Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Friday, November 8, 2013

Wanahabari shikamana kuikataa sheria hii

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.PICHA|MAKTABA 
Bunge jana liliithibitishia dunia kwamba uhuru wa habari nchini utaendelea kuwa kitanzini, baada ya kupitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2013, ikiwamo Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976. Katika marekebisho ya sheria hiyo, adhabu ya makosa ya kuchapisha habari ambazo Serikali inaona ni za uchochezi au inadhani zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani imeongezeka kwa kiwango cha kutisha kutoka Sh150,000 hadi Sh5 milioni au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema wakati akiwasilisha muswada huo bungeni juzi kwamba mapendekezo hayo yanalenga kutekeleza azimio la Mkutano wa 11 wa Bunge ambapo, pamoja na mambo mengine Serikali ilitakiwa kupitia sheria zilizopo ili kuona kama zinatosheleza kuzuia kile Bunge ilichokiita lugha au kauli za uchochezi zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipinga marekebisho hayo, ikisema yana lengo la kukandamiza haki ya wananchi kupata habari.
Haikutazamiwa hata kidogo kwamba wakati huu Serikali ingewasilisha muswada wa kuongeza makali ya sheria hiyo kandamizi, ambapo wadau wa habari nchini wanapigania kupatikana kwa Sheria ya Kupata Habari pamoja na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari. Yafaa tukumbuke kwamba mapendekezo ya wadau wa habari kuhusu sheria hizo yalipelekwa serikalini zaidi ya miaka saba iliyopita, lakini jambo la kushangaza ni kwamba Serikali imekuwa ikipata kigugumizi kueleza sababu za kutopeleka miswada ya sheria hizo bungeni, licha ya wabunge na wadau wa habari kuitaka ifanye hivyo.
Kitendo cha Serikali kupeleka tu bungeni vifungu vinavyohusu ongezeko la adhabu kwa waandishi kimetafsiriwa na wananchi wengi kwamba Serikali haina dhamira ya kuweka mazingira ya kukuza uhuru wa vyombo vya habari hapa nchini. Pamoja na wabunge wengi wa CCM kufurahia mapendekezo ya Serikali ya kuongeza adhabu hizo, wapo baadhi ya wabunge wa chama hicho, wakiwamo wajumbe wa Kamati inayohusika na vyombo vya habari, chini ya Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, ambao wameonyesha kushangazwa na hatua ya Serikali ya kuifanyia marekebisho sheria hiyo kila mara badala ya kuwasilisha bungeni miswada ya sheria hizo mbili tulizozitaja hapo juu.
Ndiyo maana baadhi yao hawakuunga mkono mabadiliko ya sheria hiyo na kusema Serikali ina ajenda ya siri ya kuua vyombo vya habari. Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeweka wazi uduni na maudhui hasi ya marekebisho hayo, ambayo kwa tafsiri yoyote ile hayana uhalali wowote katika nchi inayopigania demokrasia na utawala bora kama Tanzania. Madai ya Serikali kwamba marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha vyombo vya habari na wanahabari wanaofanya vitendo vya uchochezi wanadhibitiwa ni upotoshaji uliokithiri, kwani Serikali kama mmiliki wa vyombo vya habari haina uhalali wa kudhibiti vyombo vingine inavyoshindana navyo katika soko la habari.
Ukweli ni kwamba Serikali imegubikwa na hofu ya kuumbuliwa na vyombo vya habari kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa na ufisadi. Wanahabari wasidanganyike wala kuogopa hila hizi za Serikali zinazolenga kutumia kisingizio cha kudhibiti vitendo vya uchochezi kama kichaka cha kutofanya shughuli zake kwa uwazi. Ni wakati mwafaka kwa wanahabari na wanaharakati kuunganisha nguvu zao kuikataa sheria hii kandamizi.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment