Writen by
sadataley
1:43 PM
-
0
Comments
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dodoma/Dar. Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwasili Dodoma keshokutwa, ikiwa ni siku moja kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Habari zilizopatikana jana zinasema Rais ataongoza
kikao cha Baraza la Mawaziri kitakachopewa muhtasari kuhusu Bajeti ya
Serikali ya mwaka ujao wa fedha na baadaye atafuatilia uwasilishaji wa
bajeti hiyo bungeni akiwa Dodoma.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu
alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yuko likizo lakini
akaweka bayana kwamba kwa kawaida kabla ya bajeti kuwasilishwa bungeni,
lazima Baraza la Mawaziri lipewe muhtasari wa bajeti husika.
“Ni kawaida kabla ya bajeti kuwasilishwa, Rais
huongoza kikao cha Baraza la Mawaziri yaani pre budget cabinet meeting
ambako Waziri wa Fedha hutoa briefing (muhtasari) kuhusu maeneo muhimu
ya bajeti, kwa hiyo siyo jambo jipya ni suala la kawaida,” alisema
Rweyemamu.
Itakumbukwa kuwa mwaka jana kabla ya kusomwa kwa
bajeti ya 2013/14, Rais Kikwete alikuwa Dodoma ambako pamoja na kukutana
na mawaziri, pia alifanya kikao na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Hata hivyo, uwepo wake mjini Dodoma safari hii
umekuja wakati kukiwa na dalili za mvutano mkubwa kati ya Bunge na
Serikali kutokana na kutotolewa kwa fedha za kutosha za maendeleo kwa
mwaka wa fedha unaoisha Juni 30 mwaka huu.
Taarifa zinasema bajeti inayomalizika mwishoni mwa
mwaka huu, inapungukiwa kiasi cha Sh1.8 trilioni, huku Serikali
ikilaumiwa na wabunge kwa kutoa misamaha ya kodi inayofikia Sh1.52
trilioni, ambayo ingepunguza nakisi iliyopo kwenye bajeti kwa asilimia
84.4.
Wakati wa mjadala wa bajeti za wizara tangu kuanza
kwa Bunge la Bajeti Mei 6 mwaka huu, wabunge wamesikika mara kadhaa
wakilalamika kwamba fedha za maendeleo zilizotolewa kwa wizara katika
bajeti ya 2013/14 ni kati ya asilimia 25 na 30, jambo ambalo
limesababisha kukwama kwa miradi mingi.
Keshokutwa itakuwa siku ya mwisho ya mashauriano
baina ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Bunge kupitia Kamati yake
ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Mazungumzo hayo yaliyoanza Juni 5 mwaka huu,
yalilenga kuangalia uwezekano wa kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili
kuwezesha kuzingatiwa kwa ushauri wa wabunge, pamoja na kusaka fedha
kuziba pengo la Sh1.8 trilioni katika bajeti ya 2013/14.
Alipoulizwa jana, Chenge hakuwa tayari kuzungumzia
hatua iliyofikiwa katika mashauriano hayo na badala yake alisema kwa
ufupi: “Ndugu yangu mambo ya Bunge, tutakutana kwenye taarifa yetu ya
kamati tutakayoiwasilisha bungeni.”
Kamati ya Bajeti katika maoni yake iliyoyatoa Juni
17 mwaka jana kuhusu Bajeti ya Serikali ya 2013/14, iliweka bayana
kuwapo kwa udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato, baadhi ya wizara
kutumia fedha nyingi kuliko ilivyoidhinishwa na Bunge na Serikali kuwa
na matumizi makubwa kuliko mapato yake.
No comments
Post a Comment