Writen by
sadataley
11:56 AM
-
0
Comments
ASUBUHI ya jana ilikuwa siku mbaya kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi kwani taarifa zinaonyesha alisimamishwa kazi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa muda mfupi baada ya saa 6:00 usiku wa juzi.
Aidha, Ngalamgosi anakuwa ofisa wa umma ambaye anashikilia rekodi ya ajira yake kusimamishwa usiku zaidi.
Machi 3, mwaka jana Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama alitengua uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Carina Wangwe uliotangazwa mapema siku hiyo, saa 4:00 usiku.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa usiku huo, imeeleza kuwa uteuzi huo umetenguliwa kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya taratibu.
Ni nini sababu ya Ngalamgosi kusimamishwa mapema jana na Waziri Mkuu Majaliwa? Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliyosainiwa na Gerson Msigwa ya usiku huo haikutaja sababu.
Lakini wachambuzi wa masuala ya uchumi na siasa waliozungumza na Nipashe jana wanaona ni tangazo lililotolewa na Ewura wiki iliyopita, likiwataka wananchi kutoa maoni yao juu ya ombi la kampuni ya kufua umeme ya IPTL kutaka kuongezewa muda wa leseni yake ya kuzalisha nishati hiyo kwa miezi 55 kutokea Julai 15.
Tangazo la Ewura la Jumatano lilimtaka kila Mtanzania mwenye maoni au taarifa za kupinga ama kuunga mkono ombi la IPTL kuwasilisha kwake kwa maandishi.
Ngamlagosi aliteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kushika nafasi hiyo Februari 17, 2014 akichukua nafasi ya Haruma Masebu aliyekuwa amemaliza muda wake.
Nipashe lilimtafuta Ngamlagosi jana ili kufahamu sababu iliyosababisha kusimamishwa kwake, lakini alijibu kwa kifupi "Sina cha kuzungumza."
Alipoulizwa amepokeaje taarifa ya kusimamishwa kazi, pia alijibu kwa kifupi "Sina cha kuzugumza."
Akizungumza na Nipashe jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Bashiru Ally alisema utenguzi wowote unapofanywa na Rais ama Waziri Mkuu ni lazima kutakuwa na makosa yaliyofanywa na mhusika huyo.
Alisema kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura huenda kumesababishwa na wasaidizi wake, ama utendaji wake, lakini anayefahamu sababu haswa ni Waziri Mkuu, Rais John Magufuli na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.
"Inaweza ikawa ni kasoro ya muda mrefu, pia inaweza ikawa ni IPTL kwa sababu nchi iliingia katika mtikisiko mkubwa uliosababishwa na kampuni hiyo," alisema Dk. Ally. "Sasa leo hii tena kampuni hiyo inaleta maombi na wewe unapokea! Lazima kingetokea kitu."
Kiongozi Mkuu wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kulikuwa na kila sababu kwa Mkurugenzi wa Ewura kuwajibishwa kwa sababu yeye ndiye aliyetoa tangazo la IPTL la maombi ya leseni.
Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila alisema tangazo la Ewura kutaka umma uwasilishe maoni ingekuwa mwisho wa IPTL kuvuna pesa kwani umma ulishaifuta IPTL miaka mingi, lakini imebaki imeshikiliwa na baadhi ya wenye mamlaka.
Naye mhadhiri kutoka UDSM, Dk. Benson Banna alisema viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza mashirika ya umma wanapaswa kuwa makini na waangalifu.
Alisema sababu kubwa iliyosababishwa kuondolewa kwa Mkurugenzi wa Ewura ni suala la IPTL, na kwamba kosa alilolifanya mkurugenzi huyo ni kutokuwasiliana na wakubwa wake ili kupewa ushauri zaidi.
"Suala la IPTL siyo geni hapa nchini, liliwahi kuleta songombingo, hata Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwahi kusema akili za kuambiwa changanya na za kwako, sasa Mkurugenzi wa Ewura alipaswa kufikiria mara mbili mbili kuhusu suala hili la IPTL," alisema Dk. Banna.
Dk. Banna alisema hata kama sheria ya Ewura inaruhusu kupokea maombi na kuwashirikisha wadau, Mkurugenzi alipaswa kutolikimbilia haraka haraka kama alivyofanya.
"Siyo kila sheria iko sawa, sheria hizi zilitungwa na binadamu kama sisi ambao walikuwa na maslahi nazo au ziliendana na wakati ule," alisema Dk. Bana.
"Sasa ukiwa kiongozi wa shirika la umma unapaswa kuwaza zaidi kuliko kuangalia sheria hususani sekta nyeti."
Alisema Mkurugenzi wa Ewura alipaswa kuomba ushauri kwa Mwanasheria Mkuu, au viongozi wengine walioko juu yake.
Tangazo lililotolewa na Ewura muda mfupi baada ya kutumbuliwa kwa Ngamlagosi jana linaonekana kuunga mkono hoja ya Dk. Bana baada ya kutangaza kusitishwa kwa mchakato huo wa IPTL kwa maagizo ya Wizara ya Nishati na Madini.
Tangazo hilo lilisema:
"Taarifa inatolewa kwa umma kwamba kufuatia maombi ya kampuni ya uzalishaji umeme ya INDEPENDENT POWER TANZANIA LIMITED (IPTL) (“Mwombaji”) kuomba kuongezewa muda wa leseni yake ya kuzalisha umeme kwa kipindi cha miezi 55 kutokea tarehe 15 Julai 2017, EWURA, zaidi ya hatua nyingine za kiudhibiti, iliwasiliana na Wizara ya Nishati na Madini ili kupata maoni yake kwa mujibu wa kifungu cha 7 (3) cha Sheria ya EWURA, Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania.
Wizara ya Nishati na Madini imetoa mapendekezo ya kuwapo na mashauriano zaidi kati ya Wizara, EWURA na wadau mbalimbali wa sekta ndogo ya umeme kabla ya kuendelea na mchakato wa maombi ya Mwombaji.
"Kutokana na maoni hayo, EWURA inasitisha mchakato wa kushughulikia maombi ya leseni ya Mwombaji ikiwa ni pamoja na upokeaji wa maoni/mapingamizi dhidi ya maombi hayo mpaka hapo yatakapotolewa maelekezo mengine."

No comments
Post a Comment