Latest News

GNM Cargo

GNM Cargo
GNM CARGO & LOGISTICS

menu

Monday, June 12, 2017

Sakata la Lugumi bado bichi

KAMA ulifikiri sakata la mkataba tata kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd limeisha, ulikuwa unakosea.

Mwenyekiti wa Kamati Ndogo iliyoundwa kulichunguza na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Japhet Hasunga, amesema sakata hilo halijaisha kwa kuwa uchunguzi wao ulibaini kuwapo kwa dosari lukuki na "kufunika kombe ni kuhalalisha ubadhirifu wa mabilioni ya shilingi".

Aprili 23, mwaka jana, PAC ililazimika kuunda kamati hiyo ndogo kuchunguza utekelezaji wa mkataba huo wenye thamani ya Sh. bilioni 37 na kuwasilisha ripoti ya uchunguzi wake bungeni.

Kamati ndogo hiyo yenye wajumbe tisa kutoka PAC, chini ya uenyekiti wa Hasunga, ilikuwa na wajumbe watano kutoka Chama Cha pianduzi (CCM) huku Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) vikitoa wajumbe wawili kila kimoja.

Akitangaza maazimio ya kuunda kamati hiyo kwenye jengo la Ofisi za Utawala wa Bunge siku hiyo, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly, aliipa wiki nne kuanzia Aprili 24, 2016 kupitia hatua kwa hatua utekelezaji wa mradi huo.

Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd ilikuwa inatekeleza mradi wa kufunga vifaa vya utambuzi wa alama za vidole (AFIS) kwenye vituo vya polisi nchini.

Aeshi alisema kamati hiyo ilitakiwa kuchunguza kile ambacho hakikutolewa maelezo ya kina na maofisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi walipoitwa na kuhojiwa na PAC kwenye moja ya kumbi za Bunge mjini hapa Aprili mwaka jana.

Mbali na Hasunga ambaye pia ni Mbunge wa Vwawa mkoani Songwe (CCM), wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Mbunge wa Malindi, Dk. Hadji Hussein Mponda (CCM), aliyekuwa Mbunge wa Dimani (CCM), Hafidh Ali Tahir (sasa marehemu), Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) na Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk (CUF).

Wengine ni Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM), Mbunge wa Viti Maalum, Tunza Malapo (Chadema), Mbunge wa Viti Maalum, Khadija Ally Al-Qassmy (CUF) na Mbunge wa Same Mashariki, Naghenjwa Kaboyoka (Chadema) ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa PAC.

Kaboyoka alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa PAC baada ya kamati hiyo kukaa takribani mwaka mzima bila kuwa na mwenyekiti kutokana na mvutano uliokuwa unaendelea kati ya uongozi wa Bunge na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu mbunge wa upinzani wa kuiongoza.

Katika mahojiano maalum na Nipashe mjini hapa Jumanne, Hasunga alisema kamati yake ilibaini vituo vya polisi 15 (asilimia 13.9) vilikuwa vimefungiwa vifaa hivyo na kufanya kazi kikamilifu kati ya 108 vilivyotakiwa kwa mujibu wa mkataba.

Alisema haikuwa rahisi kukamilisha ripoti ya uchunguzi huo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya baadhi ya wajumbe wa kamati yake kutuhumiwa kupokea 'kitu kidogo' ili wahakikishe baadhi ya mambo hayaandikwi kwenye ripoti ya uchunguzi.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya Nipashe na Hasunga kuhusu sakata hilo:

SWALI: Ulifanya kazi kubwa na kwa maoni ya wananchi, wewe na Aeshi ni mashujaa kwa kuwa ni wabunge wa chama tawala, lakini mkaamua kufuatilia kwa kina mkataba huo wenye utata.

Unafikiri usimamizi wa uchunguzi wa sakata hilo ungekuwa na matokeo tofauti kama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ingebanwa na Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya PAC au PAC yenyewe kutoka upinzani?

HASUNGA: Hapana! Nafikiri matokeo yangebaki kuwa hayahaya. Kamati hii pamoja na kwamba niliiongoza mimi, bado kulikuwa na wajumbe wa upinzani. Na mwenyekiti si anayeandika ripoti.

Kamati ndogo (ya PAC) baada ya kuundwa, naomba lieleweke hili, ilipewa hadidu moja tu ya rejea ambayo ni kuangalia kama vifaa vilinunuliwa na kufungwa katika vituo vyote vilivyotakiwa kufungwa na vinafanya kazi.

Na hoja hii ilitokana na maagizo ya nyuma ya Kamati ya PAC kwamba Ofisa Masuhuli (wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi) ahakikishe vifaa vinafungwa ndani ya miezi sita lakini CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) akabaini ni vituo 14 tu kati ya 108 ndivyo vifaa hivyo vilikuwa vimefungwa na vinafanya kazi.

Kwa hiyo, sisi tuliagizwa kuangalia kwanini vituo 14 tu, hivyo tulikwenda kuangalia alichokisema CAG.

Wakati wa ukaguzi, kamati yangu iligawanyika katika makundi matatu. Matokeo kwenye ripoti yetu yanaoana pia na ripoti ya CAG. Ni vituo 15 tu ndivyo tulivituka vifaa vilikuwa vinafanya kazi sawasawa.

Mradi huo unataka mambo matatu; kwanza vifaa vichukue picha, pili vihifadhi taarifa na tatu vitume taarifa kwenye vituo vingine kwa maana ya 'sharing of information' (kubadilishana taarifa).

CAG alisema vituo 14, sisi tumekuta vituo 15. Kwa hiyo, hata angeongoza mpinzani, bado ingekuwa taarifa ileile. Bahati mbaya sana ripoti yetu yote haikusomwa bungeni badala yake yalisomwa maagizo tu.

Kitu kikubwa kwenye ripoti ni kwamba serikali kutokuwa na dhamira ya makusudi ya kuvitumia vile vifaa kwa sababu kwenye maeneo mengi vimenunuliwa na vimefungwa lakini havitumiki.

Tulipouliza tulijibiwa hakuna mtandao. Lakini kumbuka vinapaswa kufanya kazi tatu. Kama hakuna mtandao, mbona kazi mbili za kupiga picha na kuhifadhi taarifa nazo hazifanyiki?

Kutokana na kutotumika, tulibaini vifaa vingi vilikuwa vimeanza kuharibika. Kumbuka vile ni vifaa vya elektroniki, visipotumika, vinaharibika.

SWALI: Kwa muda uliokuwa Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya PAC, ulikumbana na changamoto zipi wewe binafsi na kamati kwa ujumla ambazo pengine huwezi kuzisahau?

HASUNGA: Kwanza, suala lenyewe lilikuwa nyeti. Vifaa vyenyewe vilikuwa vinahusu mambo ya usalama. Mbaya zaidi, kulitakiwa kutoa taarifa za kiusalama kwa umma. Changamoto hapa ilikuwa tutoe taarifa kwa kiasi gani kuhusu masuala hayo ya kiusalama.

Pili, ndani ya kamati kulikuwa na makundi matatu kama nilivyoeleza awali. Changamoto ilikuwa namna gani ripoti ya jumla ifanane na taarifa za makundi yote matatu. Kuziunganisha zile taarifa za makundi yote ilikuwa kazi kubwa.

Tatu, muda tuliopewa ulikuwa mdogo, (mwezi mmoja) ulikuwa mdogo sana kuzunguka nchi nzima kwenye vituo vyote na kuandaa ripoti. Wakati mwingine tulilazimika kufanya kazi hadi usiku kukamilisha kazi kwa wakati. Wiki mbili tulizitumia 'field' na wiki mbili zingine tukazitumia kuandaa ripoti.

Nne, kulikuwa na tuhuma na changamoto ya baadhi yetu kuhongwa na kuathiri kazi yetu. Nilikuwa makini sana, hadi mwisho nilifurahi tulikwenda vizuri na tulipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa serikali na Jeshi la Polisi.

Ilikuwa ni ngumu kujua ni nani kati yetu ametafutwa (ili kuhongwa), nilichokifanya nilikuwa naangalia mtu (mjumbe wa kamati) anachangia nini kujua 'objectivity' yake.

SWALI: Je, sakata la Lugumi limekwisha?
HASUNGA: Hapana! Suala hili bado halijaisha. Baada ya kuleta taarifa bungeni, Bunge lilitoa miezi mitatu kwa serikali kutekeleza mradi huo kwa kuhakikisha vifaa vinafungwa na vinafanya kazi huku PAC ikitakiwa kufuatilia maagizo hayo.

Maagizo yetu (Kamati Ndogo ya PAC) ni kuhakikisha kazi inakamilika. Kilichobaki ni Kamati ya PAC kufuatilia kama serikali imetekeleza maagizo ya Bunge.

Bila kutekeleza mradi huu, matumizi ya mabilioni ya shilingi yaliyotumika yatakuwa ni hewa. Suala hili bado halijaisha hadi pale serikali itakaposema imetekeleza kwa asilimia 100 na PAC ikajiridhisha.

SWALI: Je, unafikiri kuchaguliwa kwa Mama Kaboyoka kuongoza PAC ni mwanzo mpya wa safari yenu kutoka mlipoishia mkiwa chini ya Aeshi?

HASUNGA: Ndiyo! Nafikiri ni mwanzo mpya. Kamati hizi mbili kwa maana ya PAC na LAAC (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa) zinatakiwa kuongozwa na mwenyekiti anayetoka upinzani.

Kutokana na kuchaguliwa kwa Mama Kuboyoka, sasa tumekidhi mahitaji na matakwa ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016.

Nipashe inafahamu kwamba utata wa utekelezaji wa mkataba huo uliibuliwa na PAC Aprili 5, mwaka jana wakati kamati hiyo ilipokuwa inapitia Fungu 28 la utekelezaji wa bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Baada ya kubaini utata huo, kamati hiyo iliagiza ipewe taarifa ya utekelezaji wa mradi wa mkataba huo pamoja na mkataba wenyewe.

Kwa mujibu wa Aeshi, taarifa ya utekelezaji wa mradi huo iliwasilishwa kwenye Ofisi ya Spika wa Bunge Aprili 18, mwaka jana.

PAC ilipokea taarifa hiyo na wajumbe wake kuipitia kwa siku mbili na kubaini utata zaidi katika ufafanuzi uliotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, jambo ambalo liliilazimu kamati kuwaita na kuwahoji maofisa wa wizara hiyo na Jeshi la Polisi walioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projest Rwegasira.

Kutokana na kutoridhishwa kwake na ufafanuzi uliotolewa na maofisa hao, kamati hiyo ikaamua kuunda kamati ndogo ya uchunguzi kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni ya 117(18) cha Kanuni za Bunge toleo la Januari 2016.

Kifungu hicho kinasema: "Kamati yoyote inaweza kuunda Kamati Ndogo kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli zake, kadri itakavyoona inafaa na kila Kamati Ndogo itapangiwa kazi zake na Kamati ya Kudumu inayohusika."
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment