Writen by
sadataley
5:27 PM
-
0
Comments
Mbunge wa Longido, Lekule Laizer akizungumza katika semina ya wabunge
kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kushugulikia masuala ya wananchi.Semina
hiyo iliandaliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)
mjini Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dodoma/Dar. Shinikizo la kutaka kusitishwa kwa Bunge Maalumu la
Katiba limezidi kuongezeka baada ya Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata),
kusema mchakato huo usitishwe hadi Januari 2016 ili kupisha Uchaguzi
Mkuu wa mwakani.
Pendekezo la Jukata linafanana na msimamo wa
baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo na wananchi wengine wa kada mbalimbali
sababu ikiwa kukosekana kwa maridhiano baina ya pande mbili zinazovutana
katika Bunge Maalumu, hali ambayo Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus
Kibamba amesema imesababisha mgawanyiko mkubwa katika nchi.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba,
Yahya Khamisi Hamad ameweka wazi kuwa Bunge hilo halitasitishwa kama
wanavyoshinikiza Watanzania wengi kwa sababu uamuzi huo hautabadili
msimamo wa CCM wala wapinzani katika suala la idadi ya serikali
wanazotaka.
“Hatuwezi kubadili misimamo iliyopo hata kama
tutasitisha Bunge. Tusitishe Bunge halafu tufanye kitu gani? Kama ni
suala la kuzungumza na kuelewana kwa nini tusifanye sasa! Tujadiliane
sasa kwa sababu msimamo wa CCM au watu wengine kuhusu wanachokiamini,
kuubadili haitawezekana,” alisema Hamad.
Mgawanyiko
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma,
jana Kibamba alisema mgawanyiko huo ulianza pale yalipoibuka makundi kwa
misingi ya kiitikadi za vyama na kundi la wajumbe wanaotokana na vyama
vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliposusia
Bunge hilo.
“Kitendo cha Ukawa kushindwa kurejea bungeni ni
pigo na kinaunyima mchakato huo uhalali wa kisiasa na kisheria kwani kwa
upande wa Zanzibar tumegundua kuwa wanapungua wajumbe 16 ili kuwezesha
kupitisha Rasimu ya Katiba,” alisema Kibamba.
Alisema nje ya sheria na kanuni, Jukata haioni
ulazima wa kuendelea na Bunge hilo ilhali ikifahamika wazi kwamba Rasimu
ya Katiba haitapata uungwaji mkono na wajumbe kutoka Zanzibar na kwamba
kuendelea na mchakato huo ni matumizi mabaya ya fedha.
“Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta alisema
eti anaamini kwamba Bunge likikaribia mwisho watakuwa wamepata idadi ya
kutosha, sasa kama muda wote hawakuwahi kufanikiwa kuwashawishi, ni
kitu gani kitawawezesha kupata akidi katika muda huo?” alihoji Kibamba.
Badala yake Kibamba alisema muda uliopo unapaswa
kutumika kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, uchaguzi wa
serikali za mitaa, uandikishaji wa wapiga kura katika mfumo mpya wa
kielektroniki na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.
“Katiba Mpya ya kidemokrasia na ya viwango vya
kimataifa alivyoviweka Rais Kakaya Kikwete, haiwezi kukamilika na
kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015,” alisema Kibamba na kusisitiza
kuwa hakuna njia nyingine ya kunusuru mchakato wa Katiba zaidi ya
kuusitisha:
“Kwa hali ilivyo sasa huwezi kusema CCM ni wamoja,
kuna watu wana mitazamo tofauti, wengine wanataka Bunge lisitishwe na
wengine wanasema liendelee, lakini hata katika Kundi la Ukawa siyo
wamoja maana wangekuwa wamoja tusingesikia kwamba wengine wapo hapa
Dodoma.”
Wabunge CCM vipande viwili
Katika hatua nyingine, wabunge wa CCM katika Bunge
la Muungano jana walivutana kuhusu hoja ya kusimamishwa kwa mchakato wa
Katiba Mpya kutokana na wajumbe wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia
vikao.
Mvutano huo ulijitokeza katika semina ya wabunge
wa kamati za Bunge hilo kuhusu Dhana ya Kusikiliza Maoni ya Wadau
iliyoandaliwa na Bunge la Muungano kupitia mradi wake wa kuwawezesha
wabunge (LSP), unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP).
Mvutano huo ulianza wakati Mbunge wa Longido,
Michael Lekule Laizer aliposema mchakato wa Katiba Mpya umekuwa ni jambo
gumu na unaelekea kushindikana na hivyo kupendekeza usimamishwe hadi
hapo kutakapokuwa na mwafaka.
Alisema mchakato huo umekuwa ni vurugu na umekosa
utashi mpaka wananchi wanashindwa kuelewa nini kinachoendelea: “Ni vyema
kuusimamisha ili jambo hilo lianze pakiwapo mwafaka.”
Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Pudenciana
Kikwembe alisema siyo kweli kwamba wajumbe wa Bunge hilo waliobakia
bungeni wameshindwa kujadili na kukamilisha mchakato... “Sisi tunajadili
na tutaendelea kujadili hadi tutafika mwisho hata kama Ukawa hawapo
ndani (ya Bunge).”
Hali hiyo ilimfanya Mwenyekiti wa semina hiyo,
William Ngeleja kuingilia kati na kuwataka wabunge wenye maoni kuhusu
mjadala huo wayapeleke kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel
Sitta.
“Semina hii haihusiani na Bunge la Katiba, hapa
tulipo wote ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, kama kuna mtu
ambaye ana maoni kuhusu Bunge Maalumu apeleke maoni yake kwa utaratibu
wa kawaida,” alisema Ngeleja.
Hata hivyo, kauli ya Ngeleja haikufua dafu kwani
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy alisimama na kuhoji: “Zimeundwa
tume nyingi, Tume ya Shelukindo (William), Tume ya Jaji Nyalali
(Francis) na Tume ya Jaji Warioba (Joseph), zimekwenda kuchukua maoni ya
wadau maoni hayo yako wapi? Yameenda wapi?”
Alisema tume hizo zimepoteza fedha nyingi za
Watanzania lakini maoni ya wadau hayajulikani yamepelekwa wapi. Mbunge
wa Kwela, Iginas Malocha alisema kuna tatizo la maoni ya wananchi
kuingiliwa na wanasiasa na kutopelekwa panapostahili... “Hii
inasababishwa na kukosekana kwa uzalendo, uadilifu na ukweli.”
Imeandikwa na Neville Meena, Sharon Sauwa (Dodoma) na Fidelis Butahe (Dar).
No comments
Post a Comment