Writen by
sadataley
5:58 PM
-
0
Comments
UJUMBE WA PAPA BENEDICT XVI KWA AJILI YA SIKU YA 45 YA MAWASILIANO DUNIANI
Ukweli, Utangazaji Injili na Uhalisi wa Maisha katika Zama za Digitali
5 Juni, 2011
Wapendwa Kaka na Dada,
Katika kuadhimisha Siku ya 45 ya Mawasiliano Duniani, ningependa kushirikishana nanyi fikira kadhaa ambazo zinamotishwa na jambo ambalo linatawala wakati huu wa sasa: kuibuka kwa mtandao wa mawasiliano kikompyuta (internet) kama mtandao kwa ajili ya mawasiliano. Ni maoni ambayo katika hali ya kawaida yanaaminika kwamba, kama vile ilivyokuwa wakati wa Mapinduzi ya Viwanda ambapo yalileta mabadiliko makubwa katika jamii kwa mageuzi yaliyoanzishwa na mapinduzi hayo katika sekta za uzalishaji na katika maisha ya wafanyakazi, hivyo leo mabadiliko makubwa yanayoendelea katika mawasiliano yanaongoza maendeleo muhimu ya kiutamaduni na kijamii. Teknolojia mbalimbali za kisasa hazibadilishi tu namna tunavyowasiliana, lakini pia mawasiliano yenyewe, ili kwamba ijulikane kuwa tunaishi katika kipindi cha mabadiliko makubwa ya kiutamaduni. Njia hii ya kueneza taarifa na maarifa inazaa njia mpya ya kujifunza na kufikiri, kwa fursa zisizotarajiwa za kuanzisha mahusiano na kujenga ushirika.
Matarajio mapya sasa yamefunguliwa ambayo mpaka hivi karibuni isingewezekana kuyafikiria; yanaamsha shaka juu ya uwezekano unaotolewa na vyombo hivi vipya vya mawasiliano na wakati huohuo, vikihitaji tafakari makini juu ya umuhimu wa mawasiliano katika zama za digitali. Hili hasa linaonekana pale tunapokabiliwa na uwezo tarajiwa usio wa kawaida wa intaneti na utata wa matumizi yake. Kama ilivyo kwa kila zao jingine la ubunifu wa kibinadamu, teknolojia mpya za mawasiliano lazima ziwe ni kwa ajili ya kuhudumia ule wema hasa ulio ndani ya mtu mmoja na binadamu wote. Endapo teknolojia hizi zitatumika kwa busara zinaweza kuchangia kutosheleza nia ya kutafuta maana, ukweli na umoja ambavyo vinabaki kuwa shauku za ndani kabisa za kila binadamu.
Katika ulimwengu wa digitali, kusafirisha taarifa kunazidi kumaanisha kuifanya taarifa hiyo ifahamike ndani ya mtandao wa kijamii ambamo maarifa ni ya kushirikishana katika ngazi ya watu binafsi kubadilishana taarifa. Ubainishaji wazi wa tofauti kati ya mzalishaji na mtumiaji wa taarifa unakuwa na matazamo tofauti kati ya mtoa taarifa na mpokeji na mawasiliano yanaonekana sio tu kama mabadilishano ya habari, bali pia kama aina ya ushirikishanaji. Mabadiliko haya yamechangia kuleta utambuzi mpya wa mawasiliano yenyewe, ambayo yanaonekana kwanza kabisa kama mazungumzo, mabadilishano, mshikamano na uundaji wa mahusiano mazuri. Kwa upande mwingine, hili linazuiwa na mipaka hasa ya mawasiliano ya digitali: maingiliano ya upande mmoja, mwelekeo wa mtu kuonesha tu sehemu ya mambo ya ndani ya mtu mwenyewe, hatari ya mtu kujenga taswira yake potofu, ambayo inaweza kuwa aina fulani ya kujipendelea.
Vijana ndio hasa wanaokumbana na mabadiliko haya katika mawasiliano pamoja na fadhaa, changamoto na ubunifu ambao hasa unawahusu wale wenye hamasa na udadisi ili kukutana na mang’amuzi mapya katika maisha. Kupenda kwao kila wakati kushiriki katika jukwaa la digitali, linalotengenezwa na ile inayoitwa mitandao ya kijamii, kunasaidia kuanzisha aina mpya za uhusiano baina ya watu binafsi, kunaathiri kuwa na utambuzi binafsi na hivyo kuzua maswali sio tu ya namna ya kuchukua hatua sahihi, lakini pia kuhusu ukweli wa maisha ya mtu. Kuingia katika mitandao ya mawasiliano kunaweza kuwa ishara ya utafutaji halali wa kukutana binafsi na watu wengine, ili mradi umakini uwepo ili kuepuka hatari kama vile kujifungia katika aina ya maisha sambamba, au kuzama kupita kiasi katika ulimwengu usiogusika. Katika kutafuta kushirikishana na “marafiki”, kuna changamoto ya kuwa wakweli na waaminifu, na sio kukubali upotofu wa kujenga sura binafsi ya bandia mbele ya umma.
Teknolojia mpya huruhusu watu kukutana kupita mipaka ya mahali na utamaduni wao binafsi, kwa njia hii kutengeneza ulimwengu mpya kabisa wa aina za urafiki ambazo zinawezekana. Hii ni fursa kubwa, bali pia inataka umakini na utambuzi mkubwa wa hatari zinazoweza kutokea. Nani ni “jirani” yangu katika ulimwengu huu? Je kuna hatari iliyopo kwamba tunaweza kuwepo kidogo kwa wale tunaokutana nao katika maisha yetu ya kila siku? Je kuna hatari ya kuondolewa zaidi katika lengo kwa sababu umakini umekosekana na kuzama katika ulimwengu “mwingine” zaidi ya ule tunaoishi? Je tunao muda wa kutafakari kikamilifu juu ya chaguo zetu na kukuza uhusiano hasa ambao ni wa kina na wakudumu? Daima ni muhimu kukumbuka kwamba mawasiliano kimtandao hayawezi na sio lazima kuchukua nafasi ya mawasiliano ya moja kwa moja ya kibinadamu na watu katika kila hatua ya maisha yetu.
Pia katika zama za digitali, kila mmoja anakabiliwa na hitaji la uhalisi na tafakari. Licha, ya mabadiliko yaliyomo katika mitandao ya kijamii yaoneshayo kwamba daima mtu anashiriki katika kile ambacho anawasiliana. Wakati watu wanapobadilishana taarifa, tayari wanakuwa wamekwisha kujishirikisha wenyewe, namna wanavyoutazama ulimwengu, matumaini yao,na kanuni zao. Inamaanisha kwamba kuna njia ya Kikristo ya kuwepo katika ulimwengu wa digitali: Hili linachukua aina ya mawasiliano ambayo ni sahihi na wazi, yenye kuwajibika na kuheshimu wengine. Kutangaza Injili kwa kutumia vyombo vipya vya mawasiliano kunamaanisha sio tu kuingiza maudhui dhahiri ya kidini katika majukwaa mbalimbali ya vyombo vya habari, bali pia kuendelea kushuhudia kikamilifu, katika maelezo binafsi ya kidigitali na kwa namna mtu anavyowasilishachaguo zake, mapendeleo na maamuzi ambayo yanaendana na Injili kikamilifu, hata wakati pale ambapo haizungumzwi waziwazi. Aidha, ni kweli katika ulimwengu wa digitali kwamba ujumbe hauwezi kutangazwa bila kuwa na ushuhuda kamili kwa upande wa yule anayetangaza ujumbe huo. Katika hali hizi mpya na aina mpya za kujieleza, mkristo kwa mara nyingine anaitwa kutoa jibu kwa kila anayewauliza habari za tumaini lililo ndani yao (1 Pet 3:15).
Wajibu wa kuishuhudia Injili katika zama za digitali unadai kwa kila mmoja kuwa mwangalifu kwa vipengele vya ule ujumbe ambao unaweza kutoa changamoto kwa baadhi ya njia za fikira ambazo ni za wavuti. Kwanza kabisa, lazima tutambue kwamba ukweli tunaopenda kushirikisha haupati thamani yake kutokana na “umaarufu” au katika kiwango cha kuwa makini kuujali ukweli. Lazima tuufanye ukweli ujulikane katika uadilifu wake, badala ya kutafuta kuufanya ukubalike au kuufifisha. Ni lazima iwe lishe na sio vivutio vya muda mfupi. Ukweli wa Injili sio kitu fulani cha kuliwa au kutumiwa hivihivi; ila ni zawadi ambayo inataka jibu huru. Hata wakati unapotangazwa katika nafasi ya wavuti, Injili inadai kujumuishwa katika ulimwengu halisi na kuunganishwa na sura halisi za kaka na dada zetu, wale ambao tunashirikishana nao maisha yetu ya kila siku. Uhusiano wa kibinadamu ambao ni wa moja kwa moja daima unabaki kuwa wa msingi kwa ajili ya kueneza imani!
Ningependa basi kuwaalika Wakristo, kwamba kwa kujiamini na kwa ubunifu wenye utambuzi na uwajibikaji, kujiunga na mtandao wa mahusiano ambayo yamewezeshwa na zama za digitali. Hii si tu kutosheleza ile hamu ya kuwepo, bali kwa sababu mtandao huu ni sehemu muhimu ya maisha ya binadamu. Wavuti unachangia maendeleo ya upeo mpya na wa utata zaidi kitaaluma na kiroho, ni aina mpya ya utambuzi shirikishi. Katika Nyanja hii pia tunaitwa kuitangaza imani yetu kwamba Yesu ni Mungu, Mwokozi wa wanadamu na historia, ambaye ndani yake vitu vyote vinapata ukamilifu (Efe 1:10). Utangazaji wa Injili unataka mawasiliano ambayo mara moja ni ya heshima na nyeti, ambayo yanaamsha moyo na kusukuma dhamiri; yenye kuakisi mfano wa Kristo mfufuka alipojiunga na wafuasi walipokuwa njiani kueleka Emmaus (Lk 24:13-35). Kwa mkabala wake kwao, mazungumzo yake nao, namna yake ya kuchota kwa upole kile kilichokuwa mioyoni mwao, waliongozwa taratibu mpaka kufahamu fumbo la ufufuko wake.
Hatimaye, ukweli wa Kristo ni jibu kamili na halisi kwa ile hamu ya kuwa na uhusiano, ushirika na maana ambayo inaakisiwa katika umaarufu mkubwa wa mitandao ya kijamii. Waamini wanaotoa ushuhuda kuhusu imani zao za kina zaidi husaidia kwa kiwango kikubwa kuzuia wavuti kuwa chombo cha kuwadhalilisha, kujaribu kuwapotosha kihisia au kinaruhusu wale wenye nguvu zaidi kutawala maoni ya wengine. Kinyume chake, waamini kumtie moyo kila mmoja kuendeleza maswali ya milele ya binadamu ambayo hutoa ushuhuda kwa hamu ya kuwa na upeo upitao akili zetu na kutamani kwetu kuishi maisha halisi, ambayo kwa kweli yanafaa kuyaishi. Ama kwa hakika hii ni shauku ya kiroho ya kibinadamu ambayo kipekee inatia moyo kutafuta kwetu ukweli na ushirika ambao unasukuma ili kuwasiliana kwa ukweli na uadilifu.
Ninawaalika vijana hasa kutumia vizuri uwepo wao katika ulimwengu wa digitali. Ninarudia mwaliko wangu kwao kwenye maadhimisho yajayo ya Siku ya Vijana Duniani jijini Madrid, ambapo teknolojia mpya zinachangia sana katika maandalizi yake. Kwa maombezi ya msimamizi Mtakatifu Fransisko wa Sales, ninamwomba Mungu awajalie wafanyakazi wa mawasiliano uwezo daima wa kufanya kazi yao kwa umakini na utaalamu. Kwa hiari, ninatoa Baraka zangu za Kitume kwa wote.
Kutoka Vatican, 24 Januari 2011, Sikukuu ya Mtakatifu Fransisko wa Sales
BENEDICTUS XVI
No comments
Post a Comment