Writen by
sadataley
6:40 PM
-
0
Comments
Na James Magai, MwananchiDar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imefungua milango kwa mawaziri na wabunge kufunguliwa mashtaka kutokana na kauli watakazozitoa bungeni ambazo ni kinyume cha Katiba na Sheria.
Mahakama Kuu ilitoa msimamo huo jana wakati ikitoa
uamuzi wa pingamizi la awali katika kesi ya kikatiba iliyokuwa
ikimkabili Waziri Mkuu Mizengo Pinda, lililowasilishwa na Jopo la
Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(DAG, George Masaju.
Kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013 ilifunguliwa na
Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana
na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), dhidi ya Pinda na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), aliyeunganishwa kama mlalamikiwa wa pili.
LHRC na TLS walikuwa wakidai kuwa Pinda alivunja
Katiba kutokana na kauli aliyoitoa bungeni, wakidai kuwa ni amri kwa
vyombo vya utekelezaji wa sheria kuwapiga wananchi wakati wa vurugu.
Hivyo, walikuwa wakiiomba mahakama, pamoja na
mambo mengine, itamke kuwa kauli hiyo ni kinyume cha Katiba na imwamuru
Pinda aifute hadharani.
Hata hivyo, Pinda na AG waliokuwa wakitetewa na
DAG Masaju akisaidiana na Mawakili wa Serikali Wakuu (PSA, Gabriel
Malata, Alecia Mbuya na Sarah Mwipopo), waliweka pingamizi la awali
dhidi ya kesi hiyo, wakitoa hoja tano za kuomba kesi hiyo itupiliwe
mbali.
Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na kwamba kesi
hiyo ni batili na iko mahakamani isivyo halali kwa kuwa inakiuka Katiba
ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 na Sheria ya Mamlaka, Kinga na Haki
za Wabunge, ya mwaka 1988.
Mawakili hao walidai kuwa Pinda analindwa na
Katiba Ibara ya 100 (1) na (2), ambazo zinamkinga mbunge kushtakiwa au
kufunguliwa shauri la madai mahakamani kwa jambo lolote alilolisema, au
alilolitenda, au alililoliwasilisha bungeni kwa njia ya maombi, muswada
au hoja.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake jana ilikubaliana
na baadhi ya hoja za mawakili wa utetezi (Serikali) na kuitupilia mbali
kesi hiyo, lakini ikatamka kuwa wabunge na mawaziri wanaweza kushtakiwa
kwa kauli au jambo walilolitamka bungeni, linalokiuka sheria na haki za
binadamu.
Uamuzi huo ulisomwa na Kiongozi wa Jopo la Majaji
wa Mahakama Kuu, lililokuwa likisikiliza kesi hiyo, Jaji Kiongozi Fakih
Jundu kwa niaba ya majaji wenzake, Agustine Mwarija na Dk Fauz Twaib.
Katika uamuzi huo, majaji walikubaliana na hoja
tatu za pingamizi kuwa walalamikaji katika kesi hiyo hawakuwa na haki ya
kufungua kesi hiyo na kwamba walikosea taratibu za ufunguaji wa kesi
kama hizo kwa kuwa walikiuka amri na kanuni zinazoongoza Mashauri ya
Madai (CPC).
Katika hoja ya kwanza kuwa Pinda kama mbunge
analindwa na Katiba, jopo hilo lilisema kuwa ni kweli wabunge wanalindwa
na Katiba Ibara ya 100 (1) kuhusu haki na upendeleo (Previledge), yaani
haki na uhuru wa mjadala na maoni. Hata hivyo, lilikataa hoja za
utetezi kuwa wabunge wana kinga isiyo na mipaka ya kutokushtakiwa kwa
kauli au jambo lolote walilolitamka bungeni.
Kwa habari zaidi ingia hapahttp://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Mahakama-yaondoa-kinga-ya-wabunge/-/1597296/2339912/-/f35r0m/-/index.html
Kwa habari zaidi ingia hapahttp://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Mahakama-yaondoa-kinga-ya-wabunge/-/1597296/2339912/-/f35r0m/-/index.html
No comments
Post a Comment