Writen by
sadataley
10:27 PM
-
0
Comments
Na Geofrey Nyang’oro, Mwananchi
Iringa. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ataongoza wabunge 40 wa chama hicho kwenda kuongeza nguvu katika kampeni za lala salama za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa.
Uchaguzi mdogo wa Kalenga unatarajiwa kufanyika Jumapili ijayo, Machi 16 mwaka huu kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Dk William Mgimwa, huku mchuano mkali ukionekana kuwa kati ya Chadema na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Habari ambazo zililifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Mbowe jana zinasema, wabunge hao watatawanywa katika kata za Jimbo la Kalenga na watakuwa katika maeneo hayo hadi Jumapili.
Akizungumza kutoka mjini Dodoma, Mbowe alithibitisha kwamba ataongoza wabunge 40 wa chama chake kwenda Kalenga ili kuhakikisha chama hicho kinashinda uchaguzi huo mdogo.
Hata hivyo, Mbowe alisema safari hiyo itazingatia ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea Dodoma.
“Kama mnavyofahamu tupo hapa Dodoma ambako tuna jukumu la kitaifa, kwa hiyo hatuwezi kuondoka tukaacha jukumu hili, tunaangalia jinsi ratiba ilivyokaa ili pale tutakapopata fursa hiyo tuweze kuitumia kwenda Kalenga,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Tunafahamu kwamba baada ya kupitisha Kanuni za Bunge Maalumu, kuna kazi kubwa ya kuwaapisha wabunge, inaweza kuchukua siku mbili au tatu hivi, kwa hiyo sisi tutatumia siku hizo kwa wabunge wetu kwenda kuhakikisha ushindi unapatikana Kalenga.”
Alisema wabunge hao kabla ya kuondoka watashiriki katika uchaguzi wa viongozi wakuu wa Bunge la Katiba; Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti. Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za Bunge hilo, uchaguzi wa viongozi hao unatarajiwa kufanyika leo na kesho.
Mapema Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila alisema baada ya kuwasili, wabunge hao watapiga kambi katika jimbo hilo hadi uchaguzi utakapofanyika.
Tayari wabunge wawili wa chama hicho, Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Godbless Lema (Arusha) wapo Kalenga tangu Ijumaa iliyopita wakimnadi mgombea wa Chadema, Grace Tendega. Ofisa Habari wa Chadema, Tumain Makene alisema Mbowe anatarajiwa kuwasili leo Iringa akitokea Dodoma.
“Mwenyekiti wetu anatarajia kuwasili mjini hapa kesho (leo) akiwa na wabunge wengine 26, wanakuja kupiga kambi hadi utakapofanyika uchaguzi Jumapili,” alisema Makene.
Katika hatua nyingine, Lema aliwatoa shaka wananchi wa Kalenga kutokuwa na hofu kuhusu usalama wa kura watakazozipiga, kwa kuwa chama hicho kimeimarisha ulinzi baada ya kura kupigwa. Lema alisema Chadema kimewapeleka watu zaidi ya 1,000 ambao wametawanywa vijijini na kwamba wengine kutoka Mara, Arusha na mikoa mingine wanaendelea kuwasili kuungana na wenzao.
No comments
Post a Comment