Writen by
sadataley
4:31 PM
-
0
Comments
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Hatua ya kurejeshwa kazini
Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa baada ya
kutimuliwa kazi na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
imeibua mapya baada ya mkurugenzi huyo kutimuliwa katika Kamati ya Bunge
jana.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira walikubaliana na pendekezo la Nyalandu kutaka Profesa Songorwa
asijitambulishe katika kikao cha kamati hiyo kwa kuwa hakuwa
anatambulika.
Sakata hilo lilitokea wakati kigogo huyo na
watendaji wengine walipokuwa wakijitambulisha kabla ya kuanza kwa kikao
cha kamati hiyo kilichokuwa kikijadili Bajeti ya Serikali mwaka 2014/15.
Februari mwaka huu, Profesa Songorwa na Mkurugenzi
Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Jafari Kidegesho
walisimamishwa kazi na Nyalandu akisema ni utekelezaji wa azimio la
Bunge katika Ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili.
Hata hivyo, watendaji hao, walirejeshwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza
kwamba baada ya Nyalandu kukataa kumtambua, wajumbe walimuunga mkono
wakisema nao hawamtambui kwa sababu hatua aliyochukuliwa ilitokana na
uamuzi uliofikiwa na Kamati ya Operesheni Tokomeza, ambayo ni sehemu ya
Kamati hiyo ya Bunge.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Nyalandu alikiri
kumzuia Songorwa kujitambulisha: “Kwanza sikujua kama angekuwapo katika
kikao kile, maana suala lake bado hatujalizungumza ofisini. Sikuona
sababu ya yeye kujitambulisha. Tukirejea ofisini tutalizungumza na kazi
zitaendelea kama kawaida, ila azimio la Bunge dhidi yake lipo wazi.
Uamuzi haurudi nyuma na itabidi apangiwe kazi nyingine.”
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli
alishindwa kukiri wala kukataa kutokea kwa jambo hilo zaidi ya kusema
jambo hilo iulizwe Wizara ya Maliasili na Utalii.
Profesa Songorwa hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo na simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila majibu.
No comments
Post a Comment