Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Monday, March 24, 2014

JK awachanganya wananchi

Dar/Mikoani. Wananchi mbalimbali wa mikoani na Zanzibar wakiwamo wasomi na viongozi wa dini, wamepokea kwa hisia tofauti hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, huku wengi wakipongeza na wengine wakimlaumu kwa kuweka msimamo wake juu ya muundo wa Serikali.
Kilimanjaro
Wakili wa Kujitegemea, David Shilatu, alisema maoni ya Rais, alipaswa kuyatoa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba na siyo ndani ya Bunge Maalumu la Mabadiliko ya Katiba ambalo linapaswa kuheshimu maoni ya wananchi.
“Rais anayeshuhudia Serikali ya Zanzibar ikivunja katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutosema lolote katika hotuba yake, hakika amepoteza uhalali wa kusikilizwa hoja yake ya Serikali mbili,”alisema Shilatu.
Askofu Msaidizi wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo, alisema binafsi angetamani Rais atumie hotuba yake hiyo kueleza nini kifanyike kuondoa kero za muungano ambazo hadi sasa imeshindikana kuzitatua.
“Angeweka historia kama angekuwa na ujasiri wa kuwataka wabunge wathubutu kuzungumzia muungano kikamilifu ambao ni kuwa na Serikali moja,”alisisitiza askofu Shoo.
Wakili mwingine wa kujitegemea, Jaffar Ally alisema Rais kama mkuu wa nchi hakupaswa kusimama upande wowote katika suala la muundo wa Serikali na suala hilo angeliachia Bunge kutumia busara na hekima na kuongozwa na utaifa.
Msomi na Mwandishi wa habari wa zamani wa gazeti la Serikali la Daily News, Michael Tiruhungwa, amesema haikuwa busara kwa Rais kupingana hadharani na maoni ya Tume aliyoiteua mwenyewe.
“Hakuwa na imani na hiyo Tume? Kwa nini aliiteua? Au hakuwa na dhamira ya dhati ya kuwa na katiba mpya, Je, kama tume imekosea mahali ni tume tu ya kulaumiwa hata yeye (Rais) aliyeiteua? Kuna maswali mengi yanahitaji majibu,”alisema.
Mtafiti na mwanasayansi Bingwa, Profesa Watoky Nkya alisema mwanzo Rais Kikwete alianza vizuri hotuba yake na kuhutubia kama Rais, lakini baadaye akapoteza mwelekeo na kuhutubia kama Mwenyekiti wa CCM.
Mkazi mwingine wa Moshi, Joseph Shao alisema amesikitishwa na hotuba ya Rais Kikwete na kusema angalau hotuba ya mwanasheria mkuu wa zamani wa Kenya, Amos Wako ilikuwa na maana zaidi kwa Watanzania kuliko hotuba ya Rais Kikwete.
Wananchi wengine waliopiga simu na kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (sms), walitaka Bunge hilo livunjwe kwa vile hotuba ya Rais imeondoa uhalali wa wao kuendelea ‘kutafuna’ fedha za walipa kodi.
“Amenisikitisha sana, kama alijua Serikali mbili ndiyo jibu la kero za muungano aliunda Tume ya nini? Si Serikali ingepeleka tu muswada wa matekebisho ya katiba?”, alihoji padri mmoja wa Kanisa Katoliki.
Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Karanga wa KKKT wa mjini Moshi, Fred Njama alisema Rais Kikwete hakuwatendea haki Watanzania na alitoka nje ya msitari pale aliposema hataruhusu Serikali tatu katika utawala wake na kwamba kauli hizo za kibabe hazikupaswa kutolewa na Rais.
“ Kwa msimamo wake huo ni kama kuwaambia wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwamba wafanye wanavyofanya lakini muundo unaotakiwa ni Serikali mbili... Nafikiri kwa wajumbe makini wanapaswa kutangaza kujiuzulu,” alisema.
Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael alisema hotuba hiyo ya Rais inaweza kuliingiza taifa kwenye mgogoro mkubwa na ni hotuba isiyobeba hadhi ya kuongozi wa nchi.
“Taifa limeingizwa kwenye gharama kubwa kwa jambo ambalo wakubwa hawalitaki... Suluhu ya kero za Muungano ni kuwa na Serikali moja ama Serikali tatu zilizopendekezwa na Tume... Tuache unafiki,” alisema.
Kagera
Kada wa CCM na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho mkoani Kagera, Pius Ngeze, amesema pamoja na kutokubaliana na muundo wa Serikali tatu maoni ya Tume ya Jaji Warioba siyo ya kupuuzwa kwa kuwa yamefanyiwa utafiti.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili, Ngeze aliunga mkono hotuba ya Rais Kikwete kuhusu umuhimu wa kuboresha muundo wa Serikali uliopo na kutaka malalamiko ya pande zote za Muungano yatafutiwe ufumbuzi.
Hata hivyo, alishangaa wananchi wa Tanzania Bara kuwekewa vikwazo vya kumiliki ardhi Zanzibar na kusema suala hilo linazungumzika na kutaka uwekwe utaratibu wa wananchi kuomba kumiliki ardhi kwa mujibu wa sheria zitakazokuwepo.
Kuhusu uwezekano wa kuwepo mvutano wa kutaka kupokezana, utaratibu wa kupokezana vipindi vya kugombea urais kati ya pande mbili za Muungano, Ngeze alisema hiyo itakuwa ni kuminya demokrasia kwa kuwa kila mwananchi bila kujali upande anaotoka anaruhusiwa kugombea.
Akitoa maoni yake baada ya hotuba ya Rais Kikwete wakati za kuzindua Bunge Maalumu la Katiba, Waziri Mstaafu wa Mambo ya Nje na mbunge wa zamani wa Jimbo la Nkenge, Joseph Rwegasira alisema anaunga mkono hotuba hiyo kwa asilimia mia.
Alisema ni muhimu kuweka ukomo wa kugombea kwa viongozi wa ngazi za kitaifa na kuwa suala la ukomo wa nafasi za ubunge waachwe liamuliwe na wananchi na kusema Muungano ulikuwa na nia njema.
Pia Waziri huyo wa zamani alitetea utaratibu wa wananchi wa Bara kuzuiwa kumiliki ardhi Zanzibar, akisema hata sehemu ya ardhi waliyo nayo haiwatoshi na kuwa lazima tukubali kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo kwa kuwa Bara iliamua kuungana na nchi ndogo.
Pia katika maoni yake mmoja wa wafanyabiashara wa ndizi katika Soko la Kashai mjini Bukoba, Faustin Stanslaus, alisema kwake Katiba Mpya itakuwa na umuhimu kama itamletea unafuu wa maisha na uhakika wa soko la bishaa zake.
Mbeya
Wakazi wa Mkoa wa Mbeya wameipokea Hotuba ya Rais, Jakaya Kikwete kwa kuisifu na kuikosoa katika vipengele kadhaa.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiashara Soko la Kyela, Thabiti Somozi alisema pamoja na uzuri wa hotuba kwa yale aliyozungumzia, lakini hakugusia mambo yanayohusu wafanyabiashara jambo ambalo limemweka njia panda.
“Nilisikiliza tangu mwanzo hadi mwisho hotuba ya Rais Kikwete , alifafanua mambo kwa umakini sana, lakini hakugusia kabisa masuala ya wafanyabiashara,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku), Stephen Chambanenge, pamoja na kusifia kwa jinsi Rais alivyofafanua madhara ya Serikali tatu, alikosoa hotuba yake kuhusu suala la ukomo wa wabunge.
Chambanege alisema hofu ya Rais kuhusu ukomo wa wabunge unalenga kuendeleza uongozi wa kibeberu, ambao unazingatia zaidi wenye fedha watakaoweza kudumu kwenye wadhifa kwa kuununua.
Alisema mapendekezo ya Rasimu ya Katiba Mpya kuhusu ukomo wa wabunge hauna budi kuzingatiwa.
Anna Kyoma wa Mwanjelwa alisema hotuba ya Rais ilimfungua macho, alipozungumzia nafasi ya Jeshi katika suala zima la Muungano .
Kyoma alisema ipo haja ya kuangalia ukweli kuhusu uendeshaji wa Jeshi kwenye masuala ya Serikali tatu na kwamba kama katiba ‘ikibugi’, nchi itashikiliwa na Jeshi.
Mkazi wa Ilomba jijini hapa , Lucas Mwampiki akitoa maoni yake kuhusu hotuba hiyo alisema Rais aliamua kuwashinikiza Watanzania wafuate maoni ya CCM.
Mwampiki ambaye ni diwani jijini Mbeya kupitia Chadema alisema kauli yake ya kwamba; “ wanaotaka Serikali tatu wasubiri yeye aondoke,’’ ilionyesha wazi kwamba anawashinikiza Watanzania aunge mkono ya CCM.
Songea
Nathaniel Haule Mkazi wa Manispaa ya Songea ameipongeza hotuba hiyo kuwa ni nzuri, Rais hakuwa na chuki amewaelimisha wananchi kwa utulivu bila jazba, tofauti na watu walivyotarajia wala hakuponda wapinzani na wajumbe wa katiba ambao wameonekana kuwa ni vinara wa vijembe .
Alisema madhara ambayo amezungumzia ya kuwa na Serikali tatu yafanyiwe kazi kwa vitendo, kwani wengi waliokuwa waking’ang’ania kuwa na Serikali tatu wamejua madhara na gharama ambazo nchi itazipata.
Mpenda Mvulla mkazi wa Mfaranyaki Songea aliipongeza hotuba ilikuwa ni nzuri amempongeza Rais, amewaelekeza madhara ya Serikali tatu haina haja kwani kuna madhara makubwa na gharama.
Aliwaomba wabunge watafakari kwa kina hotuba hiyo na kuchukua mazuri aliyowaelekeza. Hotuba ilikuwa ya kusisimua na yenye mpangilio mzuri na imeelimisha na kufundisha kwa sisi wananchi ambao tulikuwa hatuna uelewa na kwa wajumbe ambao wameingia bungeni ambao hawaijui rasmu hiyo.
Alisema amevutiwa zaidi na Rais Kikwete kukubali kuzitatua kero za muungano ambazo zilikuwa sita na tatu zitaingizwa kwenye katiba.
Kwa upande wake Andrew Chatwanga, naye ameipongeza hotuba hiyo ambapo amewataka kero za muungano zijadiliwe pande zote mbili kwani hata Tanzania Bara nao wana kero zinazowasumbua katika muungano badala ya kero hizo kuachiwa Zanzibar pekee.
Zanzibar
Mwanasheria Mkuu wa zamani wa SMZ, Hamid Mbwezeleni, alisema pendekezo la muundo wa Serikali tatu katika rasimu ya Jaji Joseph Warioba halikuwa muarubaini wa kuondoa kero katika Muungano na badala yake ungezusha mivutano na kuwa kifo cha mende pia kufa mapema kwa Serikali ya tatu.
Mbwezeleni alisema hakuna kizuri chochote kisicho na kasoro na kushauri ufumbuzi wa msingi ni kuondoa matatizo yaliyopo ili kuuelezea mfumo wa Muungano wa Serikali mbili ambao una manufaa zaidi kwa pande mbili za Muungano , Tanganyika na Zanzibar.
“Tusiletewe tiba ya muarubaini pekee na kututia ukakasi, dunia ingetushangaa kubadilisha muundo wa Taifa kwa maoni ya watu 350,000 kati ya milioni 44. Mambo ya msingi na tunu za Taifa, hazikupaswa kuguswa. Alichokifanya Rais Kikwete ni kutazama kwake mbele zaidi,” alisema Mbwezeleni.
Alisema Wazanzibari na Watanzania Bara, baada ya miaka 50 kupita wana miingiliano mikubwa ya damu, ujamaa na udugu hivyo kuwepo kwa nchi mbili ndani ya Taifa moja ni dhahiri kutaibuka ushindani na watakoumia ni wananchi wanyonge si wanansiasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani alisema hotuba ya Rais Kikwete ni mbovu na imepoteza lengo zima la wananchi waliotarajia kupatikana kwa Katiba Mpya iliyo bora mwaka 2015.
Bimani alisema CUF itaendelea kudai Muungano wa Mkataba na kusisitiza hoja mbalimbali zilizotolewa zikipinga mfumo wa Muungano wa Serikali tatu , zimelenga kuimeza Zanzibar na Rais Kikwete hakupaswa kuwatisha wananchi na wanasiasa kama jeshi linaweza kuchukua nchi ikiwa Serikali ya Muungano itatetereka.
Alisema kinachoendelea hivi sasa huko Dodoma ni kasi ya ufujaji wa fedha za wananchi, kwa vile Rais amekwishatoa mwelekeo wa aina ya Katiba inayotakiwa na watawala bila ya kuheshimu matakwa ya wananchi wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Mustakabali wa Muungano utaendelea kubaki katika dimbwi la mashaka na mivutano, katiba ikishindwa kuipatia mamlaka huru Zanzibar na Tanganyika, hakutakuwa na jibu au suluhisho la kupungua kero za Muungano,” alisema Bimani .
Msemaji wa CCM Ofisi Kuu ya Kisiwandui Zanzibar Salim Reja alisema hotuba ya Rais Kikwete imejaa manufaa kwa wananchi na Taifa. Haikuwa mwafaka kwa Jaji Warioba kueleza rasimu yake haistahili kupunguzwa wala kuongezwa kitu na Bunge la Katiba na badala yake ihaririwe.
Reja alisema kusingekuwa na sababu yeyote ya kuundwa Bunge Maalumu la Katiba na kuwataka wabunge kutekeleza kwa vitendo kuongeza au kufuta vifungu visivyo na maslahi kwa wananchi na Taifa.
Naibu Katibu Mkuu wa DP Zanzibar, Ali Azzan Kiongwe, alisema hotuba ya Rais Kikwete imesaidia kuwaelimisha wananchi juu ya utaratibu uliotumika ya kuongeza mambo katika orodha ya Muungano na kuondoa upotoshaji uliokuwa ukifanywa na wanasiasa kwa maslahi yao binafsi.
Kiongwe alisema kutoka sasa hakuna Mzanzibari atakayekubali kuwa kuna mambo ya Muungano yaliingizwa kinyemelea, kutoka 11 hadi kufikia 22 na kusema yote yalifuata utaratibu kwa mujibu wa sheria na hakukuwa na hadaa wala ghiliba.
Maryam Hamad Seif mkaazi Shangani, alisema wananchi wa Zanzibar hawajashangazwa na kauli ya Rais Kikwete kwa vile wanatambua kuwa Serikali za CCM hazijawa tayari kwa mabadiliko ya kidemokrasia, hasa kupitia uchaguzi mkuu na hivyo maelezo ya Rais Kikwete yanapiga uhuru uliopo.
Alisema kwamba yeye na Wazanzibari wengine wanaaamini kuwa Muungano bora ni ule wa mkataba, huku kila upande ukiendesha mambo yake yenyewe bila ya Tanganyika kujificha kwenye koti la Muungano na kuimeza Zanzibar isifurukute.
Raya Majid Ame anayeishi Sogea, alisema hotuba ya Rais Kikwete imelielekeza Bunge la Katiba lifanye inavyotaka CCM, na sasa hategemei lolote litokee kwa maslahi ya pamoja na kupunguza kero zilizopo kwa njia za usawa na mapatano.
“Wazanzibari watafika mwisho wa kuwa watumishi wa koloni la Tanganyika, lini tutapata mamlaka yetu na kuishi kama Taifa huru linalojitegemea na kujiamualia mambo yake bila ya kuzuiwa na kiwingu cha Serikali ya Muungano”, alisema.
Dodoma
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Mustapha Okonaay wameshauri kuvunjwa kwa bunge hilo na kurejea kwa wananchi ili wapige kura ya maoni juu ya Muundo wa Muungano wanaoutaka ili kuondoa malumbano ambayo yameibuka sasa.
Akizungumza na mwananchi jana alisema kwa mazingira ya sasa katika bunge hilo na mkanganyiko uliotokana na hutuba ya Rais Jakaya Kikwete dhidi ya hotuba ya Jaji Warioba, muafaka ni kurejea katika kura ya maoni.
“Mimi nadhani ni muhimu kurudi kwa wananchi na hapo ndipo utabainika ukweli juu ya hoja ya Muundo wa muungano, kwani ndiyo msingi wa Katiba mpya,” alisema Akonaay.
Akonaay ambaye pia ni Mwanasheria alisema, Jaji Warioba alifanyakazi kubwa sana tena ya kitaalamu kukusanya maoni ya wananchi na kukusanya taarifa za tume mbali mbali na kuwasilisha bungeni, lakini sasa inaonekana mjadala umekuwa wa kisiasa na kuonekana kama takwimu za wanaotaka muungano ni wachache.
“Hapa tunatunga Katiba ya wananchi ili kuepuka kutumia mabilion ya fedha za Umma kwa jambo ambalo mbeleni litapingwa ni busara kurudi kwa wananchi “alisema Akonaay.
Daniel Mjema, Moshi, Phinias Bashaya, Bukoba, Lauden Mwambona, Mbeya, Joyce Joliga, Songea, Juma Mtanda, Morogoro, Mwinyi Sadallah, Zanzibar, Mussa Juma, Dodoma
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment