Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Saturday, June 20, 2015

Prof Lipumba ampongeza rais Kikwete kwa kufanikiwa kuimarisha ofisi ya CAG.

Dar es Salaam. Viongozi wa vyama vya siasa vya CUF, NCCR-Mageuzi, NLD na ACT-Wazalendo wameitupia lawama Serikali kwa kushindwa kutekeleza maagizo yanayotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Wakizungumza kwenye mdahalo wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kuhusu masuala ya Sera juzi jijini hapa, viongozi hao Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyetiki wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe walisema kuwepo kwa mfumo mbovu serikalini na kukithiri kwa rushwa ndiyo chanjo cha kupuuzwa kwa ripoti za CAG. Kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi maalumu wa miaka mitano ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG, imeeleza bayana kumekuwepo na ufisadi wa takribani Sh600 bilioni zilizochotwa katika matumizi mbalimbali ambayo hayana maelezo ya kutosha. Ripoti hiyo maalumu inaonyesha kuwa uovu huo umekuwa ukiwezekana kutokana na mapendekezo ya CAG ya kuziba mianya ya upotevu wa fedha, kutofanyiwa kazi. Akifungua mdahalo huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEOrt), Ali Mufuruki alisema kuwa awali mdahalo huo uliwalenga wagombea kiti cha urais, lakini kwa kuwa wengi walishindwa kushiriki kwa sababu mbalimbali, sasa utaitwa mdahalo wa uchaguzi mkuu kuhusu sera. “Ni matumaini yetu kuwa kushiriki mdahalo kwa njia hii kutaleta ujumbe ule ule tuliokuwa tumeukusudia kutoka kwa waliotangaza nia, ambapo masuala ya uchumi, utawala bora na utawala wa sheria yatakuwa msingi wa mazungumzo,” alisema Mufuruki. Akijibu swali kuhusu kupuuzwa kwa ripoti za CAG, Zitto alisema kuwa ili kazi ya CAG iwe bora ni vyema idara za Polisi, Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zishirikishwe katika kuchukua hatua zinazostahili. “Kuijadili ripoti ya CAG pekee yake haitoshi. Tatizo hili linatokana na kuwepo kwa mfumo wa kuiwajibisha Serikali, wananchi wanahitaji wafahamu wabunge wanatakiwa kuunda kamati nzuri ya kukagua hesabu za serikali,”alisema Zitto. Kwa upande wake Mbatia alisema ripoti za CAG zimekuwa zikiibua madudu yanayofanya Serikalini lakini hakuna mhusika anayechukuliwa hatua yoyote. Akitolea mfano, alisema kuwa fedha zilizotajwa na CAG kupotea mwaka zikigawanywa kila mstaafu anayeidai Serikali angelipwa Sh800, 000. Mbatia alisema ‘dawa’ ya kuidhibiti serikalini bungeni ni kwa kuhakikisha kuwa hakuna chama kinachokuwa na zaidi ya asilimia 40 ya wabunge wote. Alisema kwa kufanya hivyo, wabunge watakuwa na nguvu ya kutoa maamuzi ya pamoja. “Jiulize kwanini mapato yasiyo ya kodi yanazidi kushuka wakati bajeti inazidi kuongezeka. Hakuna nidhamu ya matumizi, hii ya kutengeneza bajeti ni kuwadanganya Watanzania,” alisema Mbatia. “Nafikiria kwa hali ilivyosasa tuweke watu ambao si wala rushwa na kupunguza nguvu ya CCM. Ndani ya Bunge watu wanapokea rushwa hawawezi kutekeleza ripoti ya CAG,” alisema Makaidi na kuongeza kuwa hata bajeti zinazoandaliwa bungeni huanza ‘kutafununwa’ siku ya pili baada ya kupitishwa kutokana na kukithiri kwa rushwa. Akitumia dakika zake tatu kuelezea msimamo wa chama chake kuhusu ripoti za CAG, Profesa Lipumba alisema kuwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete kunyooshewa kidole kwa kushindwa kutekeleza mambo kadhaa, anampongeza kwa kufanikiwa kuimarisha ofisi ya CAG. “Jambo kubwa sasa ni kwa taarifa hizo kufanyiwa kazi. Katika kesi za Escrow kuna makosa ya wazi, lakini mpaka sasa watu hawajawajibishwa,” alisema Profesa. Kuhusu ajira Pia, viongozi hao wa vyama waliulizwa watatumia mikakati gani kupunguza tatizo la ajira nchini iwapo watapewa ridhaa na wananchi kuongoza nchi. Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa ndiye aliyekuwa wa kwanza kujibu swali hilo kwa kusema kuwa sekta binafsi ikishirkiana na Serikali ina nafasi kubwa kuhakikisha kuwa ajira zinapatikana. Suala la kuwapa wazawa nafasi ya kwanza liliibuliwa na Dk Makaidi, aliyesema kuwa sera ya vijana inapaswa kuweka kipaumbele kwa wazawa kwa kuwa kufanya hivyo siyo kuhubiri ubaguzi. Kwa upande wake mtaalam wa uchumi, Profesa Lipumba alisema chama chake kitatumia fursa ya kijiografia iliyopo nchini kwa kuhakikisha bandari zinatumika vizuri kuhudumia nchi jirani na hivyo kuongeza ajira kwa wananchi. Zitto, alisema itakapofika mwaka 2030 Tanzania itakuwa na vijana milioni 36, na ongezeko hilo linahitaji kufanyiwa maandalizi. Chanzo: gazeti la mwananchi
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment