Writen by
sadataley
5:14 PM
-
0
Comments
Wakati huu ambao Bunge Maalumu la Katiba limeingia katika awamu ya pili ya kujadili na hatimaye kupitisha Rasimu ya Katiba mpya, tulitarajia kwamba wajumbe wake, wakiwamo viongozi wa Bunge hilo wangekuwa tayari wamepata uelewa wa kutosha kuhusu dhana ya Bunge Maalumu la Katiba.
Hii ni pamoja na kusoma na kuelewa vyema Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba na Rasimu ya Katiba Mpya iliyoandaliwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Tulitarajia pia kwamba wajumbe wa Bunge hilo
wangekuwa wamezielewa vyema hadidu za rejea ambazo ndiyo hasa ulikuwa
msingi wa Tume katika kukusanya maoni ya wananchi na hatimaye
kutengeneza Rasimu ya Katiba Mpya. Pamoja na hayo yote, tulitarajia
kwamba uelewa wa mambo hayo ungelisaidia Bunge hilo kufahamu mipaka yake
kama ilivyowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Lakini mkanganyiko
uliopo hivi sasa miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo unaonyesha kwamba
hawajawa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala hayo muhimu, hasa kuhusu
nafasi na mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba kwa mujibu wa Sura ya 83 ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.
Ipo dhana potofu miongoni mwa wajumbe wa Bunge
hilo kwamba chombo hicho ni moja ya mihimili mikuu ya Dola na kinayo
mamlaka kamili kama ilivyo kwa Bunge la Muungano. Ndiyo maana wajumbe
wengi wanataka eti Bunge hilo litunge kanuni zitakazolipatia ‘meno ya
kuuma’ na kuadhibu wananchi wanaolikosoa au vyombo vya habari
vinavyochapisha au kutangaza habari za wananchi wanaolikosoa. Hii ina
maana kwamba wajumbe wengi hawakufaidika na semina elekezi iliyofanyika
mjini Dodoma kabla ya kuanza kwa awamu ya kwanza ya shughuli za Bunge
hilo. Ndiyo maana pia hawajaweza kutambua kwamba Bunge Maalumu halina
dhima ya kuisimamia Serikali na kutunga sheria. Katika majadiliano
yoyote, hakuna jambo la hatari kama wahusika kujadili masuala
wasiyoyaelewa, kama tunavyoshuhudia wajumbe wengi wakifanya bungeni
humo.
Bahati nzuri Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya
mwaka 2011 imeunda vyombo muhimu na kukipa kila chombo hadidu za rejea.
Kila chombo kimewekewa utaratibu wa kazi na mamlaka yake ambayo pia
yamewekewa mipaka. Ndiyo maana Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekusanya
tu maoni ya wananchi na kuandika Rasimu ya Katiba. Kazi ya kuijadili
Rasimu na kupitisha Rasimu ya Katiba ni ya Bunge Maalumu, ambalo pia
limewekewa mipaka ya kutoandika Rasimu mbadala au kubadili mfumo wa
Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume.
Mpangilio huo unaonyesha bayana kwamba madaraka ya
Bunge Maalumu la Katiba siyo mapana kupita kiasi kama wajumbe wake
wengi wanavyodhani, kutokana na ukweli kwamba mchakato wa kupata Katiba
Mpya ulikuwa na ushirikishwaji mkubwa wa wananchi. Kwa maana hiyo, hoja
zilizomo katika Rasimu ya Katiba ni za wananchi wenyewe, siyo za Tume.
Lengo hasa ni kuzuia Bunge Maalumu lisikwapue na
kuteka madaraka ya wananchi, hivyo ushiriki wake katika mchakato huo ni
kuboresha Rasimu ya Katiba na kuipitisha.
Bunge hilo litafanya vyema iwapo litatambua kwamba
jukumu lake kuu ni kujadili na kupitisha matarajio ya wananchi na ndoto
zao ambazo waliziwasilisha katika Bunge hilo kupitia Tume ya Mabadiliko
ya Katiba.
No comments
Post a Comment