Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, February 28, 2017

Uamuzi wa pingamizi la Mwenyekiti UVCCM Machi 3


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, Machi 3 itatoa uamuzi mdogo wa pingamizi la kuendelea kwa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa wa Arusha, aliyesimamishwa uongozi, Lengai ole Sabaya.

Kesi hiyo ni ya kujipatia huduma ya chakula na malazi kwa njia ya udanganyifu kwenye Hoteli ya Sky Way jijini Arusha, kisha kujifanya ni ofisa usalama wa taifa. Uamuzi huo utatolewa na Hakimu Gwantwa Mwankunga, Machi 3 mwaka huu kuhusu pingamizi lililowekwa na wakili wa utetezi, Edna Haraka.

Awali shahidi wa kwanza, askari polisi namba F 1093, Sajenti Elia aliiambia mahakama kuwa Agosti 28, mwaka 2016 aliandika maelezo ya mshitakiwa kwa maelekezo ya mkuu wa upelelezi mkoa na kisha kumsomea maelezo hayo mshitakiwa ambaye aliyakubali na wote walisaini.

Shahidi huyo alipewa kuyasoma upya maelezo hayo mbele ya mahakama ambayo yanamuelezea mshitakiwa kujifanya ofisa usalama wa taifa, kujipatia huduma ya chakula na malazi kwa njia ya udanganyifu katika hoteli ya Sky Way ya jijini Arusha, bila ya kulipa.

Mshitakiwa aliyakana maelezo hayo na kudai kuwa alikuwa ni mteja wa mara kwa mara kwenye hoteli hiyo na hajawahi kupatiwa huduma bila kulipia pia hajawahi kufanya kazi ya usalama kama ilivyodaiwa, bali anaipenda kazi hiyo.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Mary Lucas aliiomba mahakama kupewa siku kumi ili awapelekee taarifa mashahidi wawili, ambao ni Philipo John Siaka, ambaye ni Meneja wa Hoteli ya Sky Way ambaye yuko nje ya nchi, na pia mhariri Avelin Myoke, ambaye yuko masomoni, nje ya nchi.

Ombi ambalo limepingwa na wakili wa utetezi akidai kuwa hiyo ni mbinu ya ucheleweshaji wa kesi na miongoni mwa mashahidi hao, Philip John Siaka ndiye mlalamikaji iweje asiwepo mahaklamani hivyo ana mashaka ya kuchelewesha kesi.

Alisisitiza kuwa anachohitaji kwa mujibu wa sheria ni shahidi kuwepo mahakamani ili waweze kumhoji na kumsikia na si vinginevyo.

Hata hivyo, wakili wa serikali aliiambia mahakama kuwa wanaomba siku kumi ili kuwasilisha ushahidi wa maandishi kutoka kwa mashahidi hao ambao wako nje ya nchi kwa shughuli tofauti.

Pia aliiambia mahakama kuwa kifungu cha 91 kinatoa mamlaka kwa Jamhuri wakati wowote inapotakiwa kutoa ushahidi wa mdomo, na ushahidi wa maandishi utatakiwa pale ambapo mazingira yanaonesha kwamba mwandishi wa maelezo amekufa, hajiwezi au ana matatizo ya kiafya na kiakili au yupo nje ya nchi au kama juhudi zote za kumtafuta zimeshindikana kabisa.

Kwa sababu hiyo, alisema upande wa Jamhuri ulishatoa samasi na hatua zinaendelea na mashahidi hawapo nchini. Kifungu 91 (1) a hakizui Jamhuri kupeleka kesi mahakamani na hiyo ni kesi mpya na hivyo Jamhuri haijafanya mbinu au njama za kuchelewesha kesi hiyo hivyo akaomba kesi hiyo ipokelewe na mahakama.

Hoja hizo zilipingwa na wakili wa utetezi akidai kuna njama au mbinu za kuchelewesha kesi na kusisitiza kuwa utetezi unawataka mashahidi wafike mahakamani ikiwemo Siaka ambaye ndie mlalamikaji na hawatakubali ushahidi wa maandishi utakaowasilishwa na Jamhuri.

Kutokana na mvutano huo wa kisheria hakimu Mwankunga, aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 3 mwaka huu ambapo atatoa uamuzi mdogo kuhusu pingamizi hilo la kesi kuendelea au la kutokana na mashahidi hao wawili kutokuwepo mahakamani siku ya kwanza ya kesi hiyo.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment