Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Saturday, June 27, 2015

Mwandosya amuita Lowassa kambi yake

Dodoma. Profesa Mark Mwandosya, ambaye anawania kuteuliwa na CCM kugombea urais, amemtaka Edward Lowassa kujiunga na kambi yake kwa kuwa makada wengine wanne kwenye mbio hizo wanamuunga mkono. Hata hivyo, wawili kati ya makada hao wanne wamekana kumuunga mkono. Mwandosya, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), alisema tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Steven Wasira, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wanamuunga mkono na hivyo kumshauri Lowassa kujiunga na kambi yake. “Kama (wagombea) wengi wananiunga mkono, aliyebakia basi atakuwa ni ndugu yangu, rafiki yangu, Edward Lowassa. Naye angesema hivyo ingerahisisha sana kazi ya chama, ingepunguza sana kazi, makundi yangekuwa yameisha,” alisema Mwandosya baada ya kurejesha fomu za kuomba CCM impitishe kugombea urais. “Halmashauri Kuu isingepata shida, Kamati Kuu isingepata shida nadhani tungeweza kufika pale ambako tungefika tarehe 12 (Julai, siku ambayo Mkutano Mkuu wa CCM utamchagua mgombea urais), bila kikwazo, bila makundi,”alisema mbunge huyo wa Rungwe Mashariki jana. Lakini kauli yake imepokewa kwa hisia tofauti na watu hao aliodai wanamuunga mkono, huku kambi ya Lowassa ikizungumzia kauli hiyo kuwa si ya mtu aliye makini kwenye mbio za urais. Jumla ya makada 40 wamechukua fomu za kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25 na chama hicho kina kazi ngumu ya kumpata mwanachama atakayemrithi Rais wa sasa, Jakaya Kikwete ambaye katiba inamzuia kuendelee kuongoza baada ya kumaliza vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja. Mgombea urais wa CCM pia ndio atakuwa mwenyekiti wa chama hicho. Akizungumza mara baada ya kurudisha fomu jana, Profesa Mwandosya alisema mchakato huo umewafanya wanaoomba urais kuwa marafiki zaidi licha ya kupigana vijembe, akisema ingekuwa nchi nyingine wangefanyiana vurugu. Aliwashukuru wagombea wenzake waliotamka hadharani kuwa watamuunga mkono endapo hawatapitishwa na Kamati Kuu ya CCM kugombea urais. “Namshukuru Benard Membe ambaye ametangaza na kuandikwa (kwenye vyombo vya habari) kwamba yeye ameona katika orodha yote ya watu 40, kama si yeye basi ataniunga mkono mimi na yupo tayari kuzunguka nchi nzima iwapo chama kitaniteua kuwa mgombea,” alisema Profesa Mwandosya. “Namshukuru pia Mheshimiwa Pinda, amelizungumzia hili katika vituo kama si kimoja viwili kuwa moyo wake utakuwa na furaha kama Profesa Mwandosya anaweza kuteuliwa na chama.” Alisema pia kuna baadhi ya wagombea wenzake waliochukua fomu wamesema kwa kupitia mameneja wao wa kampeni kuwa nao wanafikiria kumuunga mkono Mwandosya na kwamba jambo hilo limempa faraja kubwa. “Baadhi ya mameneja wa rafiki yangu sana Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira ni kati ya wale ambao wamesema, lakini hawajasema hadharani sasa sijui kama ninatoa siri au,” alisema Mwandosya ambaye alijitokeza mwaka 2005 kuomba ridhaa ya CCM na kushika nafasi ya tatu. “Na sidhani kwamba Mheshimiwa Sitta atakataa... hataniunga mkono. Kama nikiteuliwa basi ni kundi kubwa. Hilo linatosha kabisa kunivusha, lakini yote haya tutategemea vikao na maamuzi ya chama.” Alisema hayo ndiyo matarajio yake na bila shaka ni ya Watanzania wote. “Mimi nimuogope nani tena? Mimi namuogopa Mwenyezi Mungu. Si kumuogopa tu bali ni kumnyenyekea na kumshukuru kwa yote,”alisema Profesa Mwandosya. Bashe anena Lakini kauli hiyo haikuwa nzuri kwenye kambi ya Lowassa. Mjumbe wa kamati yake ya kampeni, Hussein Bashe alimtaka Prof Mwandosya atatafakari mara mbili wito wake. Bashe alisema anafahamu kuwa waliotangaza kumuunga mkono (Profesa Mwandosya) sio wagombea urais kwa sababu nia yao si kuongoza nchi wala chama chao cha CCM. Alisema Membe alitangaza kumuunga Profesa Mwandosya, akiwa mkoani Mbeya na akafanya hivyo tena mkoni Mara, lakini alimuunga mkono Makongoro Nyerere, ambaye pia anawania kuteuliwa na CCM kugombea urais. “Mwandosya anafahamu katika uchaguzi wa mwaka huu kuna wagombea urais, wagombea vikoba, wachekeshaji na watu makini wenye nia thabiti ya kuongoza nchi na chama chetu,” alisema bashe. Chanzo Mwananchi
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment