Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu ametoa njia tatu zinazoweza kutumika kuendeleza mchakato wa Katiba uliokwama.
Amesema hali itakuwa mbaya katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 endapo mchakato huo hautafikia mwisho na kupatikana kwa Katiba mpya.
Profesa Baregu ametoa mwarobaini huo leo Machi 2, wakati akichangia mada katika kongamano la kujadili Katiba na amani wakati wa chaguzi lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Amesema Watanzania walitegemea Katiba mpya kwa kuwa walitembelea nchi hii kwa urefu na mapana yake kukusanya maoni ya wananchi.
"Tunatokaje hapa, mosi twende katika kura ya maoni kuhusu Katiba gani ya mwaka 1977 au tuiache," amesema Profesa Baregu katika kongamano hilo akimwakilisha mwenyekiti wa Kituo cha Demokraisa Tanzania (TCD), James Mbatia.
Pili, amesema, "Tuwe na Bunge Maalum la Katiba jipya. Kuna mapendekezo kuwa liundwe Bunge jipya lisilowahusisha wabunge kwani wabunge walijiundia Katiba yao."
Tatu, Profesa Baregu alielezea jinsi Kenya walivyopata Katiba mpya ambayo inaweza kutumika hapa nchini akisema Kenya waliunda timu ya wataalamu iliyokwenda kwa wanasiasa na wadau wengine ambapo mwisho wakaja na Katiba inayopendekezwa iliyokubaliwa na Wakenya.
"Tulipofika lazima tutoke ili tupate Katiba kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 kwani hali inaweza kuwa mbaya," amesema Profesa Baregu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chadema.
"Mwaka 2015 tulivuka salama ila 2020 tukiingia bila Katiba, sitaki kusema nitaonekana mchochezi ila hiki kiporo kishughulikiwe. Tumeona uchaguzi mdogo wa Kinondoni watu wamepigwa, wameuawa," ameongeza.
Naye Rais mstaafu wa TLS, John Seka amesema haihitajiki kufika katika machafuko ndiko kubadili Katiba.
"Tufanye nini ili yaliyowakuta Kenya hadi kubadili Katiba nasi tusifike huko. Ili kuwe na uchaguzi huru na haki,” amesema.
Seka amesema kunahitajika kuwapo kwa mfumo wa kisheria ambao unawezesha uchaguzi kufanyika na mfumo huo lazima uendane na Katiba na Tume yenye weledi, inayokubalika na mtu yoyote ambaye akiisikia tu anakuwa hana shaka nayo.
Mwakilishi wa Asasi za Kiraia, Deogratius Bwire amesema: "Kwa nini Rais (John) Magufuli asifanye kama alivyofanya mtangulizi wake Jakaya Kikwete aliyekutana na makundi kadhaa kisha kuingia katika majadiliano na mchakato wa Katiba ukaanza, kwanini yeye asifanye hivyo."
Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Yeremiah Maganja amesema tatizo la chaguzi kutokuwa huru na haki inatokana Tume ya Uchaguzi kutokuwa huru na haki.
Mwananchi.
No comments
Post a Comment