WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kuridhishwa na maendeleo yake.
Mradi wa ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Juni 2019 na utakuwa na uwezo wa kuegesha ndege kubwa 24 kwa wakati mmoja, pamoja na kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka.
Waziri Mkuu ambaye ametembelea mradi huo leo (Ijumaa, Machi 23, 2018) amesema amefarijika na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo pamoja na kukuta Watanzania wengi wakishiriki katika kazi za ujenzi.
“Serikali imejiimarisha katika kuboresha usafiri wa anga, ambapo kukamilika kwa jengo hili kutachangia ongezeko la ndege kubwa nyingi kutua nchini. Pia sekta ya utalii nayo itaimarika kwa kuwa watalii wanaoingia nchiniwataongezeka.”
Mbali na ujenzi wa jengo hilo, pia Serikali inaendelea kuvikarabati viwanja mbalimbali vya ndege nchini kikiwemo cha Musoma, Iringa, Kilwa Masoko, Lake Manyara, Lindi, Moshi, Njombe, Tanga, Simiyu, Singida na Songea ili kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini.
Akisoma taarifa za ujenzi wa mradi Mkurugenzi wa Miradi wa TANROADS, Mhandisi Christianus Ako amesema mradi huo umeajiri wafanyakazi 1,400 kwa sasa na wanatarajia kuongeza watumishi na kufikia 1,800.
Pia wanatarajia kufanya majaribio ya kwanza ya mifumo na vifaa vya umeme kuanzia Julai, 2018 kwa kuwa tayari utekelezaji wa kazi kubwa za ujenzi wa mradi huo zimefanyika.
No comments
Post a Comment