Writen by
sadataley
3:22 PM
-
0
Comments
Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan amesema umoja wa viongozi wa dunia waliokutanishwa na Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela utaendelea kufanya kazi yake ya kuhakikisha amani na usalama vinatawala dunia.
Alisema kuwa umati wa viongozi wa dunia waliofurika nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kwa Mandela wana kila sababu ya kuhakikisha amani inatawala katika maeneo yao kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia.
Annan alisema kuwa ari ya Mandela katika kusimamia demokrasia ni kitu ambacho kinapaswa kuwa mfano kwa viongozi wote duniani.
“Kitendo cha kuachia madaraka katika muhula mmoja wa uongozi wake tangu alipoingia madarakani kuliashiria ni namna gani alikuwa mtu mwenye kusimamia demokrasia na kujali masilahi ya watu wengine” alisema Annan na kuongeza:
“Lakini tukiangalia sasa kifo cha Mandela kimetokea wakati kuna watu wanapoteza maisha katika nchi mbalimbali barani Afrika kutokana na wengine kung’ang’ania madaraka. Tuna kila sababu ya kujifunza kutoka kwa Mandela.
Annan pia ni mwanachama wa umoja wa viongozi wastaafu wa dunia na wanaharakati wa haki za binadamu ambao hushiriki katika kutoa ushauri wa masuala mbalimbali ya kimataifa.
Alisema pia kuwa Mandela alikuwa mwanachama wa umoja huo tangu mwaka 2007 ila kutokana na hali yake ya kiafya hakuwa mwanachama hai lakini mkewe Graca Machel ni mwanachama.
Dunia nzima imeendelea kuomboleza kifo cha Hayati Nelson Mandela, ambaye familia yake imeeleza kuwa kuwapo kwake kulikuwa kama mbuyu ambao unatoa kivuli chenye utulizo unaotoa ulinzi kwao.
No comments
Post a Comment