Writen by
sadataley
4:11 PM
-
0
Comments
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Zanzibar. Rais Mstaafu wa Zanzibar awamu ya
sita, Dk Amani Abeid Karume amekutana na viongozi wa Kamati ya
Maridhiano Zanzibar na kujadiliana hali ya kisiasa iliyojitokeza katika
mjadala wa Katiba Mpya, pamoja na kujitoa kwa wabunge wa Ukawa kwenye
vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa viongozi
hao wamekutana faragha Aprili 30, nyumbani kwa Rais huyo mstaafu eneo
la Mbweni mjini Unguja.
Viongozi wengine walioshiriki mazungumzo hayo ni
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Mkurugenzi
wa Uenezi, Habari na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Abdallah Bimani,
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Hassan Nassor Moyo na
Katibu Mtendaji wa Kamati hiyo, Mansoor Yussuf Himid.
Wajumbe wengine katika msafara huo walikuwa ni
Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu na Eddy Riyami huku mjumbe
mmoja wa kamati hiyo, Aboubakary Khamis Bakary ambaye ni Waziri wa
Katiba na Sheria wa (SMZ) akikosekana.
Imeelezwa kuwa kamati hiyo ilitoa muhtasari wa
mwelekeo wa mjadala wa Katiba Mpya na sababu za wajumbe wa Ukawa
kutoshiriki vikao vya Bunge la Katiba.
Kamati hiyo ilitaja ni Bunge hilo kutawaliwa na
ushabiki, vijembe, matusi na kebehi, huku ikielezwa pia kuwapo na
dhamira ya kupuuzwa maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba kupitia Rasimu
ya Pili ya Katiba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Mzee Moyo
aliithibitishia jana kamati yake kukutana na Rais mstaafu Karume, ingawa
alikataa kuelezea lolote lililojadiliwa wala kutaja azimio lililofikiwa
baada ya kikao hicho kumalizika.
“Ni kweli kamati yangu ilikutana Rais Mstaafu
Karume nyumbani kwake, wala si kificho, tumekubaliana Jussa atakuwa
ndiye mzungumzaji wa yale tuliyoyazungumza na kuafikiwa, yeye na
Mansoor ndiyo makatibu watendaji wa kamati yetu,”alisema Mzee Moyo.
Gazeti hili lilipompigia simu Rais Mstaafu Karume ili aeleze ajenda na madhumuni ya kikao hicho, hakuwa tayari kueleza lolote.
Hata hivyo, baada ya kumalizika mkutano huo,
baadhi ya viongozi hao akiwamo Maalim Seif , Jussa na Mzee Moyo
walikwenda moja kwa moja kushiriki mkutano wa hadhara wa Ukawa
uliohutubiwa na viongozi wa juu wa CUF, NRA, Chadema, DP, NCCR-Mageuzi
na NLD.
Naye Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF,
ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Ismail Jussa
akizungumza na Mwananchi Jumapili amesema kwamba walikutana na Rais
Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume kama waanzilishi wa maridhiano ya
kupatikana kwa mwafaka wa kisiasa Zanzibar na hatimaye kuunda Serikali
ya Umoja wa Kitaifa.
Alisema katika mkutano wao na Rais Mstaafu Karume,
walizungumza kuhusu jinsi ya kulinda maridhiano na Serikali ya Umoja wa
Kitaifa hasa kutokana na kuwapo baadhi ya watu wenye mwelekeo wa kutaka
kuvuruga maridhiano hayo.
“Kumeonekana kuwapo watu wenye dhamira ya kuvuruga maridhiano
yetu kwa maslahi yao ya kisiasa, hivyo tumetafakari nini tufanye ili
kulinda maridhiano,” alisema Jussa.
Kadhalika alisema walizungumzia Mchakato wa Kupata
Katiba Mpya jinsi ulivyokuwa katika Bunge Maalumu la Katiba na kuweka
mikakati ya kuhakikisha kuwa maslahi ya Zanzibar yanalindwa.
“Yaliyokuwa maoni ya Wazanzibari na yanayoendelea
hivi sasa katika Bunge Maalumu la Katiba, ni vitu viwili tofauti, hivyo
tunataka kuhakikisha kuwa maoni ya Wazanzibari yanaheshimiwa na haki zao
zinalindwa,” alieleza Jussa.
baadhi ya watu waliokuwa hawakuunga mkono
maridhiano hayo, kutaka kuvuruga, wafanye nini kulinda maridhiuano na
serikali ya umoja wa kitaifa hasa kutokana na majaribio yanayofanywa na
baadhi ya watu ambao wanaonekana kusaka madaraka hata kuvcuruga
maridhiano ili wafikie malengo yao ya kisiasa. Wametafakari nini wafanye
ili kulinda maridhiano
Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara Maalim
Seif alisema ikiwa CCM wanaendelea kung’ang’ania na kutetea mfumo wa
Muungano wa Serikali mbili ni jambo jema, lakini akasema ni vyema kila
upande wa Jamhuri ya Muungano ukapewa mamlaka yake kamili ya dola.
Alisema ikiwa CCM na Serikali zake wanashabikia
mfumo huo korofi wa Muungno wa Serikali mbili na kubeza Rasimu ya Tume
ya Jaji Warioba, wajumbe wa Ukawa hawatarudi kushiriki Bunge hilo na
kwamba yeye binafsi msimamo wake ni ule wa Ukawa na kamwe hatabadilika.
Mara kadhaa Mansoor na Jussa walipopigiwa simu zao
za mikononi zilikuwa zikiita bila ya kupokewa, hivyo viongozi hao
kushindwa kutoa ushirikiano ili kuelezea kwa undani mazungumzo kati ya
Rais na Makamu Mwenyekjiti mstaafu huyo wa CCM Zanzibar (Dk Karume).
Kumekuwa na mfululizo wa vikao vya siri tangu
wajumbe wa Ukawa walipojiondoa bungeni ikiwa ni pamoja na ujio wa
Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, kutembelea Zanzibar,
Aprili 21 mwaka huu ambapo alikutana na Rais wa visiwa hivyo, Dk Ali
Mohamed Shein, Mzee Moyo, Rais Mstaafu Dk Karume na Maalim Seif.
Wakati kukiwa na juhudi za kidiplomasia za
upatanishi ili wajumbe wa Ukawa warejee bungeni, tayari Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete amewataka wajumbe hao warudi
na kushiriki katika chombo hicho halali cha kikatiba na ikiwa
itashindikana baada ya siku 60 kumalizika, Katiba ya sasa ya mwaka 1977,
itaendelea kuliongoza Taifa.
No comments
Post a Comment