UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

Saturday, April 7, 2018

" Wizi ni tatizo kubwa kwenye vyama vya ushirika"- RC Kigoma

Serikali mkoa wa Kigoma imesema wizi na ubadhirifu wa mali za ushirika ni tatizo kubwa katika baadhi ya vyama kutokana na viongozi wake kufanya vitendo vya wizi wakishirikiana na baadhi ya wanachama wasio waadilifu.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa Kigoma, Emanuel Maganga mjini hapa ambapo amesema ushirika ni muhimu katika kujenga viwanda na kuwa na uchumi wa kati, kuongeza ajira na maisha ya watu kuwa bora zaidi.

“Tunataka ushirika unaolenga kuchakata mazao ya wakulima badala ya kuuza malighafi kwa ajili ya kuongeza thamani na kipato cha kaya, hivyo ni lazima vyama vya ushirika viongozwe na watu waadilifu na wenye utashi wa kuleta maendeleo katika jamii zao,” alisema Maganga.

Aliwataka wanachama wa ushirika kuwakataa watu wanaoleta migogoro kwenye vyama kwa kuwa lengo lao ni kuvuruga umoja na mshikamano kwa maslahi yao binafsi, hivyo lazima waepukwe.

Maganga alisema ushirika hautakuwa na maana kama wanaushirika na wananchi kwa jumla hawataona manufaa yake hasa katika dhana nzima ya kuongeza uzalishaji na kuwa na uhakika wa masoko ya mazao wanayolima.

Aliwataka wakulima kutumia ushirika wao kwenye sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, madini na sacos kuanzisha viwanda vidogo na vya kati kwa ajili ya kuchakata mazao na kuongeza thamani ili kuleta ushindani katika soko na kuongeza kipato.

Kuhusu masoko, Maganga alisema Kigoma inapakana na nchi za Burundi na DR Congo ambazo zinategemea chakula na bidhaa nyingine kutoka Tanzania, hasa mkoa wa Kigoma.

“Wakulima wakitumia vizuri soko la mashariki ya nchi ya DR Congo, Burundi na baadhi ya mikoa hapa nchini wataweza kupata fedha nyingi baada ya mauzo ya bidhaa, tatizo lililopo ni bidhaa hizo kuuzwa zikiwa ghafi, ni lazima zichakatwe kwanza na hicho ni kipaumbele chetu kama mkoa,” alisema.

 Mrajisi msaidizi wa ushirika mkoa wa Kigoma, John Runahi alitaja vyama 113 vya ushirika wa mazao, SACCOS zipo 233 huku vyama vikuu vilivyopo ni viwili tu, kimoja kipo wilaya ya Uvinza na kingine wilaya ya Kigoma.

Ushirika wa uvuvi kuna vyama tisa kama ilivyo kwenye ufugaji nyuki, viwanda kuna vyama vitano na ushirika wa madini vipo vyama viwili, ambapo mkoa wa Kigoma una jumla ya vyama vya ushirika 389 vyenye wanachama 51,700 ambapo wanaume wapo 33,179 na kinamama ni 18,521.

Yahya Mahwisa aliyekuwa mwenyekiti wa vyama vya ushirika vya Rumako na Kanyovu kwa muda mrefu alisema ushirika unakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa mitaji ya kutosha kwa ajili ya kununulia pembejeo za kilimo, kulipa malipo ya awali kwa wakulima.

Serikali haina budi kusimamia kwa karibu vyama vya ushirika kwa vile ndio mkombozi kwa mkulima kuongeza kipato kwani wengi wanaouza mazao kwenye soko huria wamekuwa wakipunjika ikilinganishwa na watu waliojiunga katika ushirika.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment