Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, February 28, 2017

Mateso dhidi ya dini yashamiri katika China isiyoamini uwepo wa Mungu

KUTOKA kwenye altare katika eneo ambalo lipo umbali wa saa nne kutoka Beijing, Paul Dong anaongoza ibada ya misa takatifu.

Lakini pia kwa kufanya hivyo anavunja sheria. Dong pamoja na waumini wake ni miongoni mwa mamilioni ya Wakristo wanaosali katika China ambayo haiamini uwepo wa Mungu.
Kulingana na taarifa mpya kutoka kwa taasisi isiyo ya kiserikali kutoka nchini Marekani inayofahamika kama Freedom House, mateso dhidi ya Wakristo nchini China na imani nyingine yamezidi kushamiri katika miaka ya hivi karibuni.
“Ukichanganya matumizi ya nguvu na njia nyinginezo, sera za Chama cha Kikomunisti zimeundwa ili kusitisha ukuaji wa haraka wa jamii za kidini na kutokomeza kabisa imani fulani,” ripoti hiyo imesema.
Kutolewa kwa ripoti hiyo kumefuatia tetesi kuwa Vatican na Beijing wanaweza kufikia makubaliano ya kihistoria juu ya kuwapandisha vyeo mapadri nchini China kuwa maaskofu, na kumaliza miongo kadhaa ya uhusiano mbaya baina ya pande hizo mbili.
Makubaliano hayo hayatapokewa vizuri na Dong na waumini wake ambao huabudu kinyume na sharia.
“Yesu alisema siku moja kuwa huwezi kutumikia mabwana wawili, sasa Vatican ipo tayari kumtumikia Mungu na Chama cha Kikomunisti,” alisema
Mateso
Tangu Rais Xi Jinping aingie madarakani mwisho wa mwaka 2012, Freedom House imesema, kiasi cha ukandamizi dhidi ya dini kimeongezeka katika nyanja zote za kijamii, pamoja na kuwepo kwa mapingamizi kutoka kwa waumini wa dini zote.
“Kiasi cha udhibiti dhidi ya dini, na mateso vimeongezeka sana kama ilivyo kwa upinzani kutoka kwa waumini, vitu ambavyo vinaiathiri jamii ya China na siasa,” mtafiti Sarah Cook alisema katika taarifa yake kwenye vyombo vya habari.
Dini nchini China hudhibitiwa vikali na serikali, huku kukiwa na dini tano zinazojulikana nchini humo, Budha, Wakristo wa Kikatoliki, Wakristo wa Kiprotestanti, Waislamu na Tao – ambazo husimamiwa na taasisi rasmi kama Protestant Patriotic Movement au Buddhist Association of China.
Maeneo ya ibada huandikishwa, viongozi wa kidini hufuatiliwa, mafundisho ya kidini pia hukaguliwa, sherehe za kidini na matukio kama ya Hija kwa Waislamu hufanywa na taasisi za kiserikali,” Freedom House ilisema.
Waislamu nchini China wamekabiliwa na udhibiti wa namna ya kutekeleza ibada zao katika miaka ya hivi karibuni.
Ripoti hiyo ilieleza namna ambavyo waumini wa Kiislamu – ambao wamekuwa wakizuiwa kufunga wakati wa mwezi wa Ramadan au kuvaa nguo za kuwafunika kama hijab. Kwa waumini wa Budha huko Tibet, China humtazama kiongozi wao Dalai Lama kama alama ya utengano, na kutumia mafundisho yake kumesababisha wengi kuishia jela, kulingana na kundi la kutetea haki za binadamu huko Tibet.
Falun Gong – vuguvugu la kiroho ambalo limepigwa marufuku na Beijing limekabiliwa na usumbufu mkubwa kutoka serikalini kwa miongo kadhaa sasa. Freedom House ilisema kwamba idadi ya wafungwa kutokana na Imani nchini china inafikia makumi ya maelfu, wengi wao wakiwa ni wale wenye imani ya Falun Gong.
Mateso dhidi ya Wakristo
Inakadiriwa kuwa wapo Wakristo kati ya milioni 72 hadi 92 nchini China, kundi la pili kwa ukubwa nyuma Budha.
Wengi kati ya hao ni wale ambao hawatambuliki rasmi na serikali. Zaidi ya nusu ya Wakristo wa Kiprotestanti hawajaandikishwa, kulingana na Freedom House.
Kulingana na taasisi ya kidini kutoka nchini Marekani inayofahamika kama ChinaAid, jambo hili linawafanya kuwa rahisi kushambuliwa na kuonewa na serikali. Katika jimbo la Zhejiang pekee, zaidi ya makanisa 20 yamebomolewa, huku zaidi ya misalaba 1,000 imeondolewa katika makanisa mengine katika miaka ya hivi karibuni.
Mamia ya Wakristo wanashikiliwa gerezani wakati wakijaribu kupinga ubomoaji huo, ChinaAid ilisema.
Likiwa ndiyo kundi kubwa zaidi la waumini wa Kikristo nchini China, Freedom House ilisema Waprotestanti wamekuwa ni “waathirika wakubwa ya kampeni hiyo ya kuondoa misalaba na kubomoa makanisa, adhabu ambazo huhalalishwa na viongozi wa jimbo, na kuwakamata wanasheria wa kutetea haki za binadamu ambao hujitolea kuwatetea Wakristo.
Hata hivyo, Ian Johnson, mwandishi wa kitabu kipya “The Souls of China: The Return of Religion After Mao," alisema kuondoa misalaba hakusaidii chochote.
“Naweza kusema kwamba kitu muhimu zaidi ni kwamba hakuna hata moja ya makanisa haya ambalo limefungwa,” alisema.
“Wote wanaendelea kusali na ibada kama ilivyokuwa mwanzo. Pia, kampeni hiyo haijasambaa nje ya mipaka ya jimbo moja. Baadhi ya watu wanaona kampeni hiyo kama chanzo cha kampeni kubwa zaidi ambayo itasambaa nchi nzima, lakini hadi sasa hilo halijatokea na hukuna dalili kwamba hilo litatokea.”
Kuna mamilioni ya Wakatoliki nchini China, lakini kiasi cha nusu yao hufanya ibada katika makanisa yanayoendeshwa na serikali.
Kuboreka kwa mahusiano
Wakati hali ikiwa mbaya kwa Waprotestanti, uhusiano baina ya Vatican na Beijing umeanza kuimarika katika miaka ya hivi karibuni.
Papa Francis ameeleza nia yake ya kuitembelea China, na taarifa mwaka jana zinaonyesha kuwa pande hizo mbili zilikuwa zinakaribia kufikia makubaliano juu ya suala la maaskofu, kitu ambacho kimekuwa kinakwamisha makubaliano kwa muda mrefu.
Beijing haitambui madaraka ya Papa, na hutaka maaskofu nchini humo kuteuliwa na vyombo vya kanisa hilo ambavyo vipo chini ya serikali. Vatican hukataa kuthibitisha maaskofu ambao hupewa vyeo hivyo bila ruhusa ya papa na imewatenga maaskofu wa China.
Kadinali Joseph Zen, askofu wa zamani wa Hong Kong, amekosoa makubaliano baina ya Vatican na Beijing.
Lakini baadhi ya Wakatoliki katika eneo hilo wamekuwa wakipinga makubaliano hayo. Kadinali mstaafu Joseph Zen, Askofu wa zamani wa Hong Kong, aliliambia shirika la utangazaji la CNN kwamba makubaliano ya aina hiyo yanawahatarisha wakatoliki ambao hawatambuliki kisheria nchini China na pia yanakwenda kinyume na madaraka ya Papa.
Zen alisema kwamba hali ya Wakatoliki nchini China imekuwa mbaya zaidi katika miaka ya hivi karibuni.
“Wasiwasi wetu ni kwamba yatakuwa makubaliano mabaya,” alisema. “Hakuna sababu kutumaini kuwa Wakomunisti watabadilika. Tayari wanaudhibiti mkubwa dhidi ya kanisa, matumaini yao ni kuona makanisa yote yanakuwa chini yao.”
Wakristo na waumini wa dini nyingine, wamekuwa wakikandamizwa ndani ya China.
Sera zilizokosa mwelekeo
Wakati nyaraka za Freedom House zikieleza kuzidi kushamiri kwa mateso dhidi ya waumini wa dini, Cook alisema kuwa kuendelea kushindwa kwa Beijing katika udhibiti wa dini kunaonyesha kushindwa kwa sera zake.
“Itaonekana kwamba katika mapambano ya muda mrefu, chama kisichotaka mabadiliko cha Kikomunisti kitashindwa mwishowe,” alisema.
Mamilioni ya Wachina – hasa wakristo – hufuata dini zao nje ya udhibiti wa Chama, wakiabudu kwa siri au katika makanisa ya nyumbani kama afanyavyo Paul Dong.
Dong hutoa mahubiri kwa mamia ya Wakatoliki, baadhi yao wakiwa wanadharau taasisi ambazo zimewekwa ili kuyasimamia makanisa nchini humo.
“Siwezi kujiunga na makanisa ya kizalendo,” alisema muumini mmoja mzee. “Sio makanisa ya kweli.”

Mwandishi James Griffiths aliripoti kutoka Hong Kong. Matt Rivers aliripoti kutoka Beijing. Waandishi wa CNN Yuli Yang na Delia Gallagher walichangia katika ripoti hii.
Chanzo: Gazeti la Raia Mwema Mtandaoni
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment