Writen by
sadataley
3:21 PM
-
0
Comments
MAKALA: MPATANISHI KAMALIZA, ZAMU YAKO IKIFIKA UTAITWA NANI?
![]() |
| Hayati Nelson Mandela. ©xxl mag |
Miaka 95 imepita tokea kuzaliwa kwa Nelson Rolihlahla Mandela. Almaarufu Madiba, yaani mpatanishi.
Tarehe 18 Julai 1928 ndio mwaka hasa ambao Rais huyu wa kwanza mweusi kwa kipindi cha mwaka 1994 hadi 1999., kipindi ambacho kulikuwa na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini - alizaliwa.
Mandela ambaye ni mwanasheria kwa taaluma, akisoma katika vyuo vikuu vya Fort Hare, na Witwatersrand, alijiunga na siasa mwaka 1948, baada ya chama cha taifa cha Afrika Kusini kushika dola.
Kujiunga kwake na African National Congress – ANC, kulimfanya aanzishe umoja wa vijana wa chama hicho, na mnamo mwaka 1952 – alichanua kwenye siasa, baada ya kuongoza kampeni dhidi ya sheria kandamizi, ambapo kwa harakati zake akiwa mtetezi na mwanasheria, alikamatwa mara kwa mara na vyombo vya dola.
Harakati ziliendelea hadi pale kwa kushirikiana na wenzie, waliunda kikundi cha Umkhonto we Sizwe (yaani, mkuki wa taifa – spear of the nation), mnamo mwaka 1961 kwa ushirkiano na chama cha kikomunisti cha Afrika Kusini. Ambapo Umkhonto we Sizwe iliongoza kampeni dhidi ya utawala wa kidhalimu nchini humo, jambo ambalo lilipelekea Mandela kukamatwa mwaka 1962 kwa kutuhumiwa kufanya njama za kuipindua serikali, na hivyo kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Mandela alitumikia miaka 27 ya kifungo chake kwenye magereza matatu, moja kwenye visiwa vya Robben, na kasha kumalizia miaka iliyobaki kwenye gereza la Pollsmoor kwenye gereza la Victor Verster.
Kampeni ya kimataifa ulimwenguni kote pamoja na kuliwekea taifa la Afrika Kusini vikwazo ndio ilipelekea kuachiwa kwa kiongozi huyu mnamo mwaka 1990, kipindi ambacho harakati pia zilikuwa zikiendelea – huku migomo ya wafanyakazi nayo ikishamiri.
Baada ya kuachiwa, Mandela alichapa kitabu akielezea maisha yake, na kisha kuanza mjadala na rais wa kipindi hicho, Fredrik Willem de Klerk, ili kusitisha ubaguzi wa rangi na kupangwa kwa uchaguzi wa kwanza wa watu wa rangi zote, yaani weusi kwa weupe.
Ushindi wa kishindo ulipatikana kwa Mandela katika uchaguzi wa mwaka 1994, ambapo mara baada ya kuchukua madaraka, alifanya jitihada za kupatanisha makundi yaliyokuwa na hasira, ghadhabu, na nia ya malipizi kwa yale ambayo wametendewa kwa kipindi chote.
Juhudi zake zilikutanisha makundi ya watu waliotenda maovu na waliotendwa, na hatimaye kuwapa fursa walioumizwa kueleza namna ambavyo waliteseka mbele ya waliokuwa watesi wao, na kasha kusameheana pale ambapo ilifanikiwa.
Juhudi zake kwenye uongozi kwa kipindi cha mwaka 1994 hadi 1999 ndizo zikampa jina la Madiba, yaani mpatanishi. Ni jambo lililo jema, maana imeandikwa – Heri wapatanishi maana wataitwa wana wa Mungu.
Mandela aliachia madaraka mwaka 1999, na kiti kuchukuliwa na Thabo Mbeki kutoka chama cha ANC. Na kufikia Novemba mwaka 2009, Umoja wa Mataifa ulitangaza siku ya kuzaliwa kwa Mandela – 18 July, kuwa siku ya Mandela duniani, ikiwa ni mara ya kwanza kwa tukio kama hilo kufanyika.
Mandela anakumbukwa na wengi, mataifa mengi – na dunia nzima kwa ujumla, ndio maana Rais Kikwete ametangaza siku tatu za maombolezo, huku taifa la Marekani nalo likipeperusha bendera nusu mlingoti, Kona zote kuanzia Iran hata Japan na India, wote wanamlilia. Huu si msiba wa kijiji cha Mvezo, alikozaliwa kiongozi huyu mfano wa kudumu. Bali ni msiba wa dunia nzima.
Wakati dunia inasikitika na kufurahia kupumzika kwa Baba Mpatanishi, jiulize - ukiondoka utaitwa nani?

No comments
Post a Comment