Writen by
sadataley
1:44 PM
-
0
Comments
Na Joseph Zablon na Harieth Makwetta, Mwananchi
Dar es Salaam. Nguli wa michezo ya kuigiza na
vichekesho, Saidi Wangamba ‘Mzee Small’ (59), amefariki dunia juzi
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam akiwa ni msanii
wanne kukutwa na mauti katika mwezi mmoja.
Kifo cha msanii huyo ambaye anatarajiwa kuzikwa
katika Makaburi ya Segerea, Dar es Salaam leo kimetokana na ugonjwa wa
kiharusi uliompata, mwaka 2012 alipoanguka bafuni na baadaye kupooza
upande wa kushoto.
Mtoto wa marehemu, Muhidin Saidi alisema jana
kwamba muda mfupi kabla ya kukutwa na mauti, baba yake alikuwa anakoroma
huku akitapika damu mfululizo na ilipofika saa nne usiku alikata
roho... “Sijawahi kumuona baba akiwa katika maumivu kama ilivyokuwa
usiku kabla ya kifo.”
Hata hivyo, anasema wanafarijika kwani wiki moja
kabla kifo chake, aliwaachia wasia akiwataka wanaosoma kushika elimu pia
akisisitiza upendo miongoni mwao na matunzo kwa mke wake.
“Wanangu najua kuwa ninakufa, hilo halina mjadala
na ninaomba mnizike jirani na ninapoishi ili marafiki zangu wasipate
tabu kufika kwenye kaburi langu,” alisema Muhidini akimnukuu baba yake.
Alisema Mzee Small alikataa wazo la kuzikwa kwao Kilwa, Lindi au Kiparang’anda, Pwani ambako kuna shamba lake.
Saidi alisema baba yao aliwasisitizia wanaye ambao
bado wanasoma waishike elimu kwa kuwa ndiyo ukombozi wao ingawa yeye
hakupata elimu ya kutosha na kusisitiza mshikamano baina yao. Mzee Small
ni msanii wa nne kufariki ndani ya mwezi mmoja, akiwa ametanguliwa na
Rachel Haule, Adam Kuambiana na George Otieno ‘Tyson’.
Sababu za kifo
Msanii huyo alifariki dunia baada ya hali yake kubadilika ghafla juzi nyumbani kwake Tabata Kisiwani na kupelekwa hospitali.
Said alisema baba yake alilalamika kujisikia
vibaya na kukohoa na kutapika damu na ndipo walipompeleka Muhimbili
ambako alifanyiwa vipimo mbalimbali kikiwamo cha CT-Scan.
“Alikutwa na uvimbe katika maeneo matatu tofauti
kichwani na ulionekana kama kuvia kwa damu katika ubongo na wakati
akiendelea na matibabu saa mbili alikata kauli na alikuwa akiendelea
kutapika damu,” alisema.
Alisema ingawa baba yao alikuwa amepooza upande wa
kushoto kutokana na kiharusi, alikuwa anaendelea vizuri kabla ya
kuzidiwa juzi.
No comments
Post a Comment