Mtaa wa Nyamhanga ilitokana
na Waumini wa Mtaa wa huo na wakazi wa eneo hili kutaka kusogezewa huduma ya
Kiroho katika eneo lao, kutokana na kikwazo cha Korongo lililoko kati ya eneo
la Nyamhanga na Usharika wa Ipogolo kujaa maji wakati wa masika, Waumini wa
eneo la Nyamhanga ilikuwa tatizo kwao kuvuka Korongo hilo na kwenda Ipogolo
kuhudhuria Ibada,
Baba Askofu, Usharika huu wa Nyamhanga utakaoufungua leo,
umetokana na Usharika wa Ipogolo, Nyamhanga ukiwa Mtaa moja wapo wa Mitaa kumi na mbili (12) ya Usharika huo wa
Ipogolo.
Usharika wa Nyamhanga una Mitaa saba (7), Waumini 1,180,
watu wazima ni Waumini 703, kati ya hao, Wanaume ni 266 , na Wanawake ni 439.
Watoto jumla yao ni 485,
Wanaume ni 210, na Wanawake ni 275,
Baba Askofu, Usharika wa Nyamhanga una Mitaa Saba (7) kama nilivyokwisha eleza hapo
awali, Mitaa hiyo ni:-
(1) Mtaa wa Stesheni – Nyamhanga una waumini
528
(2) Mtaa wa
Kitwiru - 174
(3) Mtaa wa
Kibwabwa - 125
(4) Mtaa wa
Lugala - 221
(5) Mtaa wa
Mseke - 65
(6)
Mtaa wa Mosi - 11
(7) Mtaa wa
Isimila – 56
Katika Mitaa hiyo Saba
(7), Mitaa Mitatu (3) ni Mitaa
ya Mission, Mitaa hiyo ni ifutatayo:-
(1)
Mtaa wa Mseke
(2)
Mtaa wa Mosi
(3)
Mtaa wa Isimila
Baba Askofu, Usharika huu Mpya wa Nyamhanga una
Wachungaji Wawili:
(1)
Mchungaji Nuru Makweta – Ambae ni Mchungaji Kiongozi
(2)
Mchungaji Lunyiliko Muhile
Baba Askofu, ninakuahidi kuwa mimi na Mchungaji mwenzangu,
tutashirikiana na Waumini wote katika kuifanya kazi ya BWANA katika eneo hili la Usharika huu.
Kufunguliwa kwa Usharika huu wa Nyamhanga, kutaimarisha
kueneza neno la Mungu na huduma yake katika eneo hili.
Pili, ni wajibu wa Usharika huu, nikiwa na maana ya
Viongozi, Wahudumu na Watenda kazi wote wa Usarika huu wa Nyamhanga kuitangaza
Injili kwa watu wote.
Baba Askofu, Usharika wa Nyamhanga pia una Mipango Kazi
Kama ifuatavyo:-
(1) Kazi ya Kiroho:
Kazi kubwa iliyooko mbele yetu ni
pamoja na;-
(a)
Kueneza neno la Mungu katika eneo la usharika wa Nyamhanga
(b)
Kushirikiana na Viongozi, Wahudumu na Watenda kazi wote
wa Usharika katika kuitangaza Injili kwa watu wote, ili waweze kuokolewa kwalo
na kumtumikia Mungu.
(c)
Kufanya Uinjilisti wa nyumba kwa nyumba katika eneo hili
la Usharika’
(d)
Kuimasha na kuendeleza Sel – groups
(e)
Kuandaa semina za neno la Mungu
(f)
Kuandaa Mikutano ya Injili
(g)
Kusomesha Wachungaji na Wainjilisti
(h)
Tuna Mipango ya Kutembelea Sharika mbalimbali katika
Dayosisi ya Iringa na nje ya Dayosisi kwa kutumia kwaya za Usharika wetu,
katika kueneza Injili na pia kujifunza kutoka kwao.
(i)
Kuimarisha huduma za Maombi.
Neno linasema,
“BWANA ASIPOIJENGA NYUMBA,
WAIJENGAO WAFANYA
KAZI BURE,
BWANA ASIPOULINDA MJI YEYE AULINDAYE AKESHA
BURE”
(Zaburi
127: 1)
(2) Kazi za Kiuchumi:
Ili kazi ya Kiroho iweze kupata msukumo wa kwenda mbele, tuna Mipango
Mkakati ya kazi za Kiuchumi kama ifuatavyo:-
(a)
Kujenga ukumbi
(b) Kujenga Shule ya watoto wadogo (Kindergarten)
(c) Kujenga Hostel
(d)
Kuendeleza Mradi wa upandaji Miti katika shamba lililopo
Lugala
(e)
Tuna mpango wa kujenga Maduka ya Biashara kuzunguka eneo
la Kanisa
(f)
Pia tuna Mpango wa ujenzi wa shule ya Ufundi
Mipango hii yote ni endelevu ( Mipango
ya muda mrefu).
Baba Askofu,
Mahali popote pale
hapakosi changamoto:
Usharika wetu kwa kuwa ndiyo unaanza, tuna changamoto
zifuatazo:-
(1)
Usharika una changamoto kubwa ya usafiri, hatuna chombo
cha usafiri kwa
ajili ya kuifikia Mitaa yetu ambayo
ipo mbali kutoka Makao makuu ya usharika, pamoja na kufanya shughuli zingine za
kila siku.
(2)
Tuna upungufu wa Majengo kwa ajili ya ofisi za idara
mbali mbali katika
Usharika
wetu.
Baba Askofu,
Kwa heshima
nakuomba, karibu ufungue rasmi usharika
wa Nyamhanga leo tarehe 12/05/2013.
“BWANA YESU ASIFIWE”
AMEN
NURU MAKWETA
MCHUNGAJI KIONGOZI – USHARIKA WA
NYAMHANGA,
No comments
Post a Comment