Writen by
sadataley
4:13 PM
-
0
Comments
Na Mwandishi Wetu MwananchiDar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameunda Tume ya Uchunguzi, kuhusu vitendo vilivyotokana na Uendeshaji wa Operesheni Tokomeza.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni
Sefue ilisema, Rais ameunda Tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha tatu cha
Sheria ya Uchunguzi Sura ya 32.
Kutokana na hatua yake ya kuunda Tume hiyo, Rais
Kikwete amemteua Jaji na Balozi Mstaafu Hamisi Msumi kuwa Mwenyekiti wa
Tume hiyo.
Vilevile, Rais Kikwete amewateua Jaji Mstaafu
Stephen Ihema na Jaji Mstaafu Vincent Lyimo kuwa Makamishna. Rais pia
amemteua Frederick Manyanda, Wakili wa Serikali katika Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa Katibu wa Tume hiyo.
Hatua ya Rais Kikwete kuunda tume hiyo inakuja
baada ya Operesheni Tokomeza Ujangili kusitishwa na Bunge kutokana
ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu wakati wa utekelezaji wake.
Operesheni hiyo iliayoanza Oktoba 2013 na
kusitishwa Nobemba 4 mwaka jana, ndiyo iliyowang’oa mawaziri wanne kwa
kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wake.
Mawaziri hao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis
Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David
Mathayo.
Taarifa ya Balozi Sefue inasema kuwa uteuzi huu
ulianza jana, na kutaja majukumu ya tume hiyo kuwa ni pamoja na
kuchunguza na kubaini Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa.
Majukumu mengine ni kuchunguza na kubaini iwapo
Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu za Rejea zilifuatwa na watu
waliotekeleza Operesheni Tokomeza na kuchunguza na kubaini iwapo yupo
mtu yeyote aliyekiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea wakati wa
Operesheni Tokomeza.
Kuchunguza na kubaini kama wapo watu wowote
waliokiuka Sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na
kupima kama hatua zilizochukuliwa dhidi yao au mali zao zilikuwa
stahiki.
Kupendekeza hatua zozote zinazopaswa kuchukuliwa
dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kukiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za
Rejea za Operesheni Tokomeza.
Kupendekeza mambo ya kuzingatiwa wakati wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka kasoro.
No comments
Post a Comment