Writen by
sadataley
1:01 PM
-
0
Comments
Na Hassan Silayo-MAELEZO
Kuanzia 02 Machi, 2017 Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alianza ziara
ya kikazi ya siku 4 katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara iliyolenga
kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi
katika mikutano ya hadhara.
Ziara hiyo kwa kiasi kikubwa
imeonesha dira na mwelekeo wa serikali ya awamu ya tano hasa katika
utekelezaji wa miradi inayolenga kuwaletea wananchi maendeleo bila
kujali Imani,kabila na itikadi za vyama vyao vya siasa.
Siku ya kwanza ya ziara yake Rais Dkt. Magufuli aliweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles)
cha Tanzania Goodwill Ceramic Tiles Ltd. kilichopo Mkuranga Mkoani
Pwani ambacho ni kikubwa Afrika Mashariki na Kati kilichogharimu Dola za
Marekani Milioni 50 kwa awamu ya kwanza.
Akiongea katika hafla ya uwekaji
wa jiwe la msingi katika kiwanda chenye uwezo wa kuzalisha mita za mraba
80,000 za vigae kwa siku Rais Magufuli alifurahishwa na teknolojia ya
kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae inayotumiwa na kiwanda hicho na
kuhoji kama kuna haja ya serikali kuendelea kusafirisha mchanga wa
madini nje ya nchi.
Rais Magufuli alisema kuwa “Nchi
hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa
kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga
nje ya nchi wakati uchemshaji wake hauhitaji kufika hata nyuzi joto
1,000, naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya
Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha mchanga nje
ya nchi”
Akiwa njiani kuelekea Mikoa ya
Lindi na Mtwara Rais Magufuli alizungumza na wananchi wa Ikwiriri na
kupokea kero zao ambapo amewaagiza Mamlaka ya Maji katika Mji huo
kuhakikisha mradi wa maji uliojengwa na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa
gharama ya Shilingi Bilioni 5, unaanza kutoka maji kabla ya mwisho wa
Mwezi wa tatu na kupiga marufuku utozaji wa ushuru kwa wafanyabiashara
wadogowadogo wa mazao.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli
anawataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzalisha mazao ya
chakula cha kutosha katika kipindi hiki mvua zinaponyesha huku akiweka
bayana kuwa Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaopatwa na
njaa ilihali wanaweza kuzalisha chakula katika maeneo yao.
Akioneshwa kutoridhishwa na
utekeleaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi alipotembelea ujenzi
wa mradi wa maji wa Ng’apa Mjini Lindi ambao ulipaswa kuwa umekamilika
tangu tarehe 17 Machi, 2015 Rais Magufuli aliagiza kushikiliwa kwa hati
za kusafiria za mwakilishi wa kampuni ya ukandarasi ya Overseas
Infranstructure Alliance Private Limited ya India Bw. Rajendra Kumar
pamoja na wasaidizi wake mpaka hapo kampuni hiyo itakapokamilisha mradi
huo unaotarajiwa kuzalisha zaidi ya lita za ujazo milioni 5 za maji kwa
siku kwa ajili ya wakazi wa Mji wa Lindi ambao wanakabiliwa na tatizo
kubwa la maji.
Katika kuthibitisha amedhamiria
kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda Rais Dkt. Magufuli aliitaka
Wizara ya Nishati na Madini Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha
inafikisha gesi katika kiwanda hicho haraka iwezekanavyo lengo likiwa
kuondoa vikwazo vya uhaba wa makaa ya mawe na ukosefu wa gesi ambavyo
vimekuwa vikisababisha uzalishaji wa saruji kusimama mara kwa mara.
Aidha, Dkt. Magufuli aliitaka
Wizara hiyo kuhakikisha wanamega eneo lenye makaa ya mawe katika eneo la
Ngaka lililopo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma na kuipatia kampuni ya
Dangote ili iweze kuzalisha yenyewe makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda
chake cha saruji kilichopo Mkoani Mtwara.
Kiwanda hicho kinachomilikiwa na
Alhaji Aliko Dangote tangu kianze kuuza saruji bei ya bidhaa hiyo sokoni
imeshuka kutoka Shilingi 15,000/- kwa mfuko mmoja wa kilo 50 hadi
kufikia Shilingi 10,000/- na ununuzi wa magari 580 yatasaidia
kusafirisha saruji nchi nzima kwa gharama nafuu ambayo watanzania wengi
wataimudu.
Wakati akikamilisha Ziara yake
Mhe. Dkt. Rais Magufuli alifanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa
Mashujaa Mjini Mtwara ambapo alisema Serikali ya Awamu ya Tano
imejipanga kuhakikisha inasukuma maendeleo ya Nchi kwa nguvu kubwa kwa
manufaa ya wananchi.
Rais Magufuli alisema kuwa
Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutilia mkazo juhudi za
uendelezaji wa bandari ya Mtwara, ujenzi wa barabara, uimarishaji wa
miundombinu ya nishati ya umeme, ujenzi wa viwanda vikubwa na usimamizi
mzuri wa shughuli za kilimo ambavyo vitasaidia kukuza uchumi, kuzalisha
ajira na kuboresha maisha ya watu.
Aidha, Rais Dkt. Magufuli
alioneshwa kusikitishwa na Mkoa wa Mtwara kufanya vibaya kielimu na
kuwataka kuweka msisitizo katika elimu kwani juhudi za Serikali
kuwapelekea maendeleo hazitakuwa na maana kama wananchi watakuwa hawana
elimu.
Ziara hiyo ya Rais Dkt. Magufuli
imeonesha mwelekeo wa Tanzania tunayoitaka hasa katika maeneo ya
usimamizi wa miradi na utekelezaji wake kwa maslahi ya umma.
No comments
Post a Comment