Writen by
sadataley
3:17 PM
-
0
Comments
Askofu Desmond Tutu
Johannesburg. Mshindi wa Nishani ya Amani ya Nobel, Askofu Desmond Tutu amesema ana imani kwamba viongozi wanaotaka umashuhuri duniani watafuata mfano wa Nelson Mandela.
Gazeti la The Telegraph liliripoti jana kuwa Askofu Tutu alisema hayo juzi usiku wakati akiwa kwenye shughuli ya kumbukumbu ya kifo cha Mandela mjini Johannesburg.
Askofu Tutu ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 82, alikuwa mtu wa karibu na Mandela katika harakati za kupigania haki za binadamu nchini Afrika Kusini.
“Sijui lakini naamini viongozi wengi wakuu wa nchi, hakuna ambaye yuko tayari kutamka neno ‘samahani’ pale anapokosea. Yeye aliweza. (viongozi) tunapaswa kufuata nyayo zake,” alionya Askofu Tutu.
Mandela amekuwa na mifano mingi ya kipekee ambayo inapaswa kuigwa na viongozi ili kutekeleza wajibu wao wa kuwatumikia wale wanaowaongoza.
Miongoni mwa mambo hayo ni kusimamia kikamilifu haki, uvumilivu na kusamehe wale waliomkosea.
Mandela alinyanyaswa kwa kufungwa na serikali ya makabaru kwa miaka 27 ikiwa ni mkakati wa kukandamiza harakati zake za kukabiliana na siasa za ubaguzi wa rangi.
Hata baada ya kutoka kifungoni na kufanikiwa kuwa rais wa kwanza mweusi, hakuamua kulipiza kisasi kwa manyanyaso aliyotapata licha ya kuwa na uwezo huo.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete aliwasili Pretoria usiku wa kuamkia jana na kuhudhuria shughuli ya Kitaifa ya Kumbukumbu ya msiba wa Nelson Mandela kwenye Uwanja wa Michezo wa FNB, mjini Johannesburg.
Rais Kikwete alijiunga na mamia ya viongozi wa nchi mbalimbali duniani kuomboleza kifo cha shujaa huyo aliyepambana na siasa za ubaguzi wa rangi zilizokuwa zikiendeshwa na makaburu.
Rais Kikwete aliambatana na Makamu Mwenyekiti wa Pili wa Zanzibar, Balozi Seif Idd na mkewe Mama Asha; Mama Salma Kikwete na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahaman Kinana.
No comments
Post a Comment