Writen by
sadataley
2:39 PM
-
0
Comments
KLABU ya Yanga imesema kwamba pamoja na hali ngumu ya kifedha
inayowakabili kwa sasa, lakini itahakikisha haikwami kwa namna yoyote.
Hayo yamesemwa na Charles Boniface Mkwasa, Katibu wa Yanga katika
mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online asubuhi ya leo.
Mkwasa amesema kwamba hali ngumu ya kifedha inasababishwa na matatizo ya
Mwenyekiti wao, Yussuf Manji kwa sasa dhidi ya Serikali.
Inadaiwa Akaunti zote za Manji na kampuni zake, ikiwemo kampuni mama,
Quality Group Limited zimefungwa kiasi cha kusababisha hadi
mfanyabiashara huyo mwenye asili ya Kiasia kuanza kuzifunga baadhi ya
kampuni zake na kusimamisha baadhi ya miradi.
Manji pamoja na kuwa Mwenyekiti, lakini ndiye mfadhili mkuu wa Yanga
tangu mwaka 2006 na Mkwasa amesema klabu imeathirika kwa kiasi kikubwa
kutokana na matatizo hayo.
“Masuala mengine yote yanaendelea, hatuwezi kusema tuna kiasi gani au
tunafanya vipi, lakini kama uongozi tunajaribu kufanya utaratibu wa timu
iendelee na shughuli zake za kila siku,”amesema na kuongeza.
“Timu inakwenda, inakaa kambini na hatujaacha deni, kwa hiyo
tunachokipata tunakitumia kwenye timu hicho hicho, vitu vikubwa ndivyo
hatujaweza kufanikisha, lakini kwa masuala madogo kama ya kambi, na
mambo mengine madogo madogo tunaweza kuyamudu,”.
Kuhusu mechi ya Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya
Zanaco ya Zambia, Mkwasa amesema timu itashiriki mchezo huo bila
wasiwasi.
“Tutacheza mechi ya nyumbani na tutasafiri kwa mechi ya ugenini hakuna
shaka, Yanga ina viongozi wanaounda Kamati ya Utendaji, watakutana na
kujadili na kujipanga,”alisema.
Aidha, Mkwasa amesema kwamba hakuna mchezaji anayeidai klabu, isipokuwa
beki Vincent Bossou ambaye wakati mshahahara wake wa Januari unatoka
alikuwa Gambia na timu yake ya taifa, Togo kwenye Fainali za Kombe la
Mataifa ya Afrika.
“Tatizo mtu ambaye alikuwa ana cheki ya mshahara wa Januari wa Bossou
(kutoka Quality Group) alitaka amkabidhi mchezaji mwenyewe cheki yake.
Sasa Bossou amerejea anatakiwa kufuatilia mshahara wake Quality,”amesema
Mkwasa.
Kuhusu taarifa za kwamba mchezaji huyo amegoma, Mkwasa amesema kwamba anasubiri taarifa ya benchi la Ufundi.
Pamoja na hayo, Mkwasa ameomba radhi kwa wanachama, wapenzi na mashabiki
wa Yanga baada ya kufungwa mabao 2-1 na watani wa jadi, Simba SC juzi
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara.
“Klabu inawaomba kuwa watulivu na pia inashukuru sana kwa utulivu
waliouonyesha na kutii sheria zote kwenye mchezo wa Jumamosi, matokeo
haya tuliyoyapata ni ya kimchezo kikubwa ni kupambana na michezo
iliobakia mbele yetu na kuendelea kuwapa sapoti vijana wetu, kwani bado
tuna mashindano mengi ma michezo mingi mbeleni,”amesema Mkwasa.
Mkwasa amesema anaamini kocha Mkuu, George Lwandamina ameona mapungufu
kwenye mchezo huo na atayafanyia kazi kuelekea michezo ijayo na timu
itafanya vizuri na kurejesha furaha ya wapenzi wake.
Chanzo: Muungwana Blog
No comments
Post a Comment