Latest News

GNM Cargo

GNM Cargo
GNM CARGO & LOGISTICS

menu

Tuesday, June 6, 2017

Mtazamo wa Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano na bara la Afrika

Akizungumza hivi karibuni katika kikao cha 51 cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS huko Monrovia mji mkuu wa Liberia, Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, amesema kuwa ushirikiano wa umoja huo na bara la Afrika una umuhimu mkubwa kwa ajili ya kudhamini amani na usalama barani humo.
Huku akiashiria kuongezeka kwa tishio la ugaidi duniani, Mogherini ametaka kuchukuliwa hatua za pamoja kwa ajili ya kupambana na ugaidi na kuzuia kuongezeka fikra za kuchupa mipaka katika pembe tofauti za dunia. Kwa hakika kushiriki Federica Mogherini, ambaye ni kiongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya katika kikao cha ECOWAS kilichoanza mjini Monrovia hapo siku ya Jumamosi, kunathibitisha wazi umuhimu unaopewa bara la Afrika na umoja huo katika sera zake za nje. Mbali na masuala ya kibiashara na kiuchumi, moja ya matatizo muhimu yanayoukabili Umoja wa Ulaya ni kuhusu suala la uhamiaji haramu wa maelfu ya Waafrika wanaoelekea barani humo kupitia Bahari ya Mediterania kwa madai ya kutafuta maisha bora.
Baada ya kufanikiwa kwa kiwango fulani mkataba uliotiwa saini kati yake na Uturuki mwezi Machi mwaka uliopita wa 2016 kwa ajili ya kuwazuia wahamiaji haramu wa Kiafrika kuingia barani Ulaya, umoja huo sasa una matumaini ya kutia saini mikataba kama hiyo na baadhi ya nchi za Kiafrika ili kuzuia wimbi la wahamiaji hao haramu wanaoelekea nchi za Ulaya. Tayari mkataba kama huo umeshatiwa saini kati ya umoja huo na Libya. Pamoja na hayo hiyo ni hatua ndogo sana ya kujaribu kupambana na tatizo hilo na hilo linatokana na ukweli kuwa ni kina cha tatizo hilo ndicho kinapaswa kutatuliwa na sio dalili zake za dhahiri tu. Ni kwa kutilia maanani suala hilo ndipo Mogherini katika matamshi yanayofanana na yale yaliyotolewa hivi karibuni na Musa Faki, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, akasisitiza kwamba njia pekee ya kupambana na tatizo la uhamiaji haramu, ni kusaidia maendeleo na ustawi wa bara la Afrika pamoja na kujenga misingi madhubuti ya uchumi kwa ajili ya vijana wa bara hilo.
Kwa msingi huo Umoja wa Ulaya umepanga kutekeleza mradi unaoitwa ''Mpango wa Uwekezaji wa Nje wa Ulaya" barani Afrika ambao kwa mtazamo wa Mogherini unaweza kuchukuliwa kuwa ni mapinduzi ya siku zijazo za uwekezaji wa Ulaya barani Afrika. Kwa kuzingatia hilo, kikao kijacho cha Ulaya na Afrika ambacho kimepangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu kitajadili zaidi suala la kubuni nafasi za kiuchumi kwa ajili ya vijana wa Kiafrika.
Pamoja na hayo lakini uzoefu wa ukoloni wa Ulaya na hasa wa Ufaransa na Uingereza barani Afrika unaonyesha kwamba nchi za Ulaya bado zinafuatilia maslahi yao ya kiuchumi na kibiashara barani humo kupitia uingiliaji wa kijeshi katika nchi kama Mali na Ivory Coast. Dhana hiyo inatiliwa nguvu hasa tukizingatia kuwa hadi sasa Umoja wa Ulaya haujachukua hatua yoyote ya maana kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kiuchumi katika nchi za Kiafrika.
Pamoja na hayo,  kuenea ugaidi katika nchi nyingi za Kiafrika zikiwemo za Somalia, Nigeria na Mali na uwezekano wa kuvuka mpaka ugaidi huo hadi nchi za Ulaya zimezifanya nchi hizo za Magharibi kufuatilia kwa karibu suala la kutaka kuchukuliwa hatua madhubuti za kukabiliana na suala hilo, bali hata baadhi ya nchi za Ulaya kama Ujerumani sasa zimeimarisha uwepo wao katika nchi kama vile Mali kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa kupambana na makundi ya kigaidi. Suala la ugaidi limekuwa tatizo sugu katika nchi za magharibi mwa Afrika. Jambo jingine ambalo linazisumbua nchi hizo ni suala zima la hatima isiyojulikana ya mkataba wa hali ya hewa wa Paris ambao Marekani imetangaza kujiondoa. Mabadiliko ya hali ya hewa yana athari za moja kwa moja kwa nchi za Kiafrika ambazo husababisha ukame, vimbunga, mafuriko na kupungua misitu. Ni kwa kutilia maanani matatizo hayo ndipo Mogherini akasisitiza katika kikao cha Monrovia mfungamano wa Umoja wa Ulaya juu ya utekelezwaji wa mkataba huo wa Paris kwa madhumuni ya kuzuia kuongezeka kwa viwango vya joto duniani.
Parstoday
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment