Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, October 22, 2013

Ukuaji Pato la Taifa waongezeka


Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dar es Salaam, Morrice Oyuke akiwaeleza waandishi jinsi Pato la Taifa lilivyokua kwa robo mwaka kati ya kipindi cha mwezi Aprili na Juni, wakati wa mkutano na waandishi jijini Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao 
Na Aidan Mhando, Mwananchi
Dar es Salaam. Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imesema Pato la Taifa kwa bei za soko limeongezeka kwa asilimia 6.7 katika kipindi cha robo ya pili mwaka 2013 kuanzia mwezi Aprili hadi Juni, ikilinganishwa na asilimia 6.4 ya mwaka 2012.
Pia, imesema jumla ya thamani ya pato la taifa kwa mwaka huu ni Sh5 milioni ikilinganishwa na Sh4.6 milioni kwa mwaka jana.
Akitoa taarifa ya ukuaji wa pato hilo kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, Morrice Oyuke alisema sababu za kuongezeka kwa pato la taifa ni kuwepo kwa ongezeko kubwa la uzalishaji wa bidhaa.
“Kwa kweli mwaka huu umekuwa mzuri kwa taifa, kwani pato limekuwa ukilinganisha na mwaka jana, lakini hayo yote yanatokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa mfano mahindi, mchele jambo ambalo linasababisha bei kushuka,”alisema Oyuke.
Kilimo
Akizungumzia ukuaji wa shughuli za kilimo Oyuke alisema, “Kilimo kimefanya vizuri kwenye ukuaji wa uchumi, kwani kwa kipindi cha robo ya mwaka huu shughuli zinazotokana na sekta hiyo zimekuwa kwa asilimia 5.3 ilikinganishwa na asilimia 5.1 kwa mwaka jana jambo ambalo tunajivunia.”
Aidha, mbali na kukua kwa pato la taifa, Okuye alibainisha kuwa kuna maeneo ambayo yamepungua kwa uzalishaji, lakini kutokana na takwimu zilizopo zinaonyesha bado maeneo hayo yanafanya vizuri, kwani yapo kwenye mwelekeo chanya.
Bidhaa za viwandani
Akizungumzia maeneo ya uzalishaji wa bidhaa za viwandani alisema, “Shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani zipo kwenye asilimia 5.8 kwa kipindi cha robo ya mwaka huu tofauti na mwaka jana ambapo ilikuwa asilimia 8.2,” aliongeza.
Umeme
Akizungumzia uzalishaji wa nishati ya umeme, alisema takwimu zinaonyesha kumekuwa na ongezeko kubwa ikilinganishwa na mwaka jana.
Alisema mwaka huu kumekuwa na ongezeko la asilimia 5.6 ikilinganishwa na kuporomoka kwa kasi ya ukuaji wa nishati hiyo kwa mwaka jana ambayo ilikuwa asilimia 1.1.Uchimbaji madini
Akizungumzia shughuli za uchimbaji madini, mawe na kokoto alisema, Shughuli hizo zimeongezeka kwa asilimia 4.3 kwa robo ya mwaka huu, ikilinganishwa na kuporomoka kwa asilimia 5.1 kwa mwaka jana.
Oyuke alitaja sababu za kuongezeka kwa shughuli hizo kwamba ni upatikanaji wa madini hasa almasi, Tanzanite na kukua kwa uzalishaji kwa robo ya mwaka huu.
Aidha, upande wa uchukuzi na mawasiliano, Oyuke alisema, “Ukuaji wa masuala ya uchukuzi yamefikia asilimia 14.8 kwa mwaka huu, hoteli na migahawa asilimia 3.2, uendeshaji serikali asilimia 5.0, elimu asilimia 5.7, uvuvi asilimia 2.4 ikilinganishwa na asilimia 6.5 kwa mwaka jana, huduma za afya na huduma na nyinginezo zimekua kwa asilimia 3.8.”
Katika hatua nyingine, mkurugenzi huyo alisema kwa Nchi za Afrika Mashariki Tanzania inashika nafasi ya pili kwenye ukuaji wa uchumi ambapo Rwanda inaongoza.
Alisema kwenye ukubwa wa uchumi Tanzania inaongoza ikifuatiwa na Kenya.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment