Writen by
sadataley
8:22 AM
-
0
Comments
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imechagua majaji wapya kushughulikia mafaili ya kesi zilizoporomoka za Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na naibu wake, Bw William Ruto kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.
Ingawa kesi hizo zilikuwa zimesitishwa baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha, kiongozi wa mashtaka, Bi Fatou Bensouda, aliambiwa yuko huru kuzifufua endapo atafanikiwa kukusanya ushahidi mpya.
Mwishoni mwa mwaka 2017, ilifichuka kuwa wapelelezi wa ICC walikuwa nchini Kenya kuchunguza masuala yanayohusiana na kesi ya Bw Ruto ambaye alishtakiwa pamoja na mtangazaji wa zamani wa redio, Bw Joshua Sang.
Ufichuzi huo ulitolewa kupitia ripoti ya kila mwaka kuhusu shughuli za afisi ya upande wa mashtaka.
Mahakama hiyo Jumamosi imefanya mabadiliko ya majaji baada ya majaji sita wapya kuchaguliwa wiki mbili zilizopita huku wengine waliokuwepo wakipewa majukumu mapya na baadhi yao kukamilisha muda wao wa kuhudumu.
Jaji Chile Eboe-Osuji ambaye wiki iliyopita alichaguliwa kuwa rais wa ICC, sasa atakuwa akihudumu kwenye kitengo cha rufaa cha mahakama hiyo. Awali alikuwa Jaji Msimamizi wa kesi ya Mabwana Ruto na Sang.
Kesi hiyo sasa itaendeshwa na Majaji Robert Fremr, Reine Alapini-Gansou na Kimberly Prost, ambao pia watashughulikia faili la Rais Kenyatta.
Bensouda alidai kuwa uamuzi wake wa kusitisha kesi za Rais Kenyatta, Bw Ruto na Bw Sang ulitokana na kuwa mashahidi walijiondoa. Alidai pia serikali ya Kenya ilikataa kumsaidia kukusanya ushahidi aliohitaji ilhali serikali ina jukumu hilo tuhuma ambazo Mwanasheria Mkuu wa Kenya Prof Githu Muigai alizikanusha vikali.
Parstoday.
No comments
Post a Comment