Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, July 2, 2013

Maelfu ‘walia’ kutomwona Obama


Dar es Salaam. Maelfu ya wakazi wa D Dar es Salaam, walijitokeza kwa wingi jana kumlaki Rais wa Marekani, Barack Obama aliyewasili nchini kwa ziara ya siku mbili inayohitimishwa leo huku wakilalamikia kutomwona.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, msafara wake ulipitia Barabara za Nyerere, Nkrumah, Samora, Magogoni hadi Ikulu.
Ukonga Majumba Sita
Wakazi wa maeneo ya Gongo la Mboto, Ukonga, Kitunda, na Tabata walifurika eneo la Majumba Sita kwa ajili ya kumwona, lakini hali ilikuwa tofauti.
Magari yalizuiwa kuanzia Njia panda ya Segerea na hayakuruhusiwa kusogea karibu na barabara inayotoka uwanja wa ndege. “Mimi nimefika hapa kwa ajili ya kumwona, sikumwona jamani yaani nimepigwa na jua bure,” alilalamika dada mmoja akiwa na wenzake huku ameshikilia kandambili mkononi.
Naye Mkazi wa Tabata Mawezi, aliyejitambulisha kwa jina la Jana Kamanzi alilalamikia mwendo kasi wa magari hayo na kushindwa kumuona kiongozi huyo.
Kipawa/Jeti Lumo
Maeneo hayo walijitokeza watu wengi huku wengine wakiwa na mikeka ya kukalia tayari kumlaki kiongozi huyo.
Gazeti hili lilishuhudia umati huo kwa wakazi kutoka maeneo ya Jeti, Kipawa, Karakata waliofika kumlaki Rais huyo wa Marekani.
Baadhi ya mama lishe walitumia nafasi hiyo kuuza chakula kwenye ndoo za plastiki kwa kificho, huku wafanyabiashara ya maji na wao wakitumia nafasi hiyo kupandisha bei ya maji huku wakiuza kwa kificho.
Vingunguti
Katika maeneo ya Vingunguti, umati ulifurika pande zote mbili za barabara kwa wakazi wa Vingunguti na Kijiwe Samli wakiwamo wafanyakazi ambao ofisi zao ziko karibu na Barabara ya Nyerere.Maafisa Usalama waliokuwa wamejichanganya na wananchi, walimkamata mama mmoja aliyekuwa akijaribu kuvuka barabara kabla ya msafara wa Rais Jakaya Kikwete kupita wakati akienda kumpokea mwenyeji wake, Rais Obama.
Kwa kuwa kila mmoja alikuwa akimwangalia, wakati anajiandaa kukatisha barabara na msafara unakuja, walimkimbilia na kumdaka na kisha kuondoka naye. Hata hivyo haikuweza kufahamika mama huyo alikuwa na lengo gani.
Magari yalizuiwa kutoka Vingunguti na hata yale yanayotokea Kijiwe Samli, barabara zake zinaingia Barabara ya Nyerere.
Baadhi ya wakazi hao walisikika wakilalamika kutomwona Rais Obama kwani walitarajia angekuwa kwenye gari la wazi waweze kumuona.
Wakazi wengine walilalamikia hali hiyo, mbali na kutotarajia umati na kushindwa kumwona, walijua kuwa atakuwa kwenye gari la wazi ambalo wangeweza kumuona.
Makutano ya Mandela na Nyerere (Tazara)
Wananchi walivamia msafara wa Rais Obama katika eneo la Tazara na kusababisha msafara huo kupunguza mwendo.
Kitendo hicho kilitokea wakati Rais huyo na msafara wake uliokuwa na zaidi ya magari 15 ukitoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ukienda Ikulu.
Msafara wa Rais Obama haukuwa katika mwendo wa kasi na ulipokaribia makutano ya barabara hizo maeneo ya Tazara, wananchi walivuka kutoka upande wa pili kushuhudia msafara huo kwa ukaribu zaidi.
Kitendo hicho cha wananchi kuvamia msafara huo kwa ghafla kiliwachanganya askari polisi waliokuwa wachache, hivyo kusababisha msafara huo kupunguza mwendo.
Awali askari Polisi waliimarisha ulinzi na kuwazuia watu kuvuka barabara kutokana na magari kupita kwa kasi eneo hilo na wananchi walitiii amari hiyo.
Njia Panda ya VetaKatika maeneo yanayounganisha Barabara ya Nyerere na Chang’ombe, polisi walifanya kazi ya ziada kuzuia mamia ya watu waliofika kumlaki .
Mamia ya watu hao kutoka Temeke, Chang’ombe, Tandika, Ilala walifurika katika eneo hilo kutaka kumuona kiongozi huyo, lakini hata hivyo wengi walisikika pia wakilalamikia kutomwona.
Kamata
Wakazi wa maeneo ya Kariakoo, Gerezani, Ilala walifurika kuanzia njia panda ya Shauri Moyo huku wakiwa katika hali ya utulivu.
Polisi walikuwa na kazi ya kuzuia wakazi hao waliokuwa wanavuka barabara kabla na baada ya misafara kupita.
Mtaa wa Nkrumah
Hali ilikuwa tete katika Mtaa wa Nkrumah ambako ulipita msafara wa Obama wakati akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.Msafara wa Rais Obama ulipita katika Mtaa wa Nkrumah kwa ajili ya kuingia Mtaa wa Samora kuelekea Ikulu.
Maduka na ofisi kadhaa zilizoko maeneo ya Nkrumah, Kidongo Chekundu na Mnazi Mmoja yalifungwa kutokana na watu kuwa na hamu ya kuuona msafara wa Obama. Watu walikuwa wengi pande zote za barabara na msafara wa Obama ulipofika kwenye eneo hilo, watu walimshangilia kwa nguvu.
Hata hivyo, watu wengi walisikitishwa na kitendo cha kutomwona Obama kwani wengi walitegemea kuwa watapanda gari lenye vioo ambavyo wangeweza kumwona kwa urahisi wakati akipita katika eneo hilo la Nkrumah.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment