Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Thursday, January 23, 2014

JK kukamilisha uteuzi wa Bunge la Katiba

Rais Jakaya Kikwete.PICHA|MAKTABA 
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete, wiki ijayo atakamilisha uteuzi wa majina ya wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba, uteuzi unaoashiria kuanza kwa bunge hilo litakalokuwa na wajumbe 640.
Bunge hilo litakaloanza mwanzoni mwa mwezi ujao mjini Dodoma, litakuwa na kazi ya kuijadili na kuipitisha Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Desemba 30 mwaka jana.
Wajumbe wengine watakaounda Bunge hilo ni 42 kutoka vyama vya siasa, 358 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na 81 kutoka Baraza la Wawakilishi.
Januari 2 mwaka huu, ilikuwa siku ya mwisho kwa Ikulu kupokea majina ya makundi mbalimbali ya kijamii ambayo yaliwasilisha mapendekezo ya majina ya watu ambao wangependa wawe wajumbe wa Bunge hilo. Makundi zaidi ya 50 yaliwasilisha majina yao.
Makundi hayo ni asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya Serikali, vyama vya kitaaluma, madhehebu ya dini na vyama vya siasa.
Kuanza kwa Bunge hilo kunatarajiwa kuwa na mvutano mkali kutokana na msimamo wa baadhi ya makundi hayo, hasa vyama vya siasa ambavyo vimekuwa vikipingana zaidi katika mfumo wa Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, ilisema mbali na uteuzi huo, Rais Kikwete pia Ijumaa hii ataichapisha rasimu ya pili ya katiba katika Gazeti la Serikali.
Taarifa hiyo ilisema hata majina ya wajumbe wa Bunge la Katiba nayo yatatangazwa katika Gazeti la Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013. Sheria hiyo inampa madaraka Rais wa Jamhuri ya Muungano kushauriana na Rais wa Zanzibar, kuteua wajumbe 201 wa Bunge la Katiba.
Pia inamtaka rais kuchapisha kwenye Gazeti la Serikali rasimu ya katiba ndani ya siku 30 baada ya kukabidhiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Atateua wajumbe 201 wa Bunge la Katiba kutoka miongoni mwa majina yanayopendekezwa kwao na makundi yaliyotajwa ndani ya sheria hiyo,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Inaeleza kuwa rasimu ya katiba itachapishwa katika Gazeti la Serikali la Januari 24 mwaka huu.
Historia ya Tanzania kuwa na Katiba Mpya itakayotokana na maoni ya wananchi ilianza Desemba 31 mwaka 2011 wakati Rais Kikwete akilihutubia taifa.
Alitamka wazi kuwa nchi sasa inahitajika Katiba Mpya ili kwenda na wakati. Baadaye aliwateua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, tume ambayo ilianza kazi ya kukusanya maoni ya wananchi Mei 3, mwaka 2012.
Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi nchi nzima na kuandaa rasimu ya kwanza ya katiba ambayo ilitoka Juni 4 mwaka jana.
Baada ya kutolewa rasimu hiyo wananchi walipewa muda wa kuipitia na kuitolea maoni katika Mabaraza ya Katiba ya wilaya yaliyokaa kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2 mwaka jana.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment