Writen by
sadataley
10:45 AM
-
0
Comments
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema kuwa anatafakari iwapo awanie urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kutokana na kuwapo kwa watu wengi hasa ndani ya CCM, wanaomtaka kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
Makamba ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM alisema: “Kwanza ni kweli kwamba kuna ushawishi kuhusu suala hilo kutoka kwa vijana walioko nje na ndani ya chama, wanataaluma, baadhi ya wazee na watu wengine iwe kwa makundi au mtu mmoja mmoja wamekuwa wakinishawishi kugombea kwa muda sasa.”
Aliongeza: “Mwanzoni sikuona uzito sana, yaani sikuzingatia sana, lakini kwa kadiri siku zinavyokwenda ni kwamba ushawishi umekuwa mkubwa na hivyo niseme ni jambo ambalo sasa ninalitafakari kwa kina”.
Alisema ikiwa ataamua kuwania urais, atafanya hivyo wakati mwafaka kwa kuzingatia utaratibu utakaowekwa na chama hicho, lakini akasema kwa sasa si wakati wake. Makamba alikuwa akijibu hoja za gazeti hili lililotaka ufafanuzi wake kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba ameanza harakati za kuusaka urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Gazeti hili lilidokezwa kuwa hatua yake hiyo imemwingiza katika mvutano usio rasmi na wanasiasa ambao tayari wameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini, wakiwamo wale wa kambi ya urais aliyokuwa akidaiwa kuwa mmoja wao.
Awali iliaminika kuwa Makamba alikuwa katika kambi ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini wachambuzi wa masuala ya kisisa wanasema ‘katika siku za karibuni mwenendo wake unaashiria kwamba si mmoja wa wanaomuunga mkono kiongozi huyo, bali ni mtu mwenye mipango yake binafsi ya kisiasa”.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema mwenendo wa Makamba umewakasirisha baadhi ya wanasiasa hususan wanaomuunga mkono Lowassa ambao mara kadhaa wamesikika hadharani wakimlalamikia kwamba ni msaliti.
Hata hivyo, Makamba katika maelezo yake anasema hajawahi kuwa katika kundi lolote la kumuunga mkono mtu yeyote kwani yeye haamini katika makundi. “Ninaamini katika kundi moja, nalo ni CCM,” alisema.
Aliongeza: “Kwa hiyo mtu yoyote akinikasirikia kwa sababu zozote zile za kisiasa nitamshangaa maana sijawahi mahali popote na kwa namna yoyote kujitanabaisha kwamba mimi nipo kwenye kundi fulani, au kundi la mtu yeyote.”
Sababu za mashaka
Miongoni mwa nyedo zinazotiliwa shaka za mwanasiasa huyo ni hatua yake ya kushiriki katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) uliofanyika Zanzibar ambako pamoja na mambo mengine aligawa simu zaidi ya 100 aina ya Samsung Galaxy kwa wajumbe wa mkutano huo.
Imethibitika kwamba mpango huo ulikuwa ni wake binafsi na haukuwashirikisha waliokuwa wakiamini kwamba wako naye katika harakati za kumuunga mkono Lowassa.Tukio jingine ni lile la vijana waliojitambulisha kuwa viongozi wa vyuo vikuu nchini kutangaza katika mkutano wao mjini Morogoro kwamba watamwomba Makamba awanie urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, kutokana na kile walichodai kwamba ni matokeo ya kura walizopiga baina ya kiongozi huyo na viongozi wengine vijana; John Mnyika na Zitto Kabwe wa Chadema.
Wapinzani wake wanaamini kwamba tamko la vijana hao zilikuwa mbinu binafsi za Makamba kutaka kuonyesha kwamba naye anakubalika na pengine maandalizi ya kujiengua rasmi kutoka katika kambi yake ya awali.
Wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Makamba alikuwa Butiama mkoani Mara ambako mbali na kushiriki Ibada ya kumwombea Baba wa Taifa, pia alikuwa mgeni rasmi katika kongamano la kumuenzi kiongozi huyo.
Kuhusu baadhi ya makada wenzake kukasirishwa na mwenendo wake kisiasa, Makamba alisema: “Hata mimi nimesikia kama wewe unavyosema umesikia, inawezekana wanakasirishwa na mvumo maana ndani ya chama chetu watu wanazungumza sana, tena hadharani kwa hiyo katika mazingira hayo taarifa zinaweza kumfikia yeyote kama zilivyokufikia wewe”.
Alitetea hatua yake ya kugawa simu kwenye mkutano wa UVCCM akisema alikuwa akitimiza ahadi aliyoitoa wakati wa semina ya vijana hao Februari mwaka huu mjini Dodoma, pale walipomuomba kuwasaidia ili waweze kutekeleza matakwa ya ushauri wake wa kukitetea CCM katika mitandao ya kijamii.
“Mimi kwa nafasi yangu nikiwa Naibu Waziri wa masuala ya teknolojia, nikiombwa kusaidia lolote katika eneo langu ndani ya chama sioni tatizo ilimradi niwe na uwezo nalo, kwa hiyo nilitimiza ahadi yangu tena kwa uwazi sikufanya kwa kificho,”alisisitiza.
Makamba ni mwanasiasa wa tatu kijana kutajwa kuwa huenda akawania urais, wengine wakiwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Wengine ambao wameishaonyesha nia ya kuutaka urais ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Lowassa.
Vita ya urais imekuwa ikikiumiza CCM, ambapo Makamu Mwenyekiti wake (Tanzania Bara), Philip Mangula aliwahi kukaririwa akiwaonya makada wa chama hicho ambao wameanza kupiga mbio za kuusaka uongozi huo kuwa hawatavumiliwa, kwani harakati hizo zimekuwa kichocheo cha mgawanyiko ndani ya chama.
No comments
Post a Comment