Writen by
sadataley
11:07 AM
-
0
Comments
Na Patricia Kimelemeta na Raymond Kaminyoge
Dar es Salaam. Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imebaini mtandao wa ufisadi unaoshirikisha wakurugenzi 70 wa halmashauri mbalimbali hapa nchini ambao wanashirikiana na baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Kitengo cha Hazina.
Baadhi ya halmashauri hizo ni pamoja na Wilaya ya Monduli, Arusha, Mwanza, Mbeya na Ilala.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajab Mohamed Mbarouk alisema keshokutwa atataja majina ya wakurugenzi hao ili wananchi waweze kuwafahamu.
Mbarouk alisema kuwa Tanzania Bara ina halmashauri 134, kwa hiyo ina maana zaidi ya nusu ya wakurugenzi wanajihusisha na mambo hayo.
“Baadhi ya wakurugenzi hao walihamishwa kwenye vituo vyao vya kazi kutokana na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali, lakini bado wanajihusisha na mambo haya,” alisema Mbarouk.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo imepanga kukutana kesho na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia ili kuzungumzia suala hilo.
“Kuna zaidi ya wakurugenzi 70 wako kwenye mtandao wa ufisadi kwa kushirikiana na watendaji wa Hazina na Tamisemi, jambo ambalo limesababisha halmashauri zao kupata hati chafu kwa miaka mitano mfululizo,”alisema Mbarouk.
Aliongeza wakurugenzi hao wamekuwa wakishirikiana na wahasibu wao katika kutumia vibaya fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri zao.
Akitolea mfano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe ambapo halmashauri yake imefanya vibaya katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini hajachukuliwa hatua na badala yake amekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.
Alisema mbali na halmashauri hiyo, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Rhoda Nsemwa ambaye alisimamishwa kazi kutokana na tuhuma za ufisadi, lakini bado anaendelea kupata mshahara na stahiki zake kama mtumishi aliye kazini.
“Tumeshangaa kuona kuwa, aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo bado anaendelea kulipwa mshahara, kodi ya nyumba na marupurupu mengine kama ofisa aliye kazini wakati ana kesi ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali,” alisema.
Alibainisha kamati hiyo pia imebaini kuwa Takukuru inajihusisha moja kwa moja na vitendo vya rushwa, kutokana na kupotosha ukweli wa taarifa za watuhumiwa na kuchelewesha kuwasilisha jalada mahakamani.
“Ukiangalia kesi zilizoko mahakamani ambazo upelelezi wake bado unaendelea utaona wazi kuwa Takukuru ni miongoni mwa watu wanaopokea rushwa, jambo ambalo limesababisha kuchelewesha upelelezi au kupindisha ukweli,” aliwatuhumu.
Akizungumzia tuhuma hizo, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema, “Hazina kuna taratibu na sheria kuhusu matumizi ya fedha na kama jambo hilo limefanyika kweli ni wazi kuwa litakuwa kinyume na sheria na taratibu zilizopo.”
Alisema licha ya kuwa mpaka sasa hajasikia malalamiko yoyote, aliahidi kufuatilia jambo hilo ili kubaini ukweli na kwamba kama kuna mtu atabainika atachukuliwa hatua stahiki. Alisema, “Ngoja tufuatilie ili kujua ukweli.”
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Kassim Majaliwa aliomba atafutwe leo kwa maelezo kuwa atakuwa ameshapata maelezo ya kutosha kuhusu tuhuma hizo.
“Sijajua hizo halmashauri ni zipi, pamoja na idara ambazo zipo chini ya wizara hii, ngoja kwanza nizungumze na wahusika ambao pia najua watanieleza kilinachoendelea, nitafute kesho (leo) nitatoa ufafanuzi wa kina,” alisema Majaliwa.
Kamati yawabana Mambo ya Nje
Katika hatua nyingine; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), imemwagiza CAG kufanya ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa hasa katika uendeshaji wa mikutano ya kimataifa.
Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Gaudence Kayombo alisema jana alipokutana na viongozi wa wizara hiyo kuwa kuna matumizi makubwa ya fedha katika uendeshaji wa mikutano ya kimataifa.
“Kamati itamwandikia CAG, afanye ukaguzi maalumu ili kubaini utata unaoonekana katika matumizi ya fedha ya wizara hiyo hasa kwenye eneo la mikutano,” alisema Kayombo.
Kayombo alisema kutokana na utata huo, kamati imeona haiwezi kuijadili ripoti hiyo ya fedha ya mwaka 2012/13 hadi CAG atakapofanya ukaguzi maalumu.
Aidha, Kayombo aliwataka viongozi hao wataje gharama za Ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliojengwa kwa mkopo na msaada wa Serikali ya China, lakini Katibu Mkuu wa wizara hiyo, John Haule alisema ataitaja baadaye baada kujiridhisha.
“Tunataka kufahamu gharama za ujenzi wa jengo hilo, vifaa vilivyosamehewa kodi ili kamati iweze kujua, kwa sababu hadi sasa haieleweki umegharimu kiasi gani,” alisema Kayombo.
Hata hivyo, alisema asilimia 46 ya gharama za ujenzi wa jengo hilo ni msaada wa Serikali ya China huku asilimia 54 ikiwa ni mkopo.
Chanzo:http://www.mwananchi.co.tz
No comments
Post a Comment