MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)Prof. Mussa Assad ametolea ufafanuzi wa Deni la Taifa ambapo hadi kufikia Juni 30, 2017 lilikuwa ni Sh.Trilioni 46.08.
Jumanne wiki hii, Prof. Assad akiwasilisha ripoti zake za ukaguzi wa mwaka wa Fedha ulioishia Juni mwaka jana kwa Rais John Magufuli alisema kuwa deni hilo ni Sh.Trilioni 46 kutoka Trilioni 41 la mwaka uliopita ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 12.
Akitoa ufafanuzi wa deni hilo jana, Prof. Assad aliwaomba radhi wa wananchi na serikali kwa usumbufu uliojitokeza kuhusu taarifa ya deni hilo alipokuwa akimkabidhi ripoti kwa Rais Magufuli.
Alisema kati ya deni hilo, Sh.Trilioni 13.34 sawa na asilimia 29 ni za deni la ndani na Deni la Nje ni Sh.Trilioni 32.75 sawa na asilimia 71.
“Kwa hiyo, deni la nje ni asilimia 31 ya Pato la Taifa(GDP).Vilevile ukaguzi umebaini kuwa Deni la Taifa kwasasa ni himilivu,”alisema.
Hata hivyo alisema bado ripoti za CAG za ukaguzi wa mwaka huo zitabaki kuwa za siri kwa umma hadi zitakapowasilishwa bungeni.
Alifafanua CAG huwasilisha taarifa zake kwa mujibu wa Ibara ya 143(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 iliyorekebishwa mwaka 2005.
“Licha ya tukio hili kurushwa mubashara na Kituo cha Televisheni cha Taifa(TBC1), kwa mujibu wa Ibara tajwa ripoti hizi bado ni siri hadi zitakapowasilishwa bungeni,”alisisitiza.
Alibainisha kuwa tukio la uwasilishaji linatarajiwa kufanyika kabla ya Aprili 12, mwaka huu katika kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa kwa Rais.
“Hivyo, matokeo ya ukaguzi yatawekwa wazi kwa Umma baada ya ripoti hizi kuwasilishwa bungeni rasmi…naomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza kwa wananchi,”alisema.
No comments
Post a Comment