Writen by
sadataley
7:49 PM
-
0
Comments
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome
Dar es Salaam. Siku moja baada ya maudhui ya Ripoti ya Tume iliyoundwa kuchunguza matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana kuwekwa wazi, wadau wa elimu wamekiri na kusema kuwa mfumo wa elimu ya Tanzania upo katika hali mbaya.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mbunge wa kuteuliwa na Rais, James Mbatia alisema matokeo ya tume hiyo yanaonyesha udhaifu wa hali ya juu katika sekta ya elimu jambo ambalo alishawahi kulisema katika hoja maalumu bungeni.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, alisema alishawahi kuishauri Serikali kuufumua mfumo wa elimu nchini na kuanza upya ili kunusuru taifa la kesho ambalo ndilo linaloathirika na rasilimali watu zisizo na ubora.
Matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana yalionyesha kuwa asilimia 60.6 ya wanafunzi Tanzania walipata alama sifuri na wanafunzi 23,520 sawa na asilimia tano ndiyo waliofaulu jambo ambalo lilisababisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuunda tume ya kuchunguza matokeo hayo.
Baadaye, mitihani hiyo ilisahihishwa upya na Pinda kukabidhiwa matokeo Juni, mwaka huu.
“Nilishasema katika hoja yangu bungeni Januari 31 na Februari 1, mwaka huu nikamwomba waziri anionyeshe mitaala ya elimu ya sasa, lakini hakuitoa,” alisema Mbatia.
Mbatia alisema ili taifa hili liondokane na janga la elimu lililopo halina budi kukubali kuwa ni kweli Tanzania ipo katika janga la elimu na kuunda dira ya elimu itakayotuongoza katika safari ya elimu nchini.
Mbatia aliongeza kuwa elimu ya Tanzania ipo mahututi na kuwa kila mwaka wanafunzi wanaomaliza katika shule mbalimbali hawana sifa za kutosha za kuweza kushindana katika masoko ya kimataifa.
“Tumeshaanza kuona taifa linaangamia kwa sababu ya ubovu wa elimu, ni lazima tukiri hilo kwa sababu hata Rais alikiri na kuikubali hoja yangu Aprili 30 mwaka huu alipokuwa mkoani Mbeya” alisema Mbatia
Mbunge huyu ambaye awali aliteuliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa tume ya uchunguzi wa matokeo haya na kukataa kushiriki alisema, ili Serikali iondokane na janga hili haina budi kuunda Kamati ya Bunge ambayo itaisimamia Serikali na kutoa mawazo mapana kuhusu elimu.
Mbatia alishauri Bunge lisiegemee itikadi za vyama au porojo za kutaka sifa za kisiasa na badala yake suala la elimu lijadiliwe kwa maslahi ya taifa.
Mdau mwingine wa elimu, Dk Method Samwel, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUSE), alisema tatizo la elimu hapa nchini lielekezwe zaidi kwenye mfumo uliopo kuliko laumu taasisi au mtu mmoja mmoja.Dk Samwel alisema tangu zamani mfumo wa elimu umekuwa ni wa kudorora na haya ni matokeo ya mfumo huo ambao haukuwa na misingi imara kwa muda mrefu.
Alitolea mfano wanaokwenda kusomea ualimu wengi ni wale waliofeli kwa kupata daraja la nne, jambo ambalo linasababisha wataalamu wa kada hiyo kuwa ni wale waliofeli pekee.
“Yapo mambo mengi yanayotakiwa kufanyiwa kazi katika sekta ya elimu Tanzania, suala la kudai kuwa Baraza la Mitihani na Taasisi kuwa ndizo taasisi zenye makosa, hazina ukweli,” alisema.
Hata hivyo, Dk Samwel alisema, tume hiyo bado ina maswali mengi ya kujibu kulingana na walichokisema katika sehemu ya ripoti yao.
“Nashindwa kuelewa kwa sababu kila nikisoma majibu ya tume hiyo napata maswali mengi zaidi. Kwa mfano, walimu waliofanya mtihani wakafeli walipewa muda wa kujiandaa? “ alihoji na kuongeza:
“Na kuhusu mitihani ya Tanzania kuonekana kuwa ni migumu zaidi, Je waliwapa mitihani ya Tanzania wanafunzi wa nchi nyingine au walitumia mbinu gani kupata matokeo hayo?”
Hata hivyo, Mkuu wa Kitivo cha Elimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo, alipinga ripoti ya tume hiyo na kusema kuwa wamepotosha taarifa kwani tatizo halikuwa katika mtihani bali ni wanafunzi wenyewe wamefeli.
Dk Mkumbo amesema tatizo si la walimu, wala baraza, wala mitihani yenyewe bali ukweli utabaki kuwa wanafunzi walifeli mtihani wa Kidato cha Nne kwa sababu ya mfumo mbovu wa elimu.
Mhadhiri huyo alihoji tena kuwa tume hiyo ilitumia njia gani kujua kuwa mtihani wa Sayansi ulihitaji saa sita kuufanya na ni kwa mbinu gani waliupima mtihani wa Tanzania na kujua kuwa ni mgumu kuliko mitihani mingine.
“Nilipata ripoti fulani iliyoonyesha kuwa mitihani ya Tanzania ni mizuri na haina matatizo, ripoti ilionyesha kuwa haina chembe ya mashaka na inatungwa kwa ustadi. Tusitafute sababu, tatizo si mitihani ni wanafunzi wenyewe wamefeli,” alisema.
Pia, Dk Mkumbo alisema kuwa ni dharau kubwa kusema kuwa baadhi ya wasahihishaji hawakuwa na sifa kwani hilo ni tusi kubwa kwa walimu kwani wao ndiyo wamekuwa wakisahihisha kila siku.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi nchini,(Tamongsco), Albert Katagira alisema si kweli kuwa mtihani ulikuwa mgumu bali tatizo lipo katika uandaaji wa wanafunzi.“Mtihani ulikuwan sahihi kabisa, mbona wanafunzi wengine walifaulu. Ni wanafunzi wenyewe, ambao nao hatuwezi kuwalaumu moja kwa moja,” alisema Katagira.
Alisema taifa bado lina tatizo katika mfumo wa elimu na kuweka mkazo katika masomo ya sayansi na hisabati ambayo yanaonekana kuwa magumu kwa wanafunzi wengi.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mafinga, Mustapha Mambea alisema, mtihani wa Fizikia na Kemia haikuwa migumu, lakini kuna mada kadhaa ambazo hawakufundishwa.
Profesa Mchome aongea
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alisema kuwa wameshindwa kuiweka hadharani ripoti hiyo kwa kuwa bado inafanyiwa kazi serikalini.
Profesa Mchome, ambaye ndio aliongoza tume hiyo, alisema kuwa ripoti hiyo inatakiwa kupelekwa kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kujadiliwa.
Alidokeza, hata hivyo, tayari walikuwa wameanza kufanyia kazi baadhi ya vitu vinavyotakiwa kufanyiwa kazi haraka kwenye ripoti hiyo.
Katibu Mkuu wa Necta, Dk Joyce Ndalichako, ambaye ameomba likizo ya muda mrefu ikitafsiriwa pengine ndio mwanzo wa utekelezaji wa ripoti hiyo.
Chanzo:www.mwananchi.co.tz
No comments
Post a Comment