Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Friday, July 19, 2013

Serikali yazidiwa nguvu kodi ya simu

                                                               Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa 
Dar es Salaam. Kuna kila dalili kwamba Serikali inajipanga kufuta kodi ya Sh1,000 kila mwezi kwa wamiliki wa laini za simu baada ya kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi, taasisi na baadhi ya kampuni za simu nchini.
Hiyo inatokana na kauli ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba aliyoitoa jana akisema kwamba wizara yake ilipinga tangu awali mpango huo kabla ya kupitishwa na kuwa sheria na kwamba anaamini itaondolewa. Kauli hiyo ya Makamba imekuja siku moja baada ya chama tawala, CCM, kukaririwa na vyombo vya habari kikiitaka Serikali kuangalia vyanzo vingine vya mapato badala ya tozo hiyo.
Akizungumza kwa simu jana Makamba alisema: “Sikubaliani na hili suala na kupita kwake ilikuwa ni kuzidiwa nguvu. Lakini najua haliwezi likatekelezeka ni lazima litabadilishwa kwa kuangalia eneo lingine la kutoza kodi.”
Alisema msimamo wa wizara yake katika suala hilo ni tofauti kwani imekuwa ikijitahidi kuhakikisha gharama za mawasiliano zinapungua... “Wizara hatukubaliani na kodi hiyo. Nia yetu ni kupunguza gharama za kupiga simu kwa kuwa ni kitu kinachowezekana.
“Nia yetu ni kushusha gharama iwe sifuri kabisa, kitu chochote kinachopandishwa bei sisi hatukubaliani nacho kwa kuwa ni kuwaumiza wananchi wetu hasa wa vijijini. Bidhaa ambayo inatakiwa kushuka ni mawasiliano hivyo lazima iwe hivyo.”
Jana, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema kwamba Serikali inapokea maoni ya wadau mbalimbali ili kuona namna ya kufanya marekebisho ya tozo hiyo. Hata hivyo, alisema uamuzi wa kuanzisha tozo hiyo haukuwa wa Serikali bali ulipitishwa na kukubaliwa baada ya kujadiliana na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
“Hayo yalipendekezwa na Kamati ya Bunge siyo Serikali. Tena walipendekeza vyanzo 67 vya kodi likiwamo hilo la kadi za simu. Walipendekeza tukate Sh1,450 kwa mwezi, lakini sisi Serikali tukashusha hadi Sh1,000 yaani kila mwananchi akatwe Sh33.3 kwa siku na mapato yatakayopatikana yatakwenda kuboresha miradi ya maji, umeme vijijini na barabara,” alisema Dk Mgimwa.
Upinzani mkali
Wabunge wa Chadema, John Mnyika wa (Ubungo) na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), wamekuwa mstari wa mbele kupinga kodi kwa kuonyesha jinsi itakavyowanyanyasa wananchi.
Mnyika amekuwa akikusanya saini za wananchi wanaopinga mpango huo wa Serikali ili awasilishe bungeni hoja ya wananchi kupinga tozo hiyo. Hadi sasa ameshakusanya saini zaidi ya 26,000.
Kwa upande wake, Zitto alisema kodi hiyo haikujadiliwa kabisa kwa kuwa iliondolewa katika mapendekezo ya mapato lakini ikarejeshwa kupitia Muswada wa Fedha ambao hutafsiri hotuba ya Bajeti kisheria.
“Kama kodi hii haikuwa kwenye hutuba, haikujadiliwa na Bunge, msingi wa Muswada wa Fedha kuwa na kodi hii haupo. Kodi hii ilirejeshwa kinyemela bungeni na kupitishwa bila mjadala.”Hata hivyo, Dk Mgimwa alipinga hoja akisema muswada huo uliokuwa na kipengele cha tozo hiyo ulijadiliwa na kupitishwa na Bunge.
Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Gaudence Mpangala alisema kodi hiyo imelenga kuwakandamiza zaidi wananchi. “Hiyo kodi itawakandamiza wananchi wa chini wanaofanya kazi ndogondogo kujipatia kipato, lakini wazalishaji wakubwa hawataathirika. Tuendelee kulalamika hadi ifutwe, hatuwezi kuwa na ujenzi wa demokrasia kama watu wa ngazi ya chini wanakandamizwa,” alisema.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment